Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura amemhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC), Theopista Mallya na nafasi yake kurithiwa na George Katabazi, huku jeshi hilo likitangaza kuwafikisha mahakamani leo watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti wa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.
Kamanda Mallya anaondolewa katika nafasi hiyo leo Jumatatu, Agosti 19, 2024, ikiwa ni siku moja baada ya kutoa kauli juu ya mwenendo wa upelelezi wa tukio hilo lililoanza kusambaa katika mitandao ya kijamii Agosti 2, 2024.
Katika kauli yake hiyo alipozungumza na Mwananchi jana Jumapili, Kamanda Mallya alisema: “Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.”
“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo,” alisema Kamanda Mallya, baada ya kuulizwa nini kinaendelea juu ya uchunguzi wa watuhumiwa hao.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limeikana kauli hiyo na kusema si msimamo wa jeshi hilo, bali kauli sahihi ni zile zilizotolewa na msemaji wa jeshi hilo kwa umma Agosti 4, 6 na 9, 2024.
Msingi wa Jeshi la Polisi kutoa taarifa hiyo ni habari iliyochapishwa na Mwananchi, Agosti 19, 2024 yenye kichwa cha habari ” RPC: Anayedaiwa kubakwa, kulawitiwa na vijana wa ‘afande’ ni kama anajiuza
Taarifa hiyo imesema kichwa hicho cha habari kimetokana na mazungumzo kwa njia ya simu na Mwandishi wa gazeti la Mwananchi.
“Vile vile, tungependa kujulisha kuwa watuhumiwa wa kesi hiyo watafikishwa mahakamani leo Agosti 19, 2024,” imeeleza.
Pia, jeshi hilo limeomba radhi kwa kila mmoja aliyeguswa na kuchukizwa na kauli hiyo inayosambaa kwenye vyombo vya habari, wakati ufuatiliaji ukifanyika kupata usahihi wake.