Wafanyabiashara walalama kupigwa danadana maeneo yao ya biashara

Tabora. Baadhi ya wafanyabiashara wa mbogamboga wanaofanya shughuli zao kwenye soko la Machinga Tabora mjini, wamelalamikia ugawaji wa maeneo bila kufuata utaratibu  baada ya kufanyiwa maboresho.

Wanadai maofisa kutoka halmashauri wameyagawa maeneo kwa watu ambao hawakuwepo kwenye mpango huo, huku wao kila siku wanaambiwa wasubiri.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Agosti 18, 2024, Mwasi Juma anayefanya biashara kwenye soko hilo, anadai awali Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedit Katwale alifika sokoni hapo na kukuta mazingira machafu, akawapa eneo la muda la kufanyia biashara kwa ahadi ya ukarabati wa eneo lao la awali ukikamilika watarejeshewa maeneo yao, kitu ambacho hakijafanyika mpaka sasa.

“Baada ya Mkuu wa wilaya kuja hapa tulimuomba atusaidie kurekebisha soko letu maana lilikua na mazingira mabaya, wakati huo tulishajichanga sisi wafanyabiashara tukanunua mabati na michango mingine, mkuu wa wilaya akasema anatupeleka Kachoma tufanye biashara kwa muda, baada ya ujenzi kuisha kila mmoja atarudi kwenye eneo lake cha ajabu ujenzi umeisha wameletwa watu wapya.”

“Tunaomba Serikali iingilie kati kuhakikisha maeneo yetu tunapewa kama ilivyokua mwanzo” amesema Juma.

Hata hivyo, Mwananchi Digital imezungumza na Katwale aliyesema kuwa kumekuwepo na watu ambao si waaminifu wanahujumu kazi hiyo kwa kutaka kuwaingiza watu ambao hawakuwepo sokoni hapo tangu awali.

“Nia yetu ni kuona mfanyabiashara anafanya kazi zake kwa uhuru bila kubughudhiwa, kilichotokea kuna baadhi ya viongozi wa hao wafanyabiashara wadogo walipanga kuhujumu hili zoezi kwa kutaka kuwaingiza wafanya biashara wengine ambao sio halali katika maeneo ya wafanyabiashara tunaowajua,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

 “Tungependa kuona kila mmoja akifanya biashara, lakini kila mfanyabiashara ambaye tunamtambua tangu mwanzo tutahakikisha anapata eneo sokoni hapa kwa ajili ya kufanyia biashara na hakuna mtu atakayekosa kama wengine wanavyodai na hakuna danadana,” amesema.

Naye Sabina James mfanyabiashara sokoni hapo anasema yeye ni miongoni mwa waanzilishi wa soko hilo, lakini anashangaa meza yake tayari ameshauziwa mfanyabiashara mwingine.

“Nilikua na mtaji wa Sh1.5 milioni zote zimepotea baada ya kuhamishwa hamishwa kufanya biashara, binafsi nimechangia Sh530,000 ili tujenge soko hili cha ajabu meza tulizotarajia kupewa wameuziwa watu wengine ambao hawakuwepo hapa, tunataka mkuu wa wilaya aje atupe maeneo yetu kama alivyotuondoa mwanzo na kuahidi kuturejesha,” amelalama mfanyabiashara huyo.

Related Posts