Dar es Salaam. Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amesema hali ya umaskini uliokithiri nchini kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa, ni sababu ya kujikuta wakigeuka kuwa ‘chawa.’
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 19, 2024 kwenye kongamano la Baraza la Wanawake (Bawacha) lililofanyikia Moshi, mkoani Kilimanjaro na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Mkoa wa Kilimanjaro na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Grace Kiwelu aliyekuwa mgeni rasmi.
Dhima ya kongamano hilo ni kuwawezesha viongozi waliochanguliwa ndani ya chama hicho kutambua haki na wajibu wao, na kuwajengea uwezo wa kujitambua kuwa na upendo kwa chama na Taifa kwa ujumla.
“Hakuna kitu kizuri kama kufanya shughuli za kisiasa kama uchumi wako mzuri, uchumi ukiwa mbaya lazima utikisike na usipoangalia vizuri unaweza kujikuta umekuwa chawa.”
“Kijamii, lazima uwe mtu mwenye sura yenye haiba nzuri unayekubalika kwa jinsi unavyowatumikia watu na kuwapenda watu. Kikubwa pendaneni wenyewe kwa wenyewe kwanza kwa kuimarishana kiuchumi baada ya hapo mtakuwa na thamani kubwa,”amesema Lema.
Katibu huyo amesema hata wakiingia kwenye uchaguzi pamoja na misukosuko wanayopitia, hawatakiwi kutengana bali hata kama wakikosa nafasi, wanapaswa kuwa kitu kimoja katika kuimarishana kiuchumi.
Kwa upande wake, Kiwelu amewashauri wanachama kuondoa tofauti miongoni mwao na kuungana kuwa kitu kimoja kama mbinu wanayoweza kuvuna viongozi wengi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Tukafanye kazi kwa kuondoa tofauti zilizopo kati yetu na kujipanga kukiondoa chama cha mbogamboga madarakani. Wanawake ni waathirika wakubwa ikiwemo mikopo ya kausha damu kwa kukosa uongozi thabiti,” amesema Kiwelu.
Akiwazungumzia wanawake, Kiwelu amesema wanapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu, wanapaswa kutambua kuwa wao ni jeshi kubwa, wanapaswa pia kugombea nafasi za uongozi.
“Niwaombe kinamama mkachukue fomu mkagombee nitakuja kufanya kampeni kwa kina mama watakaochukua fomu kuomba uongozi, hii pia ni haki yetu,” amesema.
Kiwelu amesema kwa kawaida uchaguzi una mambo mengi yanayoweza kuleta mkanganyiko, hivyo amewataka kuvumiliana na wawe na moyo wa subra.
Katika maelezo yake Kiwelo aliongeza kuwa Manispaa ya Moshi Mjini ina mitaa 60 na Kata 21 ni wajibu wa Bawacha kuwahamasisha wanawake wenye sifa kwenda kuchukua fomu za kugombea.
“Tuna uchaguzi wa madiwani, wabunge na rais mwakani, kwa hiyo kwa wale watakaoonesha nia na kupitishwa na mchakato wa chama, tunayo kazi kubwa ya kuwapigania kuhakikisha wanashinda,” amesema mjumbe huyo wa kamati kuu.
Amesema ili kufikia azma hiyo, kazi hiyo inapaswa kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa ili wajenge msingi mzuri utakaowasaidia kuvuka mwaka 2025 kwa kupata viongozi wenye sifa wanazohitaji.
Amesema chama hicho kimeshajipanga na wanachohitaji ni ari na morali kwa wananchama hasa kinamama kwa kuwa wanaaminika katika jamii kujenga ushawishi katika kampeni.