Askari JWTZ, Magereza ‘waliotumwa na afande’ kortini tena leo

Dodoma. Kesi inayowakabili watu wanne wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza inaanza kusikilizwa leo Jumanne, Agosti 20, 2024, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dodoma.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, wakiwa wameunganishwa na watuhumiwa wa kesi nyingine tofauti na jana Jumatatu, walikuwa katika ulinzi mkali wenye msafara wa magari sita na askari wenye silaha kadhaa.

Baada ya leo Jumanne Agosti 20 2024 kufikishwa mahakamani, walipelekwa kwenye chumba maalumu wakisubiri muda ufike wapandishwe kizimbani.

Watuhumiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo jana, Agosti 19, 2024 wakiwa chini ya ulinzi wa askari polisi wakituhumiwa kumbaka kwa kikundi na kumlawiti binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

Waliofikishwa mahakamani ni askari wa JWTZ MT.140105 Clinton Damas, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Lord Lema na Nickson Jackson.

Kesi hiyo inatarajia kuanza kusikilizwa kuanzia saa nane mchana watuhumiwa wamefikishwa mahakamani hapo tangu asubuhi.

Hali ya Mahakama ni tulivu na shughuli nyingine zinaendelea kama kawaida.

Jana Jumatatu, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Makao Makuu, Renatus Mkude alisema kesi hiyo itasikilizwa kwa siku nne mfululizo hadi Ijumaa ya Agosti 23, 2024.

Mkude hakutaja jina la binti aliyefanyiwa vitendo hivyo, ili kulinda utu wake mbele za jamii ambaye ametambulika kwa jina la XY.

Tukio hilo lilianza kwa kusambaa picha jongefu katika mitandao ya kijamii Agosti 2, mwaka huu likionyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.

Katika kipande hicho cha video, binti huyo alishurutishwa kumwomba radhi mtu aliyetajwa kwa jina la Afande na alisikika akifanya hivyo.

Baadaye Agosti 9, 2024, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime lilitangaza kuwakamata vijana wanne waliohusika na ubakaji huo na wengine wanne kwa kosa la kusambaza video hiyo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts