Mitihani mitano aliyoanza nayo Fadlu Simba

Dar es Salaam. Simba SC imempa jukumu Kocha Fadlu Davids kuiongoza timu hiyo msimu huu wa 2024-2025 katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki yakiwamo Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.

Fadlu raia wa Afrika Kusini, ametua Simba kuchukua mikoba ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha ambaye aliondoka kikosini hapo Aprili 2024, siku chache baada ya kufungwa 2-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara. Kabla ya kuondoka, alishinda Kombe la Muungano michuano iliyochezwa visiwani Zanzibar.

Katika kipindi cha takribani siku 40 tangu atambulishwe ndani ya Simba Julai 5, 2024 hadi Agosti 15, 2024 siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, kuna mambo matano amekutana nayo kocha huyo.

Mambo hayo unaweza kusema ni kama mitihani yake ya kwanza ambapo anapaswa kujipanga kisawasawa wakati akiuanza msimu katika harakati zake za kurudisha furaha iliyopotea Msimbazi.

Katika kuimarisha kikosi, Simba kabla ya kumpa Fadlu jukumu la kuiongoza timu, ilianza usajili haraka kwa kumtambulisha beki wa kati, Lameck Lawi kutoka Coastal Union.

Taarifa ya Simba ilibainisha hivi; “Klabu ya Simba imefanikiwa kumsajili mlinzi wa kati Lameck Elius Lawi kwa mkataba wa miaka mitatu kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja akitokea Coastal Union ya Tanga

“Lawi ni kijana mwenye kipaji kikubwa na amekuwa ngome imara kwenye kikosi cha Coastal msimu uliopita na hicho ndicho kilichotuvutia kumsajili. Usajili wa Lawi ni mkakati wa kuijenga Simba mpya yenye ushindani kuelekea msimu wa mashindano wa 2024/25.

“Lawi mwenye umri wa miaka 18 na umbile refu anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa katika kikosi chetu kuelekea msimu mpya wa Ligi. Lameck Lawi licha ya umri wake mdogo lakini ni mlinzi mwenye uwezo mkubwa aliyewavutia wapenzi wa mpira nchini Tanzania na nje ya mipaka ya nchi yetu na usajili wake tunategemea ataongeza kitu kikubwa katika kikosi akisaidiana na walinzi wazoefu waliokuwepo.”

Baada ya utambulisho huo, Coastal waliibuka na kusema makubaliano hayakwenda vizuri hivyo wanatambua bado huyo ni mchezaji wao ambapo ishu hiyo ikatua katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ikiwataka Simba na Coastal kumalizana wenyewe.

Kipindi chote hicho cha sintofahamu, Fadlu alikuwa Misri na kikosi cha Simba akiandaa program zake bila ya uwepo wa mchezaji huyo kitu ambacho kwake hakipo sawa, mchezaji aliyetambulishwa kikosini akitegemea atamuingiza kwenye mfumo wake, ghafla haonekani.

Wakati akiumiza kichwa juu ya sakata hilo huku muda ukizidi kwenda kabla ya kuanza kwa msimu, Fadlu anapata pigo lingine kikosini kwake baada ya kuumia kwa kipa tegemo kikosini hapo, Ayoub Lakred.

Lakred aliumia wakiwa mazoezini nchini Misri ambapo ikawalazimu Simba kuingia sokoni haraka na kumshusha Moussa Camara.

Wakati Ayoub akiwa majeruhi wakiwa Misri, Fadlu alilazimika kuendelea kuwatumia makipa waliopo, Hussein Abel na Ally Salim ambao wanaonekana sio chaguo la kwanza. Ayoub angekuwa fiti ndiye angekuwa chaguo la kwanza. Hiyo ni kutokana na Aishi Manula kutokuwepo na timu kwa muda mrefu.

Hata hivyo, ujio wa Camara kwa kiasi fulani umeziba pengo la Ayoub kwani ameonesha kiwango kizuri katika mechi mbili za Ngao ya Jamii walipomaliza nafasi ya tatu.

