Songea. Mahakama ya Rufani imeamuru kusikilizwa upya kwa kesi ya aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha jela, Said Hija, baada ya kubainika hapakuwepo ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ya kusikilizwa kwa kesi yake.
Hija alikamatwa na polisi Mei 21, 2020 eneo la Mkenda Wilaya ya Songea mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, akituhumiwa kusafirisha kilo 1.76 za dawa za kulevya aina ya heroin alizozificha kwenye soli za raba nne.
Amri ya kusikilizwa upya kwa kesi hiyo imetolewa jana Jumatatu Agosti 19, 2024 na majaji wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Omary Makungu baada ya Hija kukata rufaa kupinga adhabu hiyo aliyohukumiwa Februari mosi, 2023.
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa umeegemea katika ushahidi wa mashahidi watano kuthibitisha shitaka dhidi yake huku mshitakiwa huyo mbali na kukanusha mashitaka hayo, lakini aliegemea ushahidi wake mwenyewe kujitetea.
Tukio la kukamatwa lilivyokuwa
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, mrufani huyo alikamatwa Mei 21, 2020 eneo la Mkenda baada ya Ofisa wa Uhamiaji, Koplo Mussa Nassoro aliyekuwa shahidi wa tatu kutilia shaka raba zilizokuwa katika begi la mshitakiwa.
Koplo Nassoro aliomba msaada kutoka kwa shahidi wa 2 ambaye ni Ofisa wa Polisi aliyetajwa kwa jina moja la Chande aliyekuwepo zamu.
Shahidi huyo wa tatu alitilia shaka raba hizo nne kwa sababu soli zake zilionekana mpya na kuashiria kuna vitu vimewekwa katikati yake na soli hizo zilipoondolewa, kulipatikana paketi 12 zikiwa na unga mweupe.
Kwa upande wake, shahidi wa nne, Mrakibu wa Polisi (SP), Kulwa Kasile ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa upelelezi wilaya (OC-CID) Songea, alikwenda Kituo cha Polisi cha Mkenda Nakawale na kumfanyia mahojiano mshitakiwa huyo.
Juni 18, 2020, shahidi wa tano, Inspekta Msaidizi wa Polisi Shedrack Meshack alipeleka unga huo kwa mkemia mkuu wa Serikali.
Na baada ya shahidi wa kwanza, Theodori Ludanha kuufanyia uchunguzi maabara, alibaini ni dawa aina ya heroin.
Katika utetezi wake, mshitakiwa huyo aliegemea ushahidi wa kwamba hakuwepo eneo la tukio na kueleza kuwa, alikamatwa Mei 21, 2020 akiwa nyumbani kwake Temeke Wailes jijini Dar akiwa na mjomba wake.
Alieleza kuwa, waliondoka na mjomba wake Hemed Mbao, kwenda Songea Mei 24,2020 na kwamba tarehe ya kukamatwa kwake, alikuwa ametoka katika nyumba ya mjomba wake iliyopo eneo la Maenge Wilaya ya Songea.
Aliiambia Mahakama kabla ya kukamatwa alikuwa amepita dukani kununua muda wa maongezi kwa ajili ya simu yake na hapo dukani kukatokea kutoelewana kati yake na muuza duka na kuibuka mzozo uliovuta watu wengi.
Katikati ya mzozo huo, ndipo polisi walijitokeza na kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi ambako huko alifanyiwa upekuzi na hati yake ya kusafiria kuchukuliwa na anahisi hiyo ilichukuliwa baada ya kuonekana amesafiri nchi nyingi.
Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande mbili, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea aliyesikiliza kesi hiyo, Yose Mlyambina, alisema upande wa mashitaka ulikuwa umethibitisha shitaka dhidi yake pasipo kuacha shaka.
Hakuridhika na hukumu ya Jaji ya kutumikia kifungo cha maisha jela na kukata rufaa akiegemea sababu 13 lakini Mahakama ikafanyia kazi sababu moja, kuwa Jaji alikosea kisheria kwa kusikiliza kesi kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.
Katika hoja hiyo alieleza kuwa jaji alikosea kusikiliza shauri hilo kinyume na kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marejeo na Bunge na kuidhinishwa na Rais 2019.
Kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa Agosti 9, 2024, mrufani aliwakilishwa na Wakili Dickson Ndunguru wakati mjibu maombi, Wakili wa Serikali Baraka Mgaya aliunga mkono hoja hiyo ya rufaa iliyowasilishwa na wakili wa mrufani.
Wakili Mgaya alikiri kwamba usikilizwaji wa kesi hiyo ulifanyikwa pasipo idhini ya DPP kama kifungu cha 26(1) kinavyotaka na kwamba kukosekana na idhini hiyo kunafanya mwenendo wote wa kesi na hukumu uwe batili na unapaswa kufutwa.
Wakili huyo mwandamizi wa Serikali aliitaka Mahakama kuamuru kusikilizwa upya kwa kesi kwa kuwa ushahidi wa upande wa mashitaka uliopokewa kortini ulitosha na hakuna mashimo yatakayozibwa na jamhuri.
Hata hivyo, Wakili Ndunguru aliunga mkono msimamo huo wa wakili wa Serikali kuhusiana na ubatili wa mwenendo wa kesi na hukumu lakini akapinga hoja ya kesi kusikilizwa upya kwa kuwa itafanya jamhuri kuziba mashimo.
Katika hukumu yao jopo la majaji hao watatu walikubaliana na hoja za mawakili hao kuhusu ubatili wa mwenendo na hukumu kutokana na kutokuwepo kibali cha DPP na kubatilisha mwenendo huo na kufuta hukumu iliyotolewa.
Majaji hao walisema baada ya kupitia mwenendo wa shauri hilo, hawakubaliani na wakili wa mrufani kwamba wakiruhusu kusikilizwa kwa kesi hiyo, basi upande wa mashitaka ungetumia nafasi hiyo kuziba mashimo katika maeneo yenye udhaifu.
Kwa mujibu wa majaji hao, kosa ambalo mrufani anashitakiwa nalo ni kubwa na kwa ajili ya kutenda haki, wanaona ni vyema kesi hiyo ikasikilizwa upya kuanzia kwenye hatua kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa na mrufani ataendelea kubaki mahabusu.