Dodoma. “Mitaa imetulea, kura yangu itaiboresha.” Ni kauli inayoweza kutumiwa na wakazi kwenye mitaa, vitongoji na vijiji kuona umuhimu wa ushiriki wao kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Ni uchaguzi ambao mwaka huu mgombea pekee atapigiwa kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’. Hakuna kupita bila kupingwa na kampeni za uchaguzi zitafanyika kwa siku saba.
Kabla ya mabadiliko ya kanuni, nafasi ikiwa na mgombea pekee alikuwa akitangazwa amepita bila kupingwa.
“Endapo kutakuwa na mgombea pekee kwa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa au wajumbe wa kamati ya mtaa mpiga kura atapiga kura moja ya ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’ kwa nafasi ya mgombea husika,” kwa mujibu wa kanuni.
Pia, kanuni zinaelekeza umuhimu wa kitambulisho kwa wapiga kura, lakini zimetoa nafuu kwa wale ambao hawatakuwa na vitambulisho siku ya uchaguzi.
Kanuni zinaelekeza aina ya kitambulisho ambacho msimamizi wa kituo anaweza kumtaka mpiga kura kuonyesha ambavyo ni kitambulisho cha mpiga kura, kitambulisho cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha shule au chuo.
Vitambulisho vingine ni kitambulisho cha mifuko ya hifadhi ya jamii, leseni ya udereva au kitambulisho cha Taifa.
“Endapo mpiga kura atakuwa hana kitambulisho cha aina yoyote kati ya vilivyotajwa chini ya kanuni ndogo ya (3), lakini jina lake limo kwenye orodha ya wapiga kura iliyoandaliwa kwa mujibu wa kanuni hizi, msimamizi wa kituo atamruhusu mtu huyo kupiga kura baada ya kutambuliwa na wakazi wa eneo husika,” zimeainisha kanuni hizo.
Kanuni pia zimeainisha namna kampeni za uchaguzi zitakavyotakiwa kufanywa, ikiwamo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wilaya.
Kwa mujibu wa kanuni kampeni za uchaguzi zitafanyika siku saba kabla ya siku ya uchaguzi, kwa kila chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi kitawasilisha ratiba yake ya mikutano ya kampeni ya uchaguzi kwa msimamizi wa uchaguzi si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa kampeni.
Kanuni zinaelekeza kuwa msimamizi wa uchaguzi ataunganisha ratiba za mikutano ya kampeni zilizowasilishwa na vyama vya siasa kwa mujibu wa kanuni.
Ratiba hizo zitafanyiwa kazi baada ya maridhiano na vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kwa kuziwasilisha kama zilivyounganishwa siku tatu kabla ya kampeni kuanza kwa mkuu wa polisi wa wilaya.
“Endapo vyama vya siasa vitashindwa kuridhiana wakati wa uunganishaji wa ratiba za mikutano ya kampeni, msimamizi wa uchaguzi ataunganisha ratiba za mikutano ya kampeni na uamuzi wake utakuwa wa mwisho.”
Pia, kanuni zinaelekeza kuwa mgombea au mwakilishi wa mgombea au chama cha siasa chenye mgombea kinaweza kuitisha na kuhutubia mikutano ya kampeni kwa mujibu wa ratiba ya mikutano ya kampeni iliyoandaliwa na kuwasilishwa kwa mkuu wa polisi wa wilaya na mikutano hiyo itaratibiwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi.
Kanuni zinaeleza kuwa mkuu wa polisi wa wilaya atakuwa na wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwepo katika mikutano ya kampeni.
Pia, kanuni zinaelekeza kuwa ratiba ya mikutano ya kampeni za uchaguzi itakayowasilishwa na msimamizi wa uchaguzi kwa mkuu wa polisi wa wilaya itakuwa ni taarifa rasmi ya mikutano ya kampeni na mgombea au chama chake hakitowajibika kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa kanuni mikutano ya kampeni za uchaguzi kwa mujibu wa ratiba iliyopitishwa itaanza saa mbili asubuhi na itamalizika saa 12 kamili jioni ya kila siku ya kampeni.
Kanuni zinaelekeza endapo mgombea au chama cha siasa chenye mgombea kitakusudia kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni, kitafanya hivyo baada ya kuwasilisha kwa maandishi mapendekezo ya mabadiliko hayo kwa msimamizi wa uchaguzi na mapendekezo hayo kuridhiwa kwa mujibu wa kanuni.
“Msimamizi wa uchaguzi ataitisha kikao na vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi, ili kujadili maombi ya mabadiliko ya ratiba na mabadiliko yatakayokubaliwa yatawasilishwa kwa mkuu wa polisi wa wilaya kwa ajili ya kupatiwa ulinzi siku ya mkutano wa kampeni.”
Kanuni zinaelekeza mgombea, mwakilishi wa mgombea au chama cha siasa chenye mgombea kitatakiwa kuendesha mikutano ya kampeni za uchaguzi kwa mujibu wa ratiba na kwa kuzingatia muda uliowekwa chini ya kanuni.
Masharti kwa mujibu wa kanuni, mgombea au mwakilishi wa mgombea au chama cha siasa chenye mgombea hakitaruhusiwa kuendesha kampeni za uchaguzi kwa kutumia rushwa, kutoa maneno ya kashfa au lugha za matusi, kufanya ubaguzi wa jinsia, maumbile, ulemavu, dini, rangi, kabila au ubaguzi mwingine wa aina yoyote.
Pia, kanuni imekataza kutoa maneno ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kusababisha vurugu.
Kwa mujibu wa kanuni vituo vya kupigia kura vitakuwa katika majengo ya umma yaliyopo kwenye eneo husika au kama hayapo, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, baada ya kushauriana na wagombea au vyama vya siasa vyenye wagombea, atateua eneo lingine kuwa kituo cha kupigia kura.
Pia, kutakuwa na sanduku maalumu la kupigia kura lililotengenezwa kwa namna itakayomwezesha mpiga kura kutumbukiza kura yake kwa urahisi kwa kila ngazi itakayopigiwa kura bila ya kuruhusu kura hiyo kutolewa ndani ya sanduku hilo.
Kwa mujibu wa kanuni kabla ya kuanza kupiga kura, msimamizi wa kituo atawaonyesha wapiga kura sanduku la kupigia kura lililo wazi na atalifunga kwa lakiri kwa namna ambayo itazuia kufunguliwa bila kukata lakiri.