Dk Mwinyi ataka safari za ATCL Zanzibar kukuza uchumi

Unguja/Dar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amelitaka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kuangalia zaidi safari zitakazopitia Zanzibar ili kukuza uchumi.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, hatua hiyo itawezesha kuvutia watalii wanaotembelea vivutio vilivyopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Agosti 20, 2024 alipohutubia wananchi katika hafla ya mapokezi ya ndege aina ya Boeing 878-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume.

Amesema ni muhimu shirika hilo likaangalia zaidi safari za ndege zinazopitia Zanzibar ili kuvutia watalii wanaotembelea vivutio vilivyopo.

“Serikali itaendelea kusimamia sera na sheria za usimamizi wa anga ili kuona mashirika mengi yanafanya safari hapa nchini kwa manufaa ya uchumi wa nchi,” amesema.

Kuendelea kukua kwa kasi kwa sekta ya utalii nchini na kuongezeka kwa faida inayotokana na uchumi wa buluu, amesema kunategemea ufanisi wa ATCL.

Amesema kuwepo kwa usafiri wa anga wa uhakika unaoendana na mikakati ya kukuza uchumi ni muhimu.

“Hapa nataka nisisitize umuhimu wa kufanya safari za ndege kati ya Pemba na sehemu nyingine za nchi yetu kutokana na umuhimu wa fursa za utalii zilizopo huko, ambazo bado hazijatumika,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, uwekezaji unaofanywa ndani ya ATCL una mchango mkubwa katika kukuza nchi na kuiunganisha kikanda na kimataifa.

Licha ya kukua kwa uchumi, Dk Mwinyi amesema bado kuna changamoto zinazowakabili wasafirishaji wa bidhaa nje ya nchi na kwamba, zinapaswa kutatuliwa.

Ameitaka Wizara ya Uchukuzi kuisimamia bodi ya ATCL kuhakikisha ndege zilizonunuliwa zinakuwa na tija iliyotarajiwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara amesema hiyo ni ndege ya nane kupokewa katika utawala wa awamu ya sita.

Amesema ndege hiyo ina uwezo wa kutembea saa 14 hadi 24 bila kutua, na imegharamiwa na Serikali kwa zaidi ya Sh300 bilioni.

Amesema baada ya ndege hiyo, ATCL inakuwa ya kwanza katika ushoroba wa kati, hivyo inachochea matumizi makubwa ya bandari na reli na kuongeza uchumi wa Taifa.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuongezeka kwa ndege za aina hiyo na kufikia tatu kunapunguza changamoto ya kukosa safari pindi ndege moja inapoharibika.

Amesema ndege hiyo inafanya shirika hilo kuwa na ndege 16.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Dk Khalid Mohamed Salum amesema Serikali inaendelea kufanya maboresho ya miundombinu ikiwamo upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege Unguja na Pemba.

Ndege hiyo ilipaswa kupokewa Agosti 19, 2024 katika uwanja huo lakini ilishindikana kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na hali mbaya ya hewa nchini Marekani.

Related Posts