Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Songea, imebatilisha uamuzi uliomuachia huru Yassin Komba, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya ubakaji na kumpa mimba mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16, aliyekuwa akisoma kidato cha kwanza Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Mahakama hiyo imeamuru shauri hilo la jinai namba 129/2021 likaendelee na utetezi mbele ya hakimu mwingine katika mahakama hiyo ya wilaya.
Rufaa hiyo ya jinai namba 452634 ya mwaka 2022 iliyokatwa na DPP, inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru kumwachia huru Yassin katika kesi hiyo ya jinai.
Yassin alikuwa akikabiliwa na mashtaka mawili, ubakaji kinyume na kifungu cha 130 (1) na (2) (e) na 131 (1) ya Kanuni ya Adhabu na kumpa mimba mwanafunzi, kinyume na kifungu cha 60A na (3) cha Sheria ya Elimu.
Hukumu hiyo ya Mahakama Kuu imetolewa Agosti 15, 2024 na Jaji James Karayemaha aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo, ambaye baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Hellen Chuma alikubaliana nazo na kuruhusu rufaa hiyo na kuamuru shauri likaendelee na usikilizwaji.
Kupitia nakala ya hukumu ya rufaa hiyo inayopatikana kwenye mtandao wa mahakama, imeeleza mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari Mataka, alikuwa akiishi na bibi yake katika Kijiji cha Kadewele wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa katika mahakama hiyo ya chini, ilidaiwa Yassin alianza kuwa na uhusiano na mwanafunzi huyo Machi, 2021 bila kutumia kondomu na Julai 7, 2021 aligundulika kuwa mjamzito na kufukuzwa shule.
Ushahidi wa daktari aliyemfanyia uchunguzi mwanafunzi hiyo, ulionyesha alikuwa na ujauzito wa wiki 10 na siku mbili.
Aidha, ushahidi wa upande wa mashtaka ulionekana kuwa na nguvu kidogo kuishawishi Mahakama ya Mwanzo ambayo ilisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi bila shaka yoyote.
Uamuzi huo ulitokana na ushahidi wa mwathirika wa tukio hulo kudai alikuwa akifanya ngono na wavulana kadhaa, akiwemo Yassin ambapo Yassin alikuwa hana kesi ya kujibu na kuachiwa huru.
Kutokana na uamuzi huo, DPP alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, akipinga uamuzi huo na alikuwa na sababu moja kuwa Mahakama ilikosea kisheria kudharau ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa na kuamua kuwa Yassin hana kesi ya kujibu na kumuachia huru.
Aidha, baada ya kupokelewa kwa rufaa hiyo, jitihada zilifanywa ili kumpata Yassin, lakini hazikufanikiwa ambapo pamoja na juhudi za kuchapisha tangazo la hati ya wito katika gazeti la Mwananchi la Machi 13, 2024, Yaasin hakutokea ila rufaa hiyo ikaendelea kusikilizwa.
Ilielezwa kuwa Hakimu Mfawidhi alitupilia mbali shtaka hilo kwa mujibu wa kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, baada ya kudai upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha nani aliyembaka mwanafunzi huyo.
Jaji Karayemaha ameeleza baada ya kuchunguza kwa kina msingi wa kukata rufaa na ukweli uliojenga kesi ya mashtaka, ni maoni yake kuwa swali kuu ni kama upande wa mashtaka ulithibitisha kesi bila mashaka ya kutosha wakati wa kufungwa kwa kesi yake.
Ameeleza kuwa Wakili Hellen alieleza ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wa tatu uliwasilisha kesi na kufikia kiwango toshelevu ambacho kinaweza kuhalalisha madai kuwa Yassin alifanya kosa la ubakaji.
Jaji ameeleza katika kushughulikia suala hilo, ni sharti la lazima kuwa katika kesi za jinai, upande wa mashtaka una jukumu la kuthibitisha kosa kupitia ushahidi wake.
Amesema kuwa katika makosa ya ngono ushahidi bora unatoka kwa mwathirika.
“Kwa ushahidi wa shahidi wa kwanza na pili ni wazi kabisa kwamba mwathirika alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Yassin kwa karibu miezi minne, kwa hiyo alimjua na kumtambua na kama alivyosema walikuwa wakifanya mapenzi bila kondomu,” amesema Jaji.
“Ukweli huu haukubishaniwa, kwa hiyo baada ya kumaliza uchunguzi na uchambuzi wa msingi wa rufaa ya mrufani, nina maoni yanayozingatiwa kwamba, kuna sababu ya kulaumu matokeo ya mahakama ya awali,”ameongeza.
Jaji amesema kutokana na sababu hiyo, anakubali rufaa hiyo na kuamuru kesi ya jinai namba 129 /2021 ikaendelee na utetezi mbele ya hakimu mwingine mwenye mamlaka ya kuisikiliza.