Wamiliki wa mabasi wabuni mkakati kukabili athari za SGR

Dar es Salaam. Wakiwa na wasiwasi juu ya kasi ya kupoteza biashara katika njia ya Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma, wamiliki wa mabasi wamebuni mkakati utakaowawezesha kuendelea kubaki kwenye biashara, baada ya kuanza kwa safari za treni ya kisasa (SGR).

Tangu kuanza kwa usafiri wa treni ya kisasa miezi miwili iliyopita ikihusisha njia ya  Dar es Salaam na Morogoro na siku 19 kwa usafiri wa Dar es Salaam na Dodoma, wamiliki wa mabasi wamekuwa wakilalamika kushuka kwa biashara zao, baada ya abiria wengi kuvutiwa na usafiri wa treni hiyo.

Kupitia Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), wafanyabiashara hao wameandaa mkakati unaolenga kuhakikisha wanabaki kwenye biashara yao licha ya ushindani wanaoupata.

Miongoni mwa mikakati iliyotajwa na Katibu wa kitaifa wa Taboa, Joseph Prisicus, ni kuhamishia mitaji yao kwenye maeneo mengine au sekta ambazo hazijatumika.

Prisicus ameliambia gazeti dada  la The Citizen jana  kwamba chama hicho pia kinawaomba wanachama wake kuandika barua kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuomba msaada katika eneo la kodi.

Amesema ametoa ombi hilo kwa wanachama wao kwa  sababu ni wazi kuwa  wale wanaotegemea tu njia ya Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma watakumbana na changamoto za kukidhi makadirio ya awali ya kodi, kutokana na kupungua kwa idadi ya safari za mabasi.

“Dar es Salaam-Morogoro-Mwanza ni njia kuu yenye mabasi mengi kuliko mkoa mwingine wowote. Angalau mabasi 100 husafiri kwenye njia hiyo kila siku,” amesema, akibainisha kuwa mpango wa haraka ni kupunguza kiwango cha uwekezaji kwenye njia hiyo na kuhamishia mabasi hayo kwenye maeneo mengine ya usafirishaji na sekta ambazo bado hazijatumika.

Amesema kutokana na athari za SGR, wamiliki wa mabasi wanaweza tu kuunga mkono maendeleo hayo hata wanapotafuta chaguzi nyingine.

“Usafiri wa reli unatoa faida nyingi. Kwa hiyo, kama abiria watamalizia safari Dodoma, kuna mabasi yatakayowapeleka kwenye maeneo mengine. Kwa kuwa sisi sote ni walipa kodi, Serikali inapaswa kuangalia jinsi ya kuwasaidia wamiliki ili kuwe na hali ya kushinda wote katika mchakato huo,” amesema.

Amesema Taboa, bado inafanya tathmini juu ya athari halisi za SGR kwenye shughuli za wamiliki wa mabasi, zikihusisha  maeneo mbalimbali ya ajira na mitaji ya wawekezaji ambayo itajulikana baada ya miezi sita.

Amefafanua kuwa kinachojulikana hadi sasa ni kwamba kampuni ambayo hapo awali ilikuwa ikifanya safari 20 kwa siku kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, sasa imepunguza safari zake hadi kati ya tisa na kumi kwa siku. Upungufu huo unamaanisha kuwa watapata changamoto kulipa kodi iliyokadiriwa kutokana na kupungua kwa idadi ya magari.

Kwa sasa, baadhi ya madereva wamekuwa wakikaa nyumbani bila kazi nyingi za kufanya na wamiliki wa mabasi wamelazimika kuwapa pesa za kujikimu.

Madereva, amesema, wamekuwa wakiomba kazi mahali pengine. “Ushauri wetu kwa wanachama ni kwamba wafanye kazi kwa ufanisi ili waweze kushindana kwenye soko. Tunaamini kutakuwa na abiria wa reli na kutakuwa na abiria wa mabasi pia. Tofauti pekee ni kwamba faida ya mabasi itakuwa ndogo kuliko ilivyokuwa awali,” amesema.

Mapema mwezi huu, mwakilishi wa Kampuni ya Shabiby Bus, Edward Magawa, amesema kwa sasa wanafanya kazi ya kuboresha biashara yao kwa kuangalia maeneo mengine badala ya kutegemea sana njia ya Dar es Salaam-Dodoma.

Magawa ameiomba Serikali kuanzisha vituo vya mabasi karibu na vituo vya SGR ili iwe rahisi kwa abiria kuunganisha au kupata mabasi na kuendelea na safari zao.

Mkurugenzi wa Usafiri wa Barabara katika Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu (Latra), Johansen Kahatano amekiri kwamba biashara ya mabasi imepungua kwa kiasi kikubwa

Amesema wiki mbili kabla ya kuanza kwa huduma za treni inayotumia umeme, walifanya utafiti kwa njia ya Dar es Salaam-Morogoro.

Utafiti huo ulijikita katika jumla ya mara ambazo mabasi hufanya safari, kama ilivyofuatiliwa kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji wa Magari (VTS).

“Tulitambua kuwa basi ambalo lilikuwa likianza safari kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kisha kurudi kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam na tena kurudi Morogoro kutoka Dar es Salaam (safari tatu) limepunguza safari zake na kubaki na mbili tu ambazo ni Dar es Salaam-Morogoro na kurudi Dar es Salaam,” alisema.

Wakala wa Basi la Super Baraka katika Kituo cha Magufuli, Zawadi Chusi, amesema imekuwa vigumu sana kwake kupata abiria wanaosafiri kati ya Dar es Salaam na Tabora.

Hata hivyo, ni wazi kwamba mabasi yatabaki kuwa muhimu kwa baadhi ya abiria kwa sababu si kila mtu kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma atasafiri kwa treni.

Related Posts