Nairobi. Mtuhumiwa wa mauaji ya wanawake sita akiwamo mke, Collins Khalusha ametoroka katika Kituo cha Polisi cha Gigiri, Nairobi Kenya.
Khalusha anadaiwa kuua kisha miili hiyo kuitupa katika machimbo ya Kware, Kaunti ya Embakasi.
Mtuhumiwa huyo ambaye alikiri kuhusika na mauaji hayo alikuwa miongoni mwa watuhumiwa 13 waliotoroka kituoni hapo saa tatu asubuhi leo Jumanne Agosti 20, 2024.
Watuhumiwa wengine 12 ni raia wa Eritrea waliokuwa katika kituo hicho cha polisi kwa kukaa zaidi nchini Kenya kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi Nairobi, Adamson Bungei akizungumza na Gazeti la Daily Nation amesema msako umeanza ili kuwakamata tena waliotoroka.
“Tunafuatilia suala hili kwa ajili ya hatua zaidi,” amesema.
Ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika kituo hicho, yenye utambulisho OB 05/20/08/2024.
Maofisa hao wamesema walienda katika vyumba vya watuhumiwa hao kwa ajili ya kuwapatia kifungua kinywa ndipo walipogundua walikuwa wametoroka.
Wamesema walipofungua mlango wa selo, walishtuka baada ya kubaini watuhumiwa 13 walitoroka kwa kukata matundu ya nyaya kwenye dirisha.
Khalusha alikuwa akisubiri kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kujibu mashtaka yake siku ya Ijumaa, Agosti 23, 2024.
Endelea kufuatilia Mwananchi.