WINGA wa Azam FC, Gibril Sillah, amebainisha kwamba amekuwa akimtumia kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua kama sehemu ya kuimarisha kiwango kutokana na kufurahishwa na namna anavyocheza mwenzake.
Kati ya vitu anavyovipenda Sillah kwa Pacome ni pale anapokuwa na mpira mguuni huwa hamuachii nafasi mpinzani kumnyang’anya, badala yake anatumia akili na nguvu kuufikisha sehemu sahihi.
“Pacome ni kati ya viungo bora ninaowakubali katika Ligi Kuu. Kuna wakati mwingine unaona ugumu akikabana na beki mmoja, muda mwingine wanalazimika kumkaba wawili ili kumzuia. Pamoja na hayo kuna wakati wanamshindwa.
“Kuna baadhi ya vitu anavyovifanya uwanjani ambavyo vinafanana na vile ninavyovifanya. Mfano kasi, umiliki wa mpira, mikimbio vipo vitu vingi ndio maana namfuatilia,” alisema winga huyo.
Pacome, raia wa Ivory Coast, msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara ukiwa ni wa kwanza kwake alimaliza na mabao saba akitoa asisti nne, wakati Sillah alimaliza na mabao manane na asisti sita.
“Msimu uliopita ulinifunza mengi, hivyo katika ligi inayoendelea ni kupigania malengo ya timu yatakayofanya ning’are katika asisti nyingi na kufunga mabao mengi zaidi,” alisema raia huyo wa Gambia.
Nje na uwanja, Sillah amefichua kuwa tayari ameanza kujifunza Kiswahili kwani anaweza kusalimiana na watu huku akivutiwa na hali ya amani iliyopo Tanzania.