Ndege mpya ya Boeing iliyokwama jana kutua Zanzibar leo

Dar es Salaam. Ndege mpya ya Boeing B8787- Dreamliner iliyokwama kuwasili jana Jumatatu Agosti 19, 2024 kutokana na changamoto ya hali ya hewa sasa kupokewa leo Jumanne Zanzibar.

Kwa mujibu wa ratiba mpya iliyotolewa leo Jumanne Agosti 20, ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 262 inatarajiwa kutua saa 10:00 jioni kisiwani humo na kupokewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, Zanzibar.

Taarifa ilitolewa jana na kitengo cha uhusiano na mawasiliano kwa vyombo vya habari, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inasema mabadiliko hayo yamesababishwa na changamoto ya hali ya hewa ambayo ipo nje ya uwezo wao.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu leo Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Raqey Mohamed amesema hali ya hewa iliyobadilika ni ya Marekani iliponunuliwa ndege hiyo.

Hata hivyo, amesema sherehe za mapokezi ya ndege hiyo zitaanza saa 10:00 jioni.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 262 ina viti 22 vya daraja la biashara na viti 240 daraja la kawaida.

Pia, ina uwezo wa kubeba mizigo kati ya tani 15 hadi 20 kulingana na ujazo wa abiria na mizigo.

Hii ni ndege ya 15 kununuliwa na Serikali tangu mwaka 2016 ilipochukua hatua za kuifufua ATCL.

Related Posts