Arusha. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha, limetoa adhabu kwa watumishi wake watatu wa halmashauri hiyo, akiwemo mmoja kufukuzwa kazi.
Mtumishi mwingine ameshushwa cheo na mwingine ameadhibiwa kupunguziwa mshahara wake kwa asilimia 15 kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kutokana na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh300 milioni.
Adhabu hizo zimetolewa Agosti 17, 2024, katika kikao cha baraza hilo na uamuzi ulisomwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo mbele ya madiwani, watendaji wa halmashauri pamoja na mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa.
Akisoma uamuzi huo, mwenyekiti huyo amesema baraza limemfukuza kazi aliyekuwa mtendaji wa Kata ya Olmolog, Thomas Mitiaki, baada ya kumkuta na hatia ya udanganyifu wa tani 24 za mahindi ya bei nafuu yaliyokuwa na thamani ya Sh16.8 milioni.
Amesema mahindi hayo yaliyokuwa yametolewa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Arusha na ofisa mtendaji huyo alidaiwa kughushi majina ya wanufaika kinyume na Kanuni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2022.
Mwenyekiti huyo amesema mtendaji huyo ambaye alifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 12/2023, yeye na wenzake walikutwa na hatia na kutakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kifungo cha miaka miwili na kupewa amri ya kurejesha Sh16.8 milioni kwa NFRA.
Simon amesema baada ya baraza kupitia ushahidi na utetezi wa pande mbili, kamati imejiridhisha mtuhumiwa alikusudia kufanya udanganyifu wa kughushi majina ya wanufaika wa chakula hicho cha bei nafuu.
“Baraza limejiridhisha ushahidi uliotolewa umethibitisha bila shaka shtaka dhidi yake na baraza linatoa adhabu ya kufukuzwa kazi kulingana na aina ya kosa hilo,” amesema mwenyekiti.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mtumishi mwingine ni tabibu mkuu daraja la pili, Lomnyak Mollel ambaye amekutwa na hatia ya upotevu wa dawa za trakoma kopo 130 ambazo ni sawa na dawa 64,850 zenye thamani ya Sh8.8 milioni zilizokuwa zimehifadhiwa katika stoo ya Hospitali ya Wilaya ya Longido.
Amesema kwa kuzingatia ushahidi na utetezi wa mtuhumiwa kwa kina katika utetezi wake wa maandishi na uchunguzi wa awali uliofanywa na baraza hilo, umeridhika shtaka hilo limethibitika pasipo kuacha shaka.
Pia amesema baraza liliamua adhabu ya kupunguziwa mshahara wake kwa asilimia 15 kwa miaka mitatu mfululizo kwa kosa hilo na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022.
Kuhusu aliyekuwa kaimu mkuu wa idara ya ujenzi na fundi sanifu mwandamizi wa halmashauri hiyo, Dimoso Mananga, baraza limeamua kumshusha cheo kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Longido kwa kutofanya makadirio sahihi na kusababisha ongezeko la asilimia 15 ya makadirio.
Mwenyekiti huyo amesema kaimu huyo alikuwa anatuhumiwa kwa kosa la uzembe kazini uliosababisha hasara ya Sh335.2 milioni zilizotokana na ongezeko la makadirio ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Amesema kwa kuzingatia ushahidi na utetezi wa kina wa maandishi na alioutoa mbele ya kamati, baraza limeridhia shtaka hilo limethibitika bila kuacha shaka.
“Mtuhumiwa akiwa kaimu mhandisi alifanyakazi kama mhandisi, mkadiria majengo na mwenyetiki wa kamati ya ujenzi na alishindwa kudhibiti makadirio ya ujenzi na kusababisha mradi huo kuwa na tofauti ya asilimia 15 ambapo ni kinyume cha sheria. Baraza limejiridhisha na ushahidi uliotolewa na mwajiri dhidi yake na limeamua adhabu inayoendana na kosa hilo,” amesema Mwenyekiti
Amesema baraza limeamua adhabu ya kumshushwa cheo kwa kosa hilo kulingana na aina ya kosa pamoja na uzito wake. “Uamuzi huo ni kwa mujibu wa kanuni ya 42 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 48(3) cha kanuni za utumishi wa umma kwa mwaka 2022,” amesema Simon.