Fahamu siri ya msemo wa ‘mjomba ni mama’

Morogoro. Msemo wa, ‘mjomba ni mama’ unatumika katika jamii na makabila mbalimbali ya Kitanzania, lakini chimbuko lake ni Kabila la Waluguru linalopatikana Mkoa wa Morogoro.

Mjomba anayezungumziwa hapa ni yule aliyezaliwa tumbo moja na mwanamke.

Kwa Waluguru, wajomba wanapewa heshima kubwa na wanashikilia madaraka muhimu ndani ya familia kuliko baba.

Juma Ng’ondavi, mwenyeji wa Kijiji cha Tandai Kinole Wilaya ya Morogoro ambaye ni Mluguru, amefanya mahojiano maalumu na Mwananchi na kuhusu heshima ya kipekee anayopata mjomba katika jamii ya Waluguru.

Ng’ondavi anasema sababu kubwa ya heshima hii ni kwamba mjomba ndiye msemaji mkuu na mwakilishi wa mama katika uamuzi wa familia.

“Miaka ya zamani, binti alipotaka kuolewa mjomba alihusishwa na kutoa uamuzi wa mwisho. Hakuna aliyepinga uamuzi wa mjomba, hata kama binti au kijana amefariki dunia, mjomba ndiye mwenye mamlaka ya kuamua wapi na lini atazikwa. Baba anashirikishwa tu,” anasema Ng’ondavi.

Anasema hata talaka inapofikishwa, lazima iende kwanza kwa mjomba kabla ya baba. Mjomba pia hupewa taarifa kabla ya mtu mwingine yeyote pale kijana anapotakiwa kwenda jandoni.

Aidha, mjomba pekee ndiye mwenye mamlaka ya kutunza watoto wa dada yake endapo wazazi watakuwa wamefariki dunia pamoja na kufanya mgawanyo wa mali.

“Kama kuna mashamba au nyumba zilizochwa na marehemu, mjomba ndiye anayejua nani apewe nini. Hata kama binti amefiwa na mume, mjomba ndiye mwenye jukumu la kumtunza wakati wa eda hadi atakapopata mume mwingine,” anasema Ng’ondavi.

Anasema hata yeye watoto wa dada zake wanamthamini sana. Anapokuwa kwenye vikao vya familia, hakuna anayepingana na kauli yake, ingawa anakubali kuwapa nafasi wapwa zake kujieleza na kutoa mawazo yao, bila kupunguza heshima yake kama mjomba.

“Mpaka shemeji zangu wanatambua nafasi yangu kama mjomba wa watoto wao,” anasema.

Uamuzi hutoka wapi binti anapoolewa

Ng’ondavi anasema kwa mila za Kiluguru, binti haruhusiwi kuolewa na mtu wa ukoo wake.

“Wazee lazima waweke kikao na kijana anayetaka kuoa na kumchunguza ukoo wa mchumba wake. Ikiwa ukoo unafanana, mjomba anaweza kupinga ndoa hiyo hata kama wahusika wamependana,” anasema Ng’ondavi.

Kwa mila za Kiluguru, mjomba ndiye anayepanga mahali ambako mpwa wake wa kike akaolewe, huku baba akiwa na nafasi ndogo katika kupanga shughuli za harusi, jambo linalotofautiana na mila za makabila mengine ya kaskazini na bara, baba anakuwa na sauti kubwa katika uamuzi wa watoto.

Heri Hoza, kijana wa jamii ya Kiluguru kutoka Kijiji cha Mkuyuni anasema licha ya kufanikiwa kusoma hadi kufikia kiwango cha digrii, amekuwa akiheshimu na kufuata mila na desturi za Kiluguru, ikiwamo kumthamini mjomba wake.

Hoza alitaja sababu tatu za mwanamume wa Kiluguru kumthamini mtoto wa dada yake zaidi ya mtoto wake mwenyewe  ni za kisayansi (kibailojia), kulinda ukoo na mfumo jike.

Anasema mwanamume wa Kiluguru anaamini kuwa mtoto wa dada yake ndiye damu yake ya kweli kwa sababu anatoka tumboni kwa dada yake, tofauti na mtoto wake mwenyewe ambaye kwa maoni yake, hawezi kuwa na uhakika kama ni damu yake halisi.

“Mama ndiye anayejua mtoto ni wa nani, lakini mtoto wa dada yake hana shaka naye kwa kuwa anajua ametoka tumboni kwa dada yake,” anasema Hoza.

“Hata mimi, mtoto wa dada yangu ndiye ndugu yangu na ndiye damu yangu, lakini mtoto wa kaka yangu kwa mila ya Kiluguru si damu yangu, kwa sababu sina hakika kama ni wa kaka yangu. Yawezekana kaka kasingiziwa, lakini sio rahisi haiwezekani mama asingiziwe mtoto kwa sababu yeye ndiye anayebeba mimba na ndiye anayezaa.”

Hoza anasema kwa msingi huo mjomba anakuwa na haki zote kwa mtoto wa dada yake kuliko watoto wengine.

Hata anapochuma mali, anaweza kumkabidhi mtoto wa dada yake badala ya mtoto wake akiamini mali hizo zikiwa mikononi mwa mpwa wake zitakuwa salama zaidi kuliko akiwaachia watoto wake.

