Tunduma. ‘Hujafa, hujaumbika’ ndiyo kauli unayoweza kusema kwa mtoto Ebeneza Mwakasyele (8) aliyepoteza mguu wa kushoto mwaka 2019 na kutembelea magongo baada ya kukatwa kutokana na kuugua ugonjwa usiojulikana chanzo chake.
Lakini hayo yote yamepita baada ya Ebeneza anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Tunduma mkoani Songwe kupata mguu wa bandia.
Ebeneza alirejeshewa furaha yake na Rais Samia Suluhu Hassan kutekelezwa leo aliyeahidi kumpatia mguu wa bandi Julai 18, 2024 alipokuwa akihutubia katika uwanja wa Mwaka Tunduma, akiwa katika ziara aliyofanya mkoani Songwe. Ahadi hiyo hatimaye imetimizwa jana ambapo Ebeneza mbali na kufurahi pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona uhitaji alionao.
Ebeneza alikuwa miongoni mwa mamia ya wananchi waliofika katika uwanja huo kumsikiliza, akiwa na fimbo aliyokuwa akiitumia kutembelea kutokana na ulemavu aliokuwa nao.
Akiwa anahutubia, Rais Samia alimwita Mkurugenzi wa halmashauri hiyo jukwaani akitaka amwonyeshe mtoto huyo.
“Umeona kale katoto? Alikuwa nyuma kule akapenyapenya, wakamzingira nikawaambia hebu mleteni mbele, yule pale na gongo lake. Sasa nataka atengenezewe mguu wa bandia na gharama italipa ofisi yangu,” alisema Rais Samia.
Alimtaka mkurugenzi huyo kuhakikisha mtoto huyo anapelekwa hospitalini hata kama ingebidi apelekwe Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo, apelekwe.
Akizungumza leo Agosti 19,2024 baada ya kumkabidhi mguu huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Mariamu Chaurebo amesema baada ya Rais Samia kutimiza ahadi ya kumnunulia mguu wa bandia Ebeneza ofisi yake itahakikisha inabadilisha mguu huo kila muda utakapokuwa unahitajika kufanyiwa hivyo.
Amesema katika kipindi chake cha ukurugenzi ataandika barua ambayo kila mkurugenzi atakaye fanya kazi kwenye Halmashauri hiyo atatekeleza maelekezo ya kumnunulia mguu mtoto huyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tunduma, Suzana Mwakibete amesema Ebeneza alianza darasa la awali mwaka 2021 kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambapo uhitaji wake ulikuwa mkubwa ukilinganisha na wenzake waliopo 104, kwani alikuwa anatambaa muda wote.
Mwakibete amesema walimu wa shule hiyo walikuwa wakimsaidia pindi alipohitaji kwenda chooni, kwani alikuwa hawezi kwenda pekee yake maana alikuwa anasota kwa makalio.
“Tunatarajia baada ya Ebeneza kupatiwa mguu ataondokana na changamoto ya kutembelea mguu mmoja, hivyo kuhudhuria masomo pamoja na kutimiza ndoto zake.” “Anapenda michezo nadhani sasa atatimiza ndoto yake hiyo, ikiwezekana atakuja kuwa kiongozi serikalini,” amesema Mwakibete.
Akizungumza baada ya kupewa mguu huo na kuuvaa, Ebeneza alimshukuru Rais Samia na kumwahidi kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zake kimaisha ikiwepo kuwa kiongozi mkubwa serikalini.
Ebeneza amesema amepitia changamoto tangu alipokatwa mguu wake, ambapo alishindwa kutembea licha ya kusaidiwa na wenzake alipohitaji msaada akiwa darasani na wakati mwingine alinyanyapaliwa na jamii.
“Nilikuwa najisikia mpweke kutokana na hali ya kuwa tofauti na wenzangu lakini kaka yangu na wanafunzi wenzangu walikuwa wananisaidia sana pindi nilipokuwa nahitaji msaada,” amesema Ebeneza.
Mama mzazi wa Ebeneza, Atwanukiye Sanga amesema Ebeneza amepitia changamoto nyingi kabla na baada ya kukatwa mguu kwani alikosa malezi ya baba yake, ambaye walitengana mwaka 2019 baada ya mtoto wao kuanza kuumwa.
Amesema alihangaika sana kumtibu mwanaye bila kuwa na msaada wowote, huku mzazi mwenzake akioa mwanamke mwingine anayeishi naye mpaka sasa.
Amesema Ebeneza alikuwa hana furaha baada ya kukatwa mguu, alikuwa anatambaa kwa kutumia makalio, ambapo alikuwa na mawazo yaliyomfanya arudi nyuma kimasomo.
“Baada ya kukatwa mguu huo mwanangu alikuwa mpweke sana nikaamua kumpeleka shule katika kitengo cha watu wenye mahitaji maalumu, nilihakikisha kila siku namleta na kumrudisha nyumbani ili kuhakikisha ndoto zake kielimu zinatimia,” amesema Sanga.
Amesema kutokana na changamoto hiyo alipofika darasa la kwanza alimtafutia gongo la mti alilodumu nalo mpaka darasa la pili ambapo Mbunge wa Tunduma, David Silinde alimnunulia gongo la chuma alilolitumia mpaka Rais Samia alipotoa msaada wa kumnunulia mguu wa bandia.
“Namshukuru sana Rais Samia kwa msaada wa kumnunulia mguu wa bandia mwanangu hali ambayo itamsaidia kuhudhuria masomo na kutimiza ndoto zake kimaisha,” amesema Sanga.
Mama huyo amesema Ebeneza alizaliwa Septemba 4, 2016 Mtaa wa Mwaka Kati katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma mkoani Songwe, akiwa hana ulemavu wowote.
Amesema changamoto hiyo ilianza mwaka 2019, baada ya kuugua ugonjwa ambao haukujulikana.
Ameeleza ugonjwa huo ulisababisha mguu kuvimba, kutoa malengelenge yaliyosababisha ngozi ya mguuni kuanza kukauka.
Amefafanua alimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Mbozi (Vwawa), ambako alishauriwa apelekwe Hospitali ya Consolata Ikonda.
“Alipofikishwa hospitali ya Ikonda alifanyiwa uchunguzi ambao hata hivyo haukubaini ugonjwa uliokuwa ukimsumbua. Ebeneza alikatwa mguu wake wa kushoto mara tatu na kumfanya kuwa mwenye ulemavu.”
“Hali hiyo ilimwathiri kisaikolojia hasa alipokuwa akicheza na watoto wenzake, ila leo naamini amepata faraja nami namshukuru sana Rais,” amesema Sanga.