BAO moja la Clatous Chama katika ushindi wa mabao 4-0 ambao Yanga iliupata dhidi ya Vital’O ya Burundi, Jumamosi iliyopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika, limemfanya kuandika rekodi mbili huku akiboresha nyingine ya tatu.
Chama alifunga bao dakika ya 68 akiunganisha mpira uliogonga mwamba na kurudi uwanjani ambao ulitokana na shuti lililoupigwa na Stephane Aziz Ki.
Kwa kufunga bao hilo, Chama sasa amefikisha mabao 22 kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na anazidi kutamba kwenye 10 bora ya wafungaji bora wa muda wote wa mashindano hayo.
Rekodi ya kwanza Chama aliyoiweka ni ya kuwa mchezaji pekee aliyecheza Ligi Kuu Bara kufunga idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Awali alikuwa sawa na Mbwana Samatta aliyefumania nyavu mara 21 lakini kufunga bao juzi kumemfanya aandike rekodi mpya.
Chama pia ameandika rekodi yake mwenyewe ya kuwa mchezaji anayeshika nafasi ya saba kwa kufunga idadi kubwa ya mabao katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka ile ya nane aliyokuwepo awali.
Anayeongoza chati ya ufungaji bora wa muda wote kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni nyota wa zamani wa TP Mazembe na timu ya taifa ya DR Congo, Tresor Mputu ambaye amefunga mabao 39.
Kiungo huyo mshambuliaji pia ameboresha rekodi ya kuwa Mzambia aliyefunga mabao mengi Ligi ya Mabingwa Afrika. Mchezaji wa Zambia anayemfuatia Chama ni Rainford Kalaba aliyepachika mabao 13 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kwa sasa amestaafu kucheza soka.