Mkutano Mkuu wa chama cha Democratic kuanza Jumatatu – DW – 19.08.2024

Wanaharakati hao wanatarajia kupaza sauti kuhusiana na masuala ya haki za uavyaji mimba, ukosefu wa haki sawa katika masuala ya kiuchumi na vita vya Israel dhidi ya Hamas.

Huku Makamu wa Rais Kamala Harris akiwa amewafurahisha wafuasi wake wakati anapojiandaa kukubali kuteuliwa kwake na chama cha Democratic kama mgombea wa urais, wanaharakati wanashikilia kwamba malengo yao bado ni yale yale.

Funzo kutoka mkutano mkuu wa Republican

Maandamano yanatarajiwa kufanyika kila siku wakati mkutano huo ukiendelea na ingawa ajenda za wanaharakati hao ni tofauti, ila wengi wao wanakubaliana kwamba vita vya Israel dhidi ya hamas vinastahili kusitishwa.

Wanaharakati wanasema walijifunza kutokana na mkutano mkuu wa chama cha Republican mwezi uliopita uliofanyika huko Milwakee na wanatabiri watu wengi zaidi kujitokeza na maandamano yawe yenye nguvu zaidi huko Chicago, mji ulio na mizizi ya uanaharakati wa kijamii.

Donald Trump akiwa katika mkutano mkuu wa Republican Milwaukee
Donald Trump akiwa katika mkutano mkuu wa Republican MilwaukeePicha: Angela Weiss/AFP via Getty Images

Mambo yalianza mkesha wa mkutano huo hapo Jumapili ambapo wanaharakati waliandamana katika barabara ya Michigan dhidi ya vita vya Gaza na wakitaka haki kwa wapenzi wa jinsia moja pia. Maandamano hayo yalianza mchana na yakaendelea hadi usiku.

Polisi walisimama kwa mstari katika njia yalipokuwa yanafanyika maandamano hayo na hakukuwa na ishara zozote za mtafaruku baina yao na waandamanaji.

Mwandaaji wa maandamano hayo Linda Loew alisema ingawa Wademocrat wamekuwa wakishinikiza kulindwa kwa haki za uzazi nchini Marekani, suala la uavyaji mimba ni la kimataifa.

“Tunaamini kwamba mabilioni ya dola na silaha zinazoendelea kutiririka nchini Israel, zina athari mbaya hasa kwa wanawake, watoto na viumbe ambavyo havijazaliwa,” alisema Loew. “Yote haya yanaoana.”

Hakuna kikubwa kisera kinachotarajiwa kubadilika

Kundi kubwa litakaloandamana katika mkutano huo mkuu limepanga kufanya maandamano siku ya kwanza na ya mwisho ya mkutano huo mkuu.

Rais Joe Biden akiwa na makamu wake Kamala Harris
Rais Joe Biden akiwa na makamu wake Kamala HarrisPicha: Allison Bailey/NurPhoto/IMAGO

Waandalizi wanasema wanatarajia angalau wanaharakati 20,000, wakiwemo wanafunzi walioandamana katika vyuo vyao kupinga vita vya Israel dhidi ya Hamas.

Wanaharakati wengi lakini wanaamini kwamba hakuna kikubwa kitakachobadilika kwa kuwa Kamala Harris ni sehemu ya utawala wa Joe Biden.

Mkutano huo mkuu wa chama cha Democratic DNC, unakadiriwa kuhudhuriwa na wawakilishi 50,000 watakaokusanyika katika huo mji wa tatu kwa ukubwa Marekani.

 

Related Posts