Ripoti zilizotolewa na wizara ya afya hapa Kongo zinaonesha idadi ya wagonjwa waligundulika kuwa na homa ya Mpox imefikia 16,700 kutoka 16,000 siku chache zilizopita. Kwa jumla watu 570 wamekwishakufa kutokana na maradhi hayo.
Kutokana na athari hizo Waziri wa Afya Samuel Roger Kamba ametangaza baadhi ya hatua ili kupambana na kusambaa ugonjwa wa mpox.
Soma pia:Jamhuri ya Kongo yaripoti visa kadhaa vya homa ya nyani, mpox
Hatua hizo ni pamoja na kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuepuka ngono zembe, unadhifu wa mwili, kutokula nyama kibudu na kutowauguza wagonjwa.
“Lakini hatua muhimu ni ile ya chanjo. Tunawapa ifike hapa. Na tutakapoanza kuwapa watu chanjo, kipaumbele kitakuwa maeneo yaliyoathirika zaidi, maeneo tunayoyaita “hot-spot”. Lakini inabidi chanjo hiyo inayouzwa kwa bei ghali imfikie yule anayeihitaji.”
Soma pia: WHO yasema ni muhimu kujiandaa kudhibiti kusambaa kwa mpox
Waziri Kamba amesema vijana ni waathirika wakubwa kwa kuwa wengi walizaliwa baada ya kusimamishwa kwa chanjo.
Alisema “Kabla ya 1980 watu walikuwa wanakingwa na chanjo. Ilikuwa tatizo kubwa na kilichosimamisha kusambaa kwa ndui ilikuwa ni chanjo peke yake. Lakini chanjo ilisimamishwa baada ya ugonjwa huo kutoweka. Ndio maana vijana waliozaliwa baada ya kipindi hicho, hawana kinga mwilini na ndio maana wanaambukizwa kiurahisi.”
Soma pia: WHO yaitisha mkutano kuujadili ugonjwa wa homa ya nyani
Waziri huyo amesema chanjo hiyo inatarajiwa kuwasili wiki ijayo nchini humo na inatarajia kuwapatia chanjo watu zaidi ya milioni tatu. Japan na Marekani ndio wametangaza kuipatia Kongo chanjo hiyo.
Soma pia: Zaidi ya visa 18,700 vya mpox vyagunduliwa barani Afrika