LONDON, ENGLAND: SOKA kwa sasa umekuwa mchezo wa kitajiri. Na Ligi Kuu England inatoa matajiri wa kiwango cha juu kutokana na mishahara inayowalipa mastaa wake.
Wakati msimu mpya wa Ligi Kuu England 2024-25 ukianza kwa kasi, kuna mastaa wanafurahia kuwapo kwenye ligi hiyo kutokana na pesa nyingi wanazovuna.
Kama ilivyo kwa klabu zinazofanya usajili wa pesa nyingi, jambo hilo linakwenda sambamba na mishahara wanaowalipa wakali hao, ambapo kuna wachezaji wanalipwa mkwanja mkubwa sana.
Kwenye Ligi Kuu England, kuna orodha ya mastaa kibao wanaolipwa mishahara mkubwa, lakini wanaoongoza kwa sasa ni hawa hapa 10.
Dirisha la usajili bado halijafungwa, pengine anaweza kunaswa mchezaji mkubwa na kuja kuvunja 10 bora hiyo ya watu wenye mishahara mikubwa kwenye Ligi Kuu England.
Kwa mujibu wa Capology, hii ndiyo orodha ya wanasoka wenye mishahara mikubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England. Umewaona?
1. Kevin De Bruyne (Man City)
Mshahara: Pauni 400,000 kwa wiki
Hakuna ubishi, Kevin De Bruyne ni mchezaji mwenye mchango mkubwa zaidi kwenye kiungo ya Manchester City sambamba na Mhispaniola, Rodri. Kiungo huyo wa Kibelgiji atabaki kuwa mchezaji muhimu kwenye timu hiyo ya Etihad, akifunga mabao 102 na kuasisti mara 170 hadi sasa. Huduma yake bora ya uwanjani ndiyo inayomfanya alipwe kiasi hicho cha pesa na kuongoza kwenye Ligi Kuu England.
2. Erling Haaland (Man City)
Mshahara: Pauni 375,000 kwa wiki
Erling Haaland, msimu wa 2022/23, ulikuwa wa kwanza kwake kwenye Ligi Kuu England na hakika alifanyia kazi vyema kiasi cha mshahara anaolipwa kutokana na kile anachofanya uwanjani kwenye kikosi cha Manchester City. Staa huyo kwenye msimu wake wa kwanza tu alivunja rekodi ya mabao kwenye Ligi Kuu England baada ya kufunga mara 36, huku Man City wakitambua hilo kwa kumlipa Pauni 375,000 kwa wiki.
3. Mohamed Salah (Liverpool)
Mshahara: Pauni 350,000 kwa wiki
Mohamed Salah ameripotiwa kupokea Pauni 350,000 kwa wiki katika ujira wake anaolipwa huko kwenye kikosi cha Liverpool baada ya kusaini dili jipya mwaka 2022. Kinachoelezwa ni kwamba staa huyo anaweza kushawishika na kubadili timu kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini kwa kuthibitisha pesa anayolipwa, staa huyo ameanza kwa kufunga katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England msimu huu wa 2024/25. Katika mechi ya kwanza, Salah alifunga na kuasisti wakati ilipoichapa Ipswich Town 2-0.
Mshahara: Pauni 350,000 kwa wiki
Kiungo huyo wa Manchester United, Casemiro amelingana mshahara na Mo Salah huko Liverpool, ambapo Mbrazili huyo anaweka mfukoni Pauni 350,000 kwa huduma yake ya kila wiki huko Old Trafford. Bingwa huyo mara tano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya alijiunga na Man United kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 70 milioni akitokea Real Madrid. Msimu wake wa kwanza alikuwa bora sana uwanjani, kabla ya mambo kwenda kombo kwenye msimu wa pili. Lakini, wakati msimu huu mpya wa 2024-25 ukianza, matumaini ya kocha Erik ten Hag ni kwamba Casemiro atakuwa kwenye kiwango bora na kuipa ubingwa timu hiyo.
5. Bruno Fernandes (Man United)
Mshahara: Pauni 350,000 kwa wiki
Staa mwingine wa Manchester United anayelipwa sawa na Mo Salah na Casemiro ni kiungo wa Kireno, Bruno Fernandes. Staa huyo alijiunga na miamba hiyo mwaka 2020 aliponaswa kwenye dirisha la Januari, ambapo kwa sasa kwenye dili lake jipya alilosaini, ameongeza Pauni 100,000 kwa wiki, na hivyo kuondoka nyumbani na Pauni 350,000 kwa wiki, ambapo atalipwa kiwango hicho hadi Juni 2027. Ripoti zinadai kwamba kwa kulipwa kiwango hicho cha pesa, sasa kiungo huyo ameingia pia kwenye kundi la wachezaji wanaolipwa kibosi huko Old Trafford, akiwamo Marcus Rashford.
