WAKATI Prince Dube namba zake zikionekana kuwa nzuri katika kucheka na nyavu ndani ya Yanga, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amempa sharti ambalo anaamini kama mshambuliaji huyo akilifuata, basi atakuwa hatari zaidi mbele ya lango la wapinzani.
Dube ambaye amejiunga na Yanga dirisha kubwa la usajili msimu huu baada ya kuvunja mkataba ndani ya Azam, mpaka sasa amefunga mabao manne katika mechi saba alizocheza zikiwamo tatu za kimashindano dhidi ya Simba, Azam na Vital’O na nne za kirafiki dhidi ya FC Augsburg, TS Galaxy, Kaizer Chiefs na Red Arrows.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Gamondi alisema anafurahia kuona mshambuliaji wake huyo akianza vizuri na kuendelea kufunga japo ana changamoto kidogo za kuzifanyia kazi zaidi.
Gamondi amebainisha kwamba tayari ameshamueleza Dube vitu vya kufanyia kazi haraka kwa ajili ya kuimarisha kiwango chake zaidi na kuwa mtambo wa mabao ndani ya Yanga kwani ana sifa zote za kufanya hivyo.
“Nimemwambia azingatie mambo mawili. La kwanza kucheza zaidi ndani ya boksi la wapinzani, pili atulize presha, asiwe na haraka katika kuzitumia nafasi ambazo timu inazitengeneza, akifanya hivyo ataweza kuongeza idadi ya mabao kwa kuwa timu ina uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi lakini muda mwingi anashindwa kuzitumia kwa sababu anakosekana katika maeneo sahihi,” alisema Gamondi na kuongeza:
“Dube ni mshambuliaji bora mwenye akili nyingi, nguvu na kasi lakini zaidi uwezo wa kulenga (target) ambavyo sio rahisi kwa mshambuliaji kupata vyote hivyo, wengi unaweza kuwakuta wana sifa moja au mbili tu.”
Kutokana na hilo, Gamondi ni kama anamtengeneza Dube kuwa mshambuliaji wake kinara ndani ya kikosi cha kwanza cha Yanga, kwani mpaka sasa amemuanzisha katika mechi zote tatu za kimashindano walizocheza msimu huu akiwaacha nje Kennedy Musonda, Jean Baleke na Clement Mzize ambao wanacheza eneo moja la ushambuliaji.
Katika mechi nne ambazo Dube amefunga tangu atue Yanga kati ya saba alizocheza ni ile ya Yanga 1-0 TS Galaxy alipofunga dakika ya dakika 55 akimalizia pasi ya Stephane Aziz Ki. Hiyo ilikuwa nchini Afrika Kusini katika maandalizi ya msimu huu, kisha akafunga tena moja waliposhinda 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs hukohuko Afrika Kusini katika Toyota Cup.
Baada ya hapo, fainali ya Ngao ya Jamii dhidi Azam, alifunga bao moja dakika ya 19 akimalizia pasi ya Mudathir Yahya, Yanga ikishinda 4-1, kabla ya Jumamosi iliyopita kupachika lingine moja dakika ya tano Yanga iliposhinda 4-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi katika mchezo wa kwanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.