Moshi. Gharama kubwa za matibabu zimetajwa kuwa moja ya changamoto inayowafanya wananchi wengi hususani wa maeneo ya vijijini, kushindwa kufuata huduma za matibabu za kibingwa.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Agosti 19, 2024 wakati wa kambi ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali iliyotolewa bure na madaktari kutoka Hospitali ya kanda ya Kaskazini KCMC, Mawenzi na TPC, katika eneo la Kahe, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya siku ya afya ya familia inayofadhiliwa na Club ya Rotari ya Mwika na Moshi.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma wamesema gharama kubwa za matibabu zimekuwa kikwazo kwao, kwenda hospitali kupima na kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo yasiyoambukiza hali ambayo inasababisha kugundulika ugonjwa ukiwa katika hatua mbaya.
Bakari Mohamed, mkazi wa Kijiji cha Oria Kata ya Kahe Magharibi amesema wananchi wamekuwa wakishauriwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini kama wana maradhi yanayowasumbua na kupata matibabu mapema, lakini wengi wanashindwa kufanya hivyo kutokana na kushindwa kumudu gharama.
“Huduma za uchunguzi wa afya kwa wananchi ni jambo la msingi sana kwani watu tunatembea lakini ni wagonjwa, na idadi hii kubwa ya wananchi waliojitokeza hapa, ni ishara kuwa watu wengi ni wagonjwa lakini hawawezi kwenda hospitali kwa sababu ya gharama za matibabu,” amesema na kuongeza:
“Hapa leo wapo watu wamekuja na baada ya kufanyiwa uchunguzi wamegunduliwa kumbe ni wagonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine, kwa sababu hata mimi nimegundulika kuwa na shinikizo la damu na sikuwa nafahamu kwa sababu sijawahi kufika kwa wataalamu kufanyiwa uchunguzi.”
Naye Kadria Salvia mkazi wa Kahe, ameomba wataalamu wa afya kutoa huduma hizo mara kwa mara, ili wananchi waweze kusaidiwa kutokana na wengi kutaabika kwa kukosa fedha za kuwafikia wataalamu hao hospitalini.
“Huduma zinazotolewa hapa ni nzuri wananchi wengi wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi na hata kupewa ushauri wa kitaalamu. Tunaomba huduma kama hizi zitolewe mara kwa mara hasa katika maeneo ya vijijini kwani wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kwenda hospitali kuonana na wataalamu kutokana na kushindwa kumudu gharama”
Dk John Lugata kutoka idara ya wanawake na afya ya uzazi amesema katika kambi hiyo wamebaini wananchi wengi, hushindwa kufuata huduma za kibingwa na bobevu kutokana na kutomudu gharama hali inayosababisha wafike hospitali katika hatua za mwisho.
“Hapa tumewaona kinamama ambao tayari waligundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi na walianza matibabu sehemu, lakini walikuwa wamekosa kufuatilia maendeleo yao na wakawa hawana mwendelezo mzuri,” amesema Dk Lugata.
Amesema baada ya kuzungumza nao, wamedai wanaogopa gharama za matibabu hawawezi kuzimudu na hawana bima za afya.
Daktari huyo amesema hali hiyo inawafanya wawe wanazunguka kwenye hospitali ndogo na kufanya vipimo vya awali na kukosa mwendelezo wa huduma za kitaalamu zaidi.
“Tumegundua wananchi wengi waliokuja hapa hawana bima za afya na hawawezi kumudu gharama za matibabu kutokana na vipato vyao hivyo matokeo yake wanaogopa kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi,” amesema.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kambi hiyo, Baraka Max amesema wanakusudia kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 2,000 na kwamba uchunguzi wanaofanya ni pamoja na uzito wa mwili, sukari, shinikizo la damu, viashiria vya saratani ya kizazi na matiti.
Amesema pia wanapima maambukizi ya virusi vya ukimwi, macho pamoja na kutoa huduma za afya ya misuli na viungo, kinywa na meno na afya ya akili.