6. Raheem Sterling (Chelsea)
Mshahara: Pauni 325,000 kwa wiki
Mambo si shwari kabisa kazini kwake huko Chelsea kutokana na kutokuwa na uhakika wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza. Lakini, hilo wala halimfanyi Sterling kuondoka kwenye orodha ya wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye Ligi Kuu England kutokana na ukweli kwamba, anaweka kibindoni Pauni 325,000 kwa wiki. Kutokana na kukosa muda wa kutosha wa kucheza, Sterling kwa sasa anafikiria mpango wa kuachana na miamba hiyo ya Stamford Bridge kabla ya dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kufungwa.
7. Romelu Lukaku (Chelsea
Mshahara: Pauni 325,000 kwa wiki
Imepita miaka miwili, straika Romelu Lukaku haijaichezea Chelsea. Hata hivyo, hilo halimwondoi kwenye orodha ya wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa huko Stamford Bridge. Staa huyo alicheza kwa mkopo kwa misimu miwili iliyopita kwenye vikosi vya Inter Milan na AS Roma za huko Italia. Kinachoelezwa ni kwamba mkataba wake wa huko Chelsea, fowadi huyo analipwa Pauni 325,000 kwa wiki na anazivuna akiwa tu kwenye benchi na kuzurura kwenye timu nyingine. Kwa kile ambacho Chelsea ilipata ni kuwafungia mabao machache sana na hata alipokwenda AS Roma kwa mkopo msimu uliopita, alifunga mabao 13 pekee. Kocha wa Chelsea wa sasa, Enzo Maresca anafikiria tu namna ya kumpiga bei.
8. Marcus Rashford (Man United)
Mshahara: Pauni 300,000 kwa wiki
Manchester United imeamua kumtunuku kijana wao, Marcus Rashford kwa kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye Ligi Kuu England. Staa huyo alianzia soka lake kwenye kikosi hicho hicho na mkataba wake mpya alisaini kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka 2023 ambapo alisaini dili la kulipwa Pauni 300,000 kwa wiki. Rashford bado yupo kwenye kikosi cha Man United licha ya kuhusishwa sana na mpango wa kuachana na timu hiyo kwa kipindi cha hivi karibuni, alipohusishwa na timu kibao ikiwamo Paris Saint-Germain, ambao walidaiwa kumtaka ili akazibe pengo la Kylian Mbappe aliyetimkia Real Madrid.
9. Jack Grealish (Man City)
Mshahara: Pauni 300,000 kwa wiki
Ni kitu ulichokitarajia kumwona analipwa pesa nyingi baada ya ada iliyotumika kunasa saini yake kuwa Pauni 100 milioni. Manchester City ililipa pesa hiyo ili kumnasa Jack Grealish kutoka Aston Villa na baada ya kutua tu Etihad, winga huyo Mwingereza alikwenda kupandisha mshahara wake hadi Pauni 300,000 kwa wiki. Mabao 14 na asisti 18 katika mechi 125 alizochezea Man City ndicho kitu amefanya winga huyo hadi sasa, huku akimpa pigo kocha Pep Guardiola kwenye mechi za mwanzo za msimu huu kwenye Ligi Kuu England kutokana na kuwa majeruhi.
10. Bernardo Silva (Man City)
Mshahara: Pauni 300,000 kwa wiki
Bernardo Silva ni mchezaji muhimu sana kwenye mbinu za kocha Pep Guardiola katika kikosi chake cha Man City, ambapo staa huyo amekuwa moto kwelikweli ndani ya uwanja. Huduma yake bora ndicho kitu kinachomfanya mkali huyo wa Ureno kulipwa pesa nyingi, akipokea Pauni 300,000 kwa wiki. Mwanzoni mwa dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi staa huyo alihusishwa sana na mpango wa kuachana na Man City, lakini alibaki kwenye kikosi hicho cha Etihad na kuisaidia timu hiyo kushinda Ngao ya Jamii mwaka huu baada ya kufunga bao la kusawazisha kwenye mechi dhidi ya Manchester United kabla ya kunyakua taji hilo kwa ushindi wa mikwaju ya penalti.