Madina awasha tena moto Uganda

MTANZANIA Madina Iddi anaendelea kuwanyanyasa Waganda baada ya kushinda tena mashindano ya wazi ya wanawake ya Uganda yaliyomalizika mwshoni mwa juma jijini Kampala.

Ushindi huu unakuja takriban mwezi mmoja baada ya Madina kushinda mashindano ya wazi ya wanawake ya Zambia akiimshinda Mganda Peace Kabasweka kwa mikwaju 21.

Ikumbukwe kuwa wakati Madina Iddi akimshinda Kabasweka nchini Zambia, Waganda, walidai mbele ya aliyekuwa Waziri wa Habari na Mawasiliano, Nape Nnaye, kuwa hawaamini kama Madina Iddi ni Mtanzania kutokana na ubora wake katika gofu.

Safari hii tena, Madina amemshinda Kabasweka katika raundi zote akiwa bora kwa mikwaju mine, kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa Jumamosi jioni.

Madina alianza mashindano haya kwa kishindo akipiga kupiga mikwaju 78  na kufuatiwa kwa karibu na Kabasweka aliyerudisha mikwaju 80. Madina alikuwa moto zaidi siku ya pili ambapo aliboresha uchezaji wake kwa kurudisha mikwaju 76 huku Kabasweka akipata mikwaju 78.

“Nashukuru Mungu nimeshinda tena kama nilivyofanya miaka ya nyuma.Hata hivyo mchezo ulikuwa mgumu siku ya kwanza ambapo nilipata mikwaju 78,” alisema Madina kutoka klabu ya Arusha Gymkhana.

Katika  mashndano ya Zambia, Madina pia aliongoza kwa siku zote tatu akimaliza mbabe wa mashindano hayo kwa kupiga jumla ya mikwaju 234 na kumchapa mzpinzani wake wa karibu Peace Kabasweka kutoka Uganda  kwa mikwaju 21 ambayo ni ushindi  mkubwa mno.

Kabasweka aliyemaliza katika nafasi ya pilI, alifanikiwa kurudisha jumla  ya mikwaju 255 katika siku zote tatu za mashindano hayo.

Madina ni mmoja wa wacheza gofu ambao wamekuwa wakishinda mara kwa mara mashindano ya gofu ya wanawake nchini Uganda.

Wengine ni Neema Olomi aliyeshinda mwaka jana na Angel Eaton ambaye sasa amekuwa mchezaji gofu wa kulipwa.

Mtanzania mwingine aliyeshiriki mashindano ya Uganda ni Aalia Somji aliyemaliza katika nafasi ya saba kwa kupiga jumla ya mikwaju 168. Alianza na mikwaju 83 na siku ya pili kurudisha mikwaju 85. Somji pia alishiriki katika mashindano ya wanawake ya Zambia na kumaliza katika kumi bora.

Related Posts