Askari JWTZ, Magereza kortini madai ‘waliotumwa na afande’

Dodoma. Watu wanne akiwemo askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza wanaotuhumiwa kumbaka kwa kikundi na kumlawiti binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kusomewa mashtaka mawili.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu, Agosti 19, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi, Zabibu Mpangula na kusomewa mashtaka hayo ambayo wameyakana.

Waliofikishwa mahakamani ni askari wa JWTZ MT.140105 Clinton Damas, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Lord Lema na Nickson Jackson.

Kesi hiyo imesikilizwa katika chemba ambayo inaruhusu kuingia washtakiwa pekee.

Akizungmza nje ya Mahakama, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Makao Makuu, Renatus Mkude amesema washtakiwa wataendelea kuwa rumande kutokana na unyeti wa kesi hiyo pamoja na maombi ya upande wa mashtaka ya kuzuia dhamana.

Amesema kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa siku nne mfululizo kuanzia kesho Jumanne Agosti 20 hadi 23, mwaka huu, ili kulipeleka haraka shauri hilo ambalo limevuta hisia za watu wengi nchini.

Hata hivyo, Mkude hakutaja jina la binti aliyefanyiwa vitendo hivyo, ili kulinda utu wake mbele za jamii ambaye ametambulika kwa jina la XY.

“Sasa kama ilivyo kwa mfumo wetu wa kisheria hapa nchini, kwa mujibu wa katiba na kwa mamlaka aliyonayo Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatua zilichukuliwa, shauri hili lilipelelezwa na kama ambavyo mlipata taarifa awali kwenye vyombo vya chunguzi kwamba watuhumiwa wanne walitiwa nguvuni ambao kwa sasa ni washtakiwa,” amesema na kuongeza;

“Leo wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka mawili moja ni kubaka kwa kundi, lingine ni kumwingilia huyu binti kinyume na maumbile, wamekana tuhuma hizo… kwa mujibu wa sheria ilivyo tutaendelea na taratibu nyingine za usikilizaji.”

Amesema lingine ambalo limefanyika ni kumlinda binti aliyefanyiwa tukio hilo na hata kwenye hati ya mashtaka jina lake halikutajwa, bali alijulikana kwa jina la XY, ikiwa ni njia mojawapo ya kulinda mashahidi ili asipate fedheha au kudhalilika kwa namna yoyote ile.

Amesema suala hilo pia lipo kimataifa kama kuna mazingira ya kuwalinda mashahidi.

Mkude amesema kutokana na usalama wa watuhumiwa na mambo mengine yanayoendelea, Mahakama imekubali ombi la upande wa mashtaka la kuzuia dhamana, hivyo wataendelea kuwa ndani wakati shauri lao linaendelea kusikilizwa.

Pia amesema kutokana na upekee wa shauri hilo, limepangwa kusikilizwa mfululizo kuanzia kesho mpaka Ijumaa, ili haki itendeke kwa wakati.

“Uzuri ni kwamba nchi yetu inafuata mfumo wa sheria kwa hiyo panapotokea matatizo kama haya kuna haki ya washtakiwa na ya wahanga, kwa sababu jambo limefikishwa mahakamani, watu wawe watulivu waendelee kusikiliza na waamini haki itatendeka kadri ambavyo sheria inataka,” amesema.

Walivyofikishwa mahakamani

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani saa 9:25 alasiri chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha mbalimbali waliokuwa kwenye msafara wa magari sita.

Wakati wa kuingia na kutoka mahakamani, mtuhumiwa namba moja, MT.140105 Clinton Damas, maarufu kama Nyundo, alikuwa amedhibitiwa na askari wawili wenye silaha, huku wenzake watatu wakiwa nyuma yake wakiongozwa na askari wengine zaidi ya 10 waliokuwa wamevaa sare na wengine wakiwa wamevaa kiraia.

Pia waandishi wa habari walizuiwa kuingia kwenye chumba walichosomewa mashtaka kwa sababu hawakusomewa kwenye Mahakama ya wazi, bali walikuwa chemba.

Kabla ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani, vilio vya kudai haki itendeke viligubika tukio hilo, baada ya wananchi kuonyesha wasiwasi wa kuyumbishwa kwa hatua za kisheria dhidi ya waliohusika.

Hofu na wasiwasi wa wananchi, wakiwemo watu maarufu na wadau wa haki za binadamu ulitokana na kile walichokiandika katika mitandao ya kijamii kuwa kuna namna mamlaka zinachelea kuchukua hatua.

Wasiwasi zaidi ulijengwa na kauli ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya alipozungumza na Mwananchi jana Jumapili Agosti 18, 2024, akisema binti huyo alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.

“Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.”

“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo,” alisema Kamanda Mallya.

Ingawa Jeshi la Polisi leo asubuhi lilitoa taarifa ya kumuondoa katika wadhifa huo Kamanda Mallya na kumhamishia Makao Makuu, maswali lukuki yameulizwa na wadau kuhusu kauli hiyo, huku wengine wakiibua kampeni ya kupinga mwenendo wa upelelezi wa tukio hilo.

Miongoni mwa kampeni zinazoshuhudiwa katika mitandao ya kijamii ni ile yenye picha inayoonyesha vidole vitano na taswira ya binti chini yake, ikiwa na maneno ya ‘Enough is Enough Tunadai haki kwa binti aliyebakwa na kulawitiwa.’

Katika tamko lao la pamoja, mashirika yanayotetea haki za msichana na mtoto yalitaka haki ya binti huyo isiishie kutendeka tu, bali ionekane ikitendeka.

“Jeshi la Polisi lina maslahi katika kesi hii, sababu mtuhumiwa mkuu ni mmoja wao, tunapendekeza kuwepo kwa uchunguzi huru ili kutokuingilia ushahidi au kupindisha ukweli wakati shauri linaendelea,” yalieleza mashirika hayo.

Rai nyingine iliyotolewa na mashirika hayo kwa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha usalama wa binti huyo, huku watuhumiwa wote wafikishwe mahakamani, wakiwemo wale ambao bado hawajakamatwa.

Wito wa haki itendeke, ulitolewa pia na Wabunge wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), wakisisitiza waliohusika wafikishwe mahakamani haraka.

Hatua hizo dhidi ya waliohusika, wametaka zimhusishe pia anayedaiwa kuwatuma ‘Afande’ ambaye katika kipande cha video iliyosambaa mitandaoni alitajwa.

“Tunataka haki itendeke kwa binti aliyebakwa na kulatiwa na wahusika wote wafikishwe mahakamani haraka, akiwemo anayetuhumiwa kuwatuma vijana hao kubaka na kulawiti endapo itathibitika,” walisema wabunge hao kupitia taarifa yao ya pamoja.

Pamoja na wito huo, walimpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kwa hatua za kuondolewa kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya.

Maswali tata LHRC, Madeleka

Katika taarifa yake mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amehoji maswali 11, likiwemo zipi taarifa sahihi kati ya zilizotolewa na jeshi hilo makao makuu, Wizara ya Mambo ya Ndani au makamanda wa polisi wa mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.

Maswali hayo ni pamoja na zipi ni taarifa sahihi kutoka kwa jeshi hilo, za makao makuu, Wizara ya Mambo ya Ndani au makamanda wa Polisi wa Mikoa  wa Dar es Salaam na Dodoma.

Pili, je watuhumiwa ni maofisa wa jeshi lipi. Tatu, watuhumiwa katika tukio hilo walikuwa watano, je huyo mwingine ni nani na yupo wapi. Nne, binti alilazimishwa kumuomba msamaha ‘afande’ je afande ni nani.

Tano, wanajiuliza kama mwathirika yupo salama katika mikono ya wanaomhukumu kuwa ni kama alikuwa anajiuza. Sita, binti huyo kuwa katika mikono ya polisi hakutaathiri upatikanaji wa haki na ushahidi na je mtu kuwa kama anajiuza inahalalisha kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kubakwa.

Saba, vipi binti huyo kuwa mikononi mwa polisi, je hakutaathiri upatikani wa haki na ushahidi. Nane, Je kwa vitendo hivi jeshi la polisi linasimamia maslahi ya nani. Tisa, je kuwa mlevi na mvuta bangi ni kinga ya uhalifu? Kumi, kwa kutajwa Afande bila kusema ni afande wa jeshi gani je polisi hawana mgogoro wa maslahi na shauri hili na swali la mwisho LHRC wamehoji taarifa ya Polisi ya Agosti 9 ilisema upelelezi umekamilika, na leo ni Agosti 19, je lini shauri hili litapelekwa mahakamani?

Maswali ya kituo hicho, yalifuatiwa na aliyoulizwa na Wakili Peter Maadeleka alipozungumza na Mwananchi, aliyehoji, licha ya madai ya polisi kuwa, binti huyo alikuwa anafanya biashara ya ngono ‘ukahaba’ Madeleka amehoji Je, hilo linahalalisha kubakwa au kulawitiwa?

Swali lingine lililoibuliwa na wakili huyo ni ukahaba alionao binti huyo unamnyima haki ya uraia, kulindwa na kuhakikishwa usalama wake na vyombo vya dola?

Kadhalika, amehoji kilichoelezwa na Kamanda Mallya kuwa waliohusika ni walevu na wavuta bangi,je sifa hizo zinawapa uhalali wa kutenda tukio hilo na hawaruhusiwi kukamatwa?

RPC Dodoma alivyoondolewa

Kutokana na mijadala hiyo, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa iliyotiwa saini na msemaji wake, David Misime ya kumhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya na nafasi yake kurithiwa na George Katabazi.

Sambamba na kuondolewa katika nafasi hiyo na kurudishwa Makao Makuu, taarifa hiyo pia iliyakana maneno ya kamanda huyo, likisema si msimamo wa chombo hicho cha dola.

“Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa kuwa kauli hiyo kama inavyoonekana kwenye hicho kichwa cha habari siyo msimamo wa Jeshi la Polisi na kwamba kauli sahihi ya Jeshi la Polisi ni kama zilivyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi kwa umma Agosti 4, 6 na 9, 2024,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, jeshi hilo liliomba radhi kwa kila mmoja aliyeguswa na kuchukizwa na kauli hiyo inayosambaa kwenye vyombo vya habari wakati ufuatiliaji ukifanyika kupata usahihi wake.

Related Posts