KUNA kitu kinakuja. Hiyo ni kauli ya Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids wakati akiendelea kujenga timu yenye wachezaji 15 wapya.
Miongoni mwa wachezaji hao yupo kiungo Awesu Awesu ambaye timu hiyo ilipambana vilivyo siku ya mwisho ya dirisha la usajili msimu huu kumalizana na KMC ili atue Msimbazi.
Simba katika usajili wa dirisha hili imewasajili kipa Moussa Camara, mabeki Kelvin Kijili, Abdulrazack Hamza, Valentine Nouma, Chamou Karaboue, viungo Awesu Awesu, Debora Fernandez Mavambo, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Omary Omary, Yusuf Kagoma na washambuliaji Jean Charles Ahoua, Valentino Mashaka, Steven Mukwala na Leonel Ateba.
Juzi Awesu alianza kuwapa furaha mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao la mwisho katika ushindi wa mabao 3-0 ilioupata katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya Tabora United iliyochezwa Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Fadlu aliyemkosa Awesu katika mechi mbili za Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na Coastal Union, amesema kiungo huyo anaweza kuwa mchezaji muhimu kikosini kutokana na uwezo mkubwa wa kufanya uamuzi.
“Ni mchezaji mwenye uwezo wa kufanya uamuzi pindi awapo na mpira lakini pia anatengeneza muunganiko mzuri wa kitimu hivyo naamini atakuwa mchezaji muhimu kwetu,” alisema.
Alichosema Fadlu kuhusu Awesu kinaonyesha anaandaliwa ufalme ndani ya Simba kwani mpaka sasa kuna ishara kama nne ambazo zimeanza kuonekana kuandaliwa kwake kuwa tegemeo siku za usoni.
Ishara ya kwanza ni nguvu ambayo Simba ilitumia katika usajili wa mchezaji huyo kuanzia gharama hadi namna ilivyoshughulikia suala lake na waajiri wake wa zamani, KMC.
Simba imetumia zaidi ya Sh150 milioni katika kufanikisha uhamisho huo baada ya kuonekana mchezaji huyo alivunja mkataba kiholela na timu yake ambapo kati ya hizo, Sh100 milioni zilienda kwa KMC na zilizobakia kwa mchezaji huyo.
Ishara nyingine ni muda wa kutosha wa kucheza ambao benchi la ufundi la Simba limekuwa likimpa Awesu licha ya ushindani mkubwa wa namba uliopo katika kikosi cha timu hiyo.
Wakati Simba ilipokuwa kambini Misri, Awesu alicheza mechi zote tatu za kirafiki ambazo timu hiyo ilicheza ambapo mbili alianza kikosini na moja alitokea benchi, baada ya hapo akawa katika kikosi cha kwanza katika Tamasha la Simba Day dhidi ya APR.
Hakucheza mechi mbili za Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na Coastal Union kwa vile usajili wake haukuwa umekamilika lakini juzi aliingia kutokea benchi akiwa badiliko la kwanza la kocha Fadlu Davids katika mchezo huo dhidi ya Tabora United dakika ya 31 akichukua nafasi ya Joshua Mutale aliyeumia.
Ishara ya tatu ni uhuru wa kucheza ambao benchi la ufundi la Simba limempa ndani ya uwanja kulinganisha na wachezaji wengine.
Katika mechi dhidi ya APR na ile ya Tabora United, Awesu Awesu ndiye mchezaji aliyekuwa huru kuzunguka katika sehemu nyingi za uwanja na hata kulinganisha na wachezaji wengine ambao Kocha Fadlu alionekana kuwasisitiza mara kwa mara wawepo katika nafasi walizohitajika kuwepo. Ishara ya mwisho ni namna ambavyo kundi kubwa la wachezaji limekuwa likimchezesha kwa kumpasia mpira mara kwa mara kulinganisha na wengine jambo ambalo limemfanya awe anagusa mpira na kujaribu kupiga pasi za mwisho mara nyingi.
Ndani ya Simba eneo la kiungo cha ushambuliaji analocheza Awesu kuna wachezaji wengine wanne ambao ni Saleh Karabaka, Edwin Balua, Ladaki Chasambi na Joshua Mutale. Chasambi na Karabaka wamekuwa wakisubiri, huku waliobaki wakipishana.