Fadlu amekaribishwa Simba na Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga ambayo alijikuta akipoteza kwa bao 1-0 ikiwa ni katika Ngao ya Jamii.

Mchezo huo uliochezwa Agosti 8, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Fadlu aliingia uwanjani akiwa ametoka kushinda mechi zote nne za kirafiki zikiwemo tatu walipokuwa kambini Misri na moja ya Simba Day.

Usajili wa Awesu wapangua mipango yake

Awesu Awesu ni kiungo aliyetambulishwa ndani ya Simba Julai 17, 2024 kutoka KMC.

Katika utambulisho wake, Simba ilisema: “Kiungo mshambuliaji Awesu Awesu amejiunga nasi kutoka KMC kwa mkataba wa miaka miwili. Awesu amejiunga nasi akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na KMC aliyodumu nayo kwa miaka mitatu.

“Awesu ni mchezaji mzoefu kwenye Ligi Kuu na anaweza kumudu nafasi ya kiungo wa ushambuliaji na winga zote ingawa pia amewahi kutumika kama kiungo mkabaji. Mbali na KMC, Awesu amewahi kutimikia timu za Kagera Sugar, Azam FC na Mwadui FC kwa nyakati tofauti.

“Tumefanya marekebisho makubwa ya kikosi kwa kusajili nyota wapya ndio maana tunaongeza na wachezaji wazawa wenye ubora. Kuelekea msimu mpya wa mashindano tunaandaa kikosi imara ambacho katika kila nafasi kutakuwa na wachezaji wenye ubora unaolingana.”

Wakiwa kambini Misri, Kocha Fadlu alionekana kuridhishwa na uwezo wa Awesu kiasi cha kumuingiza kikosi cha kwanza ambapo lilionekana hilo katika mchezo wa mwisho aliocheza akiwa na jezi ya Simba katika Tamasha la Simba Day dhidi ya APR.

Baada ya hapo, Awesu hakucheza mechi yoyote ya kimashindano ambapo Simba ilicheza mbili katika Ngao ya Jamii. Sababu za kutocheza ni kutokana na usajili wake kuwekewa pingamizi na KMC ambayo mwisho wa siku Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ikatoa majibu ya kwamba kiungo huyo ni mchezaji halali wa KMC.

Kwa ishu ya Awesu, inaelezwa alishakuwa kwenye mipango ya kocha Fadlu Davids kwa ajili ya mechi za Ngao ya Jamii, lakini Simba ilipokea taarifa kutoka Bodi ya Ligi kwamba hairuhusiwi kumtumia kutokana na kulalamikiwa na klabu aliyokuwa akiichezea ya KMC, hivyo ikatibua mikakati ya Fadlu katika mchezo huo.

Mukwala, Freddy walivyomzingua

Simba ilisajili washambuliaji wawili, mzawa Valentino Mashaka na Steven Mukwala raia wa Uganda, wameingia kikosini hapo kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kwa kushirikiana na Freddy Michael aliyekuwapo tangu dirisha dogo msimu uliopita.

Baada ya Simba kucheza mechi mbili za Ngao ya Jamii na moja ya Simba Day, washambuliaji hao wakashindwa kumshawishi Fadlu kuendelea kuwaamini, hivyo akaagiza asajiliwe mshambuliaji mwingine. Kitendo hicho ni wazi washambuliaji hao wamemzingua Fadlu kwani mwanzo aliamini wanatosha lakini imekuwa tofauti.

Kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji, Simba imemalizana na Leonel Ateba raia wa Cameroon, mchezaji ambaye Fadlu anaamini hatamuangusha.

“Ujio wa Mshambuliaji mpya utakuwa chachu ya ushindani na kuendelea kumuimarisha Karabaka ambaye naamini atakuja kuwa Mshambuliaji tishio hapo baadae kutokana na umri wake na amekuwa akiimarika siku hadi siku,” alisema Fadlu.

Related Posts