Mtwara kusaini mikataba ya Sh23.5 bilioni ujenzi wa barabara

Mtwara. Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Mtwara, Zuwena Mvungi amesema mwaka huu wanatarajia kuingia mikataba 75 yenye thamani ya Sh23.5 bilioni.

Amesema hayo leo Jumanne Agosti 20, 2024 katika hafla ya utiaji saini mikataba 54 yenye thamani ya Sh17 bilioni.

Mvungi amesema miradi hiyo inayokwenda kutekelezwa itaamsha ari ya uwajibikaji na usimamiaji mzuri wa miradi mingine inayofuata.

 Katika awamu ya kwanza, amesema mikataba 54 yenye thamani ya Sh17.4 bilioni imesainiwa, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuwa na mikataba 21 yenye thamani ya Sh6.11 bilioni. “Na utekelezaji wa mikataba hii utaanza mara moja na itazingatia ubora na thamani ya fedha iliyosainiwa,” amesema Mvungi.

Mwakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya Rose, Selina Saria, akizungumza katika hafla hiyo amesisitiza umuhimu wa malipo kwa wakati.

Amesema ucheleweshaji wa malipo mara nyingi husababisha miradi kuchelewa huku akiiomba  Serikali kuhakikisha malipo yanatolewa kwa wakati ili kurahisisha utekelezaji wa miradi.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amewataka makandarasi kuhakikisha wanakamilisha miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango bora na kwa wakati, akionya usumbufu na ucheleweshaji wa miradi.

Kanali Sawala amesema baadhi ya makandarasi ni wasumbufu na wanapaswa kufuatiliwa kwa karibu.

“Makandarasi wenye tabia hiyo watatolewa kwenye miradi ya mkoa, ili kuepusha kuahirishwa kwa miradi mingine,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Related Posts