Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) kufanyika Morogoro

Baraza la Michezo ya Majeshi hapa nchini (BAMMATA) limetangaza michezo hiyo kuanza kutimua vumbi Mkoani Morogoro kuanzia Septemba 6 hadi 15 mwaka huu ambapo mashindano ya michezo mbalimbali inatarajiwa kufanyika huku zaidi ya wanamichezo 1300 kutoka Kanda 8 za michezo hiyo hapa nchini wakibainisha kushiriki.

Hayo yamebainishwa Mwenyekiti wa BAMMATA Brigedia Jenerali Said Hamis Said wakati wa kikao cha wajumbe wa Baraza hilo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake kikiwa na lengo la kujitambulisha na kueleza lengo la kufanyia mashindano hayo Mkoani humo.

Akifafanua zaidi Brigedia Jenerali Said Hamis amesema mashindano hayo yatajumuisha kanda 8 ambazo ni Ngome, Ngome visiwani, polisi, magereza, uhamiaji, zimamoto, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Vikosi maalum vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kushiriki michezo mbalimbali.

“… sisi kama Baraza la michezo la majeshi tumeona tuje Morogoro tuwe sehemu ya kuimarisha Ulinzi na Usalama kwa kuwakutanisha wanausalama wote kupitia michezo…” amesema Brigedia Jenerali huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ametaja baadhi ya faida za michezo kuwa huunganisha wananchi na kuwa kitu kimoja bila kujali chama, kabila au bila kujali tofauti za imani zao hivyo amevipongeza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuanzisha mashindano hayo Mkoani kwake na kuahidi Ofisi yake kutoa ushirikiano wa kutosha kipindi chote cha mashindano hayo.

Aidha, amesema mashindano hayo yana manufaa makubwa katika kuimarisha umoja wa kitaifa na kimataifa katika kuleta ushirikiano baina ya majeshi na wananchi sambamba na kuimarisha Ulinzi na Usalama na ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo Mhe. Adam Malima ameyataka mashindano hayo kuwa daraja la kubaini vipaji vilivyo ndani ya majeshi hayo na kuendelezwa ili kupata wanamichezo watakaoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kwa sababu hiyo amewataka wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki michezo hiyo ili kuwapa nguvu majeshi yao na kujifunza michezo itakayochezwa.

 

Related Posts