Ngoma Arusha kupigwa mwezi ujao

TIMU za kikapu Mkoa wa Arusha zimekuwa zikisubiri kwa muda mrefu kuanza kwa ligi mkoani humo, lakini hatimaye katibu mkuu wa Chama cha Kikapu mkoa, Barick Kilimba ametangaza rasmi tarehe ya kuanza.

Akizungumza na Mwanasposti, Kilimba alisema ligi hiyo inatarajiwa kuanza Septemba Mosi.

Hata hivyo kiongozi huyo hakusema sababu zilizofanya ligi hiyo ishindwe kuanza mapema, huku zile za mikoa mingine zikiwa katika hatua mbalimbali.

Alitaja timu zitakazoshiriki ligi hiyo upande wa wanaume kuwa ni Sinoni, Hooperz, Pamoja, IAA, Spider, Makumira, Baptist, Donbosco, Kings, Tico Tengeru na ATC.

Kwa upande wanawake ni Orkeeswa, IAA Ladies, City Queens na Tico Queens.

Wakati Kilimba akieleza hayo, kocha wa timu ya Pamoja, Phabian Mjarufu alisema wanaendelea na mazoezi katika viwanja vya Ngarenaro Sports Complex wakidhamiria kubeba ubingwa msimu huu.

Mjarufu alisema wanatarajia kuingiza timu mbili katika ligi hiyo ambazo Pamoja ya wakubwa na ya chini ya umri wa miaka 18.

Alisema timu zote mbili zinafundishwa na makocha Masanja Mjaba, Juma Ally, Collins, Vicent Eliudy pamoja na yeye.

Related Posts