Azam FC imeanza vyema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua za awali baada ya kuichapa APR FC ya Rwanda bao 1-0 Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Timu mbili kutoka Tanzania Azam FC na Yanga zinawakilisha kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kumaliza nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambapo Yanga jana ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote mbili hazikuruhusu bao lolote, lakini dakika ya 55 Azam ilipata penalti baada ya kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuchezewa madhambi kwenye eneo la hatari na mkwaju huo kufungwa na Jhonier Blanco.
Azam ambayo ndio ilikuwa mwenyeji wa mchezo huo, iliingia kwenye mchezo kwa kasi lakini uimara wa APR uliwazuia kupata mabao mengi kwenye mechi hiyo.
Kwa ushindi huo mwembamba utawafanya Azam kuwa na kazi ya ziada kwenye mchezo wa pili wa kufuzu raundi ya kwanza ambao watakuwa ugenini Agosti 24, Uwanja wa Amahoro nchini Rwanda kulinda ushindi huu.
Kama Azam itafanikiwa kupita raundi hii itakutana na mshindi kati ya Uhamiaji ya Zanzibar na Pyramids ya Misri, mechi inayopigwa muda mchache ujao.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha tangu Azam ianze kushiriki mashindano ya Klabu Afrika 2013 ikicheza Kombe la Shirikisho haijafanikiwa kucheza hatua ya makundi.