Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umewasilisha maboresho ambayo yamefanyika katika kanuni mbili za usalama na afya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
Maboresho hayo ambayo yamefanyika katika kanuni za Igonomia na Mazingira ya Kazi yalishauriwa kufanyika na Kamati hiyo katika kikao chake cha Oktoba 26, 2023 baada ya OSHA kuwasilisha kanuni hizo mpya mbele ya Kamati hiyo.
Wasilisho hilo limefanywa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi, ambaye alimwakilisha Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete. Katambi ameambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa na Watendaji wengine wa Wizara na Taasisi ya OSHA.
Mhe. Katambi ameiambia Kamati kuwa mapendekezo yote yaliyotolewa ikiwemo kujumuisha tafsiri ya neno Mamlaka pamoja kuondoa maudhui yanayojirudia katika kanuni hizo yameshughulikiwa ipasavyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) pamoja na Taasisi ya OSHA kwa kupokea na kutekeleza maagizo ya Kamati yake.
Aidha, ameahidi Kamati yake kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi chini yake katika kuwahudumia Watanzania kupitia ushauri na maelekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji wa Serikali.
Wakati huo huo, OSHA imekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kufanya wasilisho kuhusu utendaji wa Taasisi hiyo ambapo Mtendaji Mkuu, Bi. Khadija Mwenda, ameieleza Kamati hiyo umuhimu wa kulinda nguvukazi ya Taifa kupitia uimarishaji wa mifumo ya usalama na afya katika sehemu za kazi.
“Hadi inapofika hatua ya mtu kuajiriwa kama mfanyakazi serikali inakuwa imewekeza rasilimali nyingi sana kwake kuanzia anapozaliwa, kukua, kusoma hadi kuajiriwa hivyo inakuwa ni hasara kubwa kwa Taifa endapo mfanyakazi huyu atapata ulemavu au kupoteza maisha kabla ya kutoa mchango wake wa kutosha katika uzalishaji,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:
Akihitimisha mjadala wa wajumbe wa Kamati hiyo ya Bajeti baada ya wasilisho la OSHA, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Oran Njeza, amesema Kamati yake itaendelea kutoa ushauri unaolenga kuboresha utendaji wa Serikali ikiwemo Taasisi ya OSHA.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Zuhura Yunus, wakifuatilia mjadala katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambapo OSHA ilifanya wasilisho kuhusu utendaji wake.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akifanya wasilisho kuhusu utendaji wa OSHA katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi, akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika kikao ambacho OSHA ilifanya wasilisho kuhusu utendaji wake.