UN: Mwaka 2023 ulikuwa ‘mgumu’ kwa watoa huduma za kibinadamu ulimwenguni

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Watoa Huduma za kibinadamu Ulimwenguni, imeelezwa mwaka 2023 ulikuwa mwaka mgumu kwa watoa huduma hizo kutokana na baadhi yao kupoteza maisha wakati wakitekeleza majukumu yao, hususan kwenye maeneo yenye vita na machafuko ya kisiasa.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo Jumatatu Agosti 19, 2024 jijini Dar es Salaam, Elkie Wisch kutoka Umoja wa Mataifa (UN), amesema moja ya sababu iliyochangia baadhi ya watoa huduma hao kupoteza maisha ni pamoja na baadhi ya mataifa kutozingatia misingi ya sheria ya kimataifa zinazowalinda raia pamoja na watoa huduma hao wakati wa vita.

“Wakati tunasheherekea siku ya watoa huduma za kibinadamu, wakati wa maafa tunatoa wito kwa mataifa hayo kuzingatia sheria hiyo ya kimataifa na kuacha kuwashambulia watoa huduma hao pamoja na raia wote kwa ujumla,” amesema.

Pia, Wisch amesema maadhimisho ya siku hiyo ni fursa ya kuwapongeza watu wanaojitokeza kutoa msaada wa kibinadamu pale yanapotokea maafa mbalimbali, ikiwemo mafuriko, ukame, vita, machafuko ya kisiasa na mengineyo.

Amesema pia ni fursa inayomkumbusha kila mmoja wajibu wake wa kusaidia watu wengine wenye mahitaji na kurejesha tabasamu kwa watu waliorudishwa nyuma kimaisha kutokana na maafa.

Hata hivyo, wadau mbalimbali wametumia fursa hiyo kutoa maoni mbalimbali yatakayosaidia kuboresha utolewaji wa huduma za kibinadamu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, mkurugenzi mtendaji wa shirika linaloshughulikia masuala ya watoto la Save the Children, Angela Kauleni amesema Tanzania katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kibinadamu, ikiwemo zile zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uwepo wa muda mrefu wa wakimbizi kutoka nchi jirani.

Kauleni amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimesababisha kuwepo kwa majanga kama mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa, athari za El Niño, njaa, tishio la vimbunga, maporomoko ya ardhi na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza yanayochangia kuongezeka kwa mahitaji ya misaada ya kibinadamu.

Amesema ili kukabiliana na hayo, wao kama wadau wanashauri kuanzisha kuanzisha mfuko wa Taifa wa dharura ambapo Serikali itatenga bajeti kila mwaka, pamoja na michango kutoka kwa washirika wengine/mashirika ya misaada na sekta binafsi, ili kuepuka kutegemea msaada wa dharura ambao hauwezi kuwa endelevu.

Pia kila  wizara kuingiza mikakati ya kupunguza mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa hatari za majanga katika mipango yao, ili kuhakikisha shughuli za uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa majanga zinakuwa sehemu ya utendaji wa kila wizara.

Ameongeza kuwa ni muhimu kuangalia uwezekano wa kuwahamisha watu kutoka maeneo yenye hatari kubwa, kujengwa kwa miundombinu inayostahimili pamoja na kuandaa vifaa vya dharura mapema kabla ya maafa hayajatokea.

“Kuchukua hatua za kimkakati na kutekeleza mabadiliko ya kimuundo na sera ili kuongeza uwezo wa Serikali, wadau wote na jamii katika usimamizi wa majanga, tunapaswa pia kuchukua hatua za kuzuia, kupunguza hatari, na kujiandaa kwa majanga kwa lengo la kupunguza hatari za muda mrefu,” amesema.

Kwa upande wake, Maria Bilia ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Rapid Tanzania ameshauri uwepo wa sheria inayojitegemea itakayosimamia utolewaji wa huduma za kibinadamu pale yanapotokea maafa, ili wale watakaokwenda kinyume wachukuliwe hatua kali.

Naye Victor Katambala, meneja mratibu wa maafa na majanga kutoka Shirika la Word Vision amesema kinga ni bora kuliko tiba, hivyo ni muhimu kuwekeza zaidi katika kuwapa elimu katika jamii kuliko kusubiri maafa yanapojitokeza.

Kauli hiyo imeungwa mkono na mkurugenzi mtendaji wa Tasisi ya SUKOS, Suleiman Kova ambaye pia ni Kamanda mstaafu wa Jeshi la Polisi aliyesisitiza elimu hiyo ianzie katika ngazi ya familia.

Related Posts