YANGA imecheza dakika 90 za kwanza katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Vital’O licha ya tambo na kejeli zilizotolewa mapema na Warundi waliodai Vijana wa Jangwani ni wadogo, hivyo watanywewa kama ‘supu’ mapema tu uwanjani.
Hata hivyo, kile kilichoonekana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kilidhihirisha Yanga ilikuwa ni kubwa zaidi mbele ya Vital’O na hata ushindi huo wa 4-0 ni kama walijiamulia tu, ungekuwa zaidi ya hapo.
Vital’O waliokuwa wenyeji wa mchezo huo jijini Dar es Salaam kutokana na kukosa uwanja wenye viwango bora nchini kwao Burundi, walionekana kucheza vyema mwanzoni mwa mchezo, lakini walipobadilishiwa gia wakatepeta na kumfanya msemaji wa klabu hiyo, Arsene Bucuti ashindwe kuitimiza ahadi yake ya kujiuzulu endapo watafungwa.
Licha ya Vital’O kuwa mwenyeji ikihitaji zaidi ushindi, katika mchezo huo, iliamua kujilinda kwa kupaki basi muda mwingi wa mchezo ikihofia mvua ya mabao kutoka kwa Yanga iliyotoka kuifyatua Azam kwa mabao 4-1 kwenye fainali ya michuano ya Ngao ya Jamii, siku chache tu tangu ilipoipasua Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa mabao 4-0 katika ya michuano maalumu ya Toyota International Cup.
Vital’O ilitumia mfumo wa kucheza kwa mashambulizi ya kushtukiza ikiwatumia viungo wawili wa pembeni Hamisi Hererimana na Dieume Eboma kuwahisha mashambulizi ya timu hiyo ambayo hata hivyo yalikuwa yakiishia miguuni mwa mabeki wa Yanga wakiongozwa na nahodha Bakar Mwamnyeto.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika, Vital’O ilipiga shuti moja pekee lililolenga lango dakika ya 25 likipigwa na mshambuliaji Kessy Nimbona ambalo hata hivyo lilikiwa jepesi zaidi kwa kipa Djigui Diarra.
Yanga kushinda mabao 4-0 ni makosa yao tu, kwani ingeweza kutengeneza ushindi mkubwa zaidi kama wachezaji wa timu hiyo wangekuwa na utulivu wa kutumia nafasi ilizotengeneza.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara wanatakiwa kujiimarisha zaidi katika kutumia nafasi, kwani hilo linaweza kuwatibulia kwenye mechi ambazo hazitakuwa na utengenezaji wa nafasi za kutosha huko mbele kwa mechi za mtoano kama hizi.
Kocha wa Yanga, anaendelea kufurahia upana wa kikosi chake ambapo juzi alikuwa na mabadiliko matatu makubwa akiwaanzisha nahodha mkuu, beki Bakari Mwamnyeto akichukua nafasi ya Ibrahim Job aliyeanzishwa benchini.
Mbali na Mwamnyeto, aliwaanzisha pia beki wa kushoto Nickson Kibabage aliyechukua nafasi ya Chadrack Boka ambaye hakucheza mechi hiyo kutokana na kuchelewa usajili wa mechi hizo mbili za kwanza dhidi ya Vital’O huku pia akianza na Clatous Chama kwa mara ya kwanza akichukua nafasi ya Pacome Zouzoua.
Licha ya mabadiliko hayo, bado Yanga ilitulia na kucheza mpira mkubwa, ikipata matokeo hayo ambayo yatawapa nguvu kubwa kuelekea mechi ya marudiano itakayopigwa wikiendi hii Agosti 24 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Wakati mashabiki wa upande wa pili wakiombea staa huyo wa zamani Msimbazi, Clatous Chama apotee ndani ya kikosi cha watani wao, mwenyewe ameendeleza makali yake akitoa asisti katika baadhi ya mechi kama ile ya Azam alipompasia Clement Mzize na juzi kuweka chuma chake cha kwanza akiwa na uzi wa njano.
Ndani ya Yanga, bado Chama kuna aina ya soka analihitaji kulizoea na wenzake ambapo mdogomdogo ameendelea kufanya kitu tofauti huku akionyesha kiwango kikubwa cha utulivu.
Bao hilo la asisti imemfanya Chama aendelee pale alipoishia msimu uliopita katika michuano hiyo alipoifungia Simba bao na kuasisti ikiishia robo fainali na kuboresha rekodi ya mabao aliyonayo CAF.
Mshambuliaji mpya wa Yanga Prince Dube ameendelea kuwa na mwanzo mzuri ndani ya timu hiyo akifunga bao lake la nne lakini hili la juzi likiwa na rekodi yake nzito akiwa ndani ya jezi za Yanga.
Hilo linakuwa bao lake la kwanza la mashindano tena la kwanza katika historia ya Ligi ya Mabingwa akishiriki mara ya kwanza tangu atue nchini 2020.
Ukiacha hayo mshambuliaji huyo amekuwa akijiweka kwenye maeneo sahihi kufunga na akipata nafasi hataki kufanya makosa hatua ambayo itaendelea kumpa alama za kuwa mshambuliaji kinara atakayepata nafasi ndani ya kikosi cha kocha Miguel Gamondi.
Yanga ina kikosi bora zaidi msimu pengine kushinda msimu uliopita, hatua hiyo inawapa presha kubwa mpaka wachezaji wa timu hiyo ambao wanapopata nafasi wanajikuta na deni la kutakiwa kufanya kitu tofauti ili kulinda kuaminiwa na benchi la timu yao.
Kwa mwenendo huu, Yanga ina nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya pili ya awali.
Yanga inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya sio tu kuulinda ushindi wa mechi ya juzi, bali pia kushinda mechi ya marudiano dhidi ya Vital’O Agosti 24 hata hivyo kuna kitu mabingwa hawa wa soka Tanzania wanatakiwa kukifanya.
Timu hiyo ya Wananchi inatakiwa kuhakikisha inashinda vizuri wakati huo huo ikiutumia mchezo huo kuendelea kujiimarisha kwa kutatua changamoto ambazo wameziona kwenye mechi iliyopita, lakini ikitambua kuwa itaendelea kuvuna mamilioni ya fedha za bonasi maarufu kama ‘Goli la Mama’ baada ya juzi tu kuchukua Sh20 milioni kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushindi huo wa 4-0.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema mchezo huo wangeweza kushinda kwa ushindi mkubwa zaidi lakini kitu muhimu kwake ni kuhakikisha kikosi hicho kinafuzu kwenda hatua inayofuata.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kushinda mchezo huu lakini ni mechi ambayo nadhani tungeweza kushinda kwa mabao mengi, kulingana na nafasi ambazo tumezitengeneza, kwangu mimi kitu muhimu ilikuwa kupata ushindi na kufuzu, moja limetimia lakini bado hatujafuzu tutatakiwa kujipanga kwa mchezo wa marudiano,” alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Kocha wa Vital’O Feruzi Haruna alisema timu yake imepoteza mchezo huo kutokana na kuzidiwa uzoefu na wenzao wa Yanga ambao waliwaadhibu kwa makosa waliyoyafanya.
“Timu yangu ina wachezaji wachanga sio wakomavu kama utawalinganisha na wale wa Yanga, tumepoteza mechi ya kwanza tutakwenda kujirekebisha kwa mechi ijayo,” alisema.