“Kwenye mila za Kiluguru kuna ukoo ambao unatoka kwa mama na unatoka kwa baba. Hata hivyo, ukoo huu unaweza kupotea ama kufutwa hasa pale mtoto wa kike anapozalishwa na mwanamume bila ya kumtolea mahari na pia mwanamume huyo akimbie mimba. Hapo ndipo mjomba anapochukua uamuzi wa kufuta mtala (ubini) wa huyo mtoto aliyezaliwa na badala yake atampa jina la ukoo ambalo litatoka kwa mama,” amesema Hoza.

“Kwa mfano, ukoo wangu ni Magari. Halafu mtoto wa dada yangu kapata ujauzito na huyo mwanamume kakimbia. Mjomba moja kwa moja anahusika kwenye matunzo ya mtoto wa dada yake na hata huyo mjukuu. Nina uwezo wa kufuta majina aliyopewa na baba yake huyo mtoto na kuamua kumpa jina la ukoo wangu,” amesema.

Shani Mohamed alipozungumza na Mwananchi amesema binti wa Kiluguru wakati wa kuchezwa ngoma lazima awekwe ndani zaidi ya wiki mbili na siku ya kutoka (kunema), shughuli hiyo inafanyika kwa mjomba.

Anasema hata siku ya kunemwa akiwa mkoleni, anafundwa na lazima mjomba atokee, ndipo ngoma hupigwa na kuimba, “jamani kolo huyo hana udodo,” wakimaanisha kuwa mjomba huyo hana udogo.

Amesema kwa mila ya Waluguru, mjomba anaheshimika na ana sauti mbele ya wapwa zake, ndiyo maana Mluguru anaweza kumpisha kiti ama kumwamkia mjomba wake hata kama amempita umri.

“Hata ukifanya makosa nyumbani, baba na mama wakikufukuza, sehemu pekee na ya salama ya kukimbilia ni kwa mjomba. Na ikitokea kijana wa Kiluguru ameenda kijijini kusalimia akiwa na zawadi, mtu wa kwanza kumpa zawadi ni mjomba wake. Atamkabidhi zawadi zote, mjomba akisharidhika ndipo atawapelekea baba na watu wengine,” amesema Mohamed.

Naye Robert Francis anasema jamii ya Kiluguru inaishi kwa kufuata mfumo jike ambao pia hutumiwa na jamii za makabila mengine ya Pwani kama vile Wazaramo, Wakwere, Wakutu, Wakam na Wandengereko, mwanamke ndiye mwenye kuongeza ukoo.

Francis, ambaye ni Mluguru na msomi wa Shahada ya Uzamili katika masomo ya sayansi ya siasa na utawala wa umma,  amesema ukiondoa masuala ya imani za dini, kisayansi na kibailojia, mtoto ni wa mama.

Anasema baba kazi yake ni kuweka mbegu tu, lakini mama ndiye anayebeba mimba, anayejifungua na anayelea. Hata tabia za mtoto mara nyingi hutokana na tabia za mama.

“Kwa kutambua hilo, ndiyo maana jamii ya Waluguru inamthamini sana mwanamke kwa kuwa tangu zamani anaonekana ni kiumbe dhaifu. Hapo ndipo mjomba anapewa madaraka yote ya mama. Kifupi, mjomba ni mwakilishi wa mama katika masuala yote. Ikitokea mtoto wa dada anaolewa, basi mjomba ndiye anapanga mahari kwa niaba ya mama.

“Iwe mtoto amefariki dunia, mjomba ndiye anajua wapi kwa kuzika. Iwe mtoto kavunja ungo, mjomba ndiye anapanga shughuli ya ngoma, baba anakuwa mtu wa kushirikishwa kama alivyoshirikishwa kwenye kuweka mbegu tu,” amesema Francis.

Makabila mengine yanasemaje?

Aziz Habibu, ambaye anatoka jamii ya Kabila la Wapare lakini ni mkazi wa Morogoro kwa zaidi ya miaka 15, anasema mfumo huo wa Waluguru wa kumthamini mjomba na pia mjomba kumthamini mtoto wa dada yake ni mzuri, tofauti na mifumo ya makabila mengine ambayo inamthamini zaidi mtoto wa kiume na baba kuwa na maamuzi yote.

“Mifumo ya makabila mengine imekuwa ikisababisha mwingiliano wa makabila kwenye ukoo, kwani baba ndiye anayesambaza ukoo. Katika mwingiliano huo, mara nyingine kunasababisha migogoro hasa pale kabila moja linapokuwa na tamaduni tofauti na kabila jingine ndani ya familia. Migogoro hii mara nyingi hutokea pale binti ama kijana anapotaka kutoa ama kuolewa,” amesema Habibu.

Aidha, amesema kwa Waluguru mfumo wao ni kuongeza ukoo kwa kutumia mwanamke, na kwa kuwa mjomba ndiye mwenye mamlaka ya watoto wa dada yake, basi mila na desturi za mjomba ndizo zitakazotawala kwenye ukoo mzima.

Mfumo huo wa mila, desturi na tamaduni za Waluguru kwa sasa unaonekana kupungua nguvu kutokana na mabadiliko ya kimaendeleo, elimu, dini na hata mwingiliano wa makabila mengine.

Hata hivyo, yapo maeneo ya Mkoa wa Morogoro ambayo mila hizi bado zinazingatiwa na kufuatwa ni Kinole, Mkuyuni na Matombo.

Related Posts