Tabora United na rekodi mbovu mechi 16 ugenini

KICHAPO cha mabao 3-0 ilichokipa Tabora United dhidi ya Simba juzi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa KMC Complex jiji Dar es Salaam, kimeifanya timu hiyo kuendeleza rekodi mbovu ya ugenini kuanzia msimu uliopita hadi sasa.

Kikosi hicho kilichopanda daraja msimu wa 2022-2023 na kucheza Ligi Kuu Bara msimu uliopita kilicheza michezo 15 ya ugenini kati ya 30 ambapo hakikushinda hata mmoja zaidi ya kuchapwa mechi 10 na kutoka sare tano.

Ukiongeza na mchezo wa juzi dhidi ya Simba ambao pia ilipoteza ikiwa ugenini, Tabora United inafikisha michezo 16 tangu ipande daraja na kucheza Ligi Kuu Bara ambapo kwa sasa inakifanya kikosi hicho kupoteza mechi 11, huku mitano iliyobakia ikitoa sare.

Katika michezo 16 ya ugenini iliyocheza hadi sasa ndani ya Ligi Kuu Bara, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 29, huku ikifunga mabao saba ambayo yalikuwa ni ya aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho Mghana Eric Okutu aliyejiunga na Pamba Jiji msimu huu.

Mbali na hilo, Tabora United pia imeendeleza rekodi mbovu inapocheza na Simba kwani mchezo wa juzi ni wa tatu wa Ligi Kuu Bara kukutana na haijashinda hata mmoja zaidi ya kuchezea vichapo huku ikishindwa kufunga bao. Mchezo wa kwanza zilianza kukutana Februari 6, mwaka huu ambapo Tabora United ikiwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora ilichapwa mabao 4-0, kisha marudiano Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam ilipoteza mabao 2-0, ilikuwa Mei 6, mwaka huu.

Kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Francis Kimanzi alisema licha ya kupoteza mchezo huo, lakini bado kuna nafasi nzuri zaidi ya kurekebisha upungufu uliojitokeza, huku akitambia usajili mkubwa uliofanyika kwa mastaa wapya kikosini.

“Kila kosa ni funzo kwetu, tumejifunza kutokana na kile tulichokipata katika mchezo wetu uliopita, kwa sasa malengo na mikakati yetu ni kuangalia mpinzani aliyekuwa mbele ili kupata kilichokuwa bora japo ushindani wa hapa ni mkubwa sana,” alisema.

Kimanzi aliyezaliwa Mei 29, 1976, amejiunga na kikosi hicho msimu huu huku akiwa na rekodi ya kuzifundisha timu mbalimbali za Kenya ikiwemo ile ya taifa ‘Harambee Stars’ na klabu ambazo ni Wazito, Mathare United, Sofapaka na Tusker FC

Related Posts