TAMASHA kubwa la ngumi za kulipwa Mkoa wa Ruvuma, limepangwa kufanyika Septemba 8, 2024 kwenye Uwanja wa Majimaji uliopo Songea mkoani humo.
Muandaaji wa tamasha hilo, Jofrey Miti wa JBM Fitness Gym ya Lizaboni, alisema kuwa mapambano mbalimbali ya ngumi za kulipwa yatafanyika katika tamasha hilo lililopangwa kuanza saa 11:00 jioni.
Miti alisema kuwa bondia Chidi Benga wa Songea atapambana na Mbwana “Vandame” Ally wa Dar es Salaam katika pambano la uzito wa Super Mddle, wakati James Ntanga wa Songea atazichapa na James Kiyeyeu wa Iringa katika pambano la raundi sita la uzito wa super light.
Pia kutakutakuwa na pambano la uzito wa cruiser ambapo bondia Doza Mnyama wa Songea atazipiga na Sadi Tompoo wa Dar es Salaam huku Taimu Saidi akipanda ulingoni kupambana na Alex “Big Dad” Phillemon wa Mbeya katika pambano la raundi sita la uzito wa juu, Heavyweight.
Pia kutakuwa na pambano la uzito wa super light la mabondia wa kike kati ya Fatuma Yazidu wa Dar es Salaam dhidi ya Suzana Mhagama wa Iringa na bondia Mussa Chitepete wa Songea atapambana na Festo Chipona wa Dar es Salaam.
Kwa upande wake, mratibu wa tamasha hilo, bondia wa zamani, Omari Yazidu alisema maandalizi yote muhimu yanaendelea vizuri na kuwataka wadau wa mchezo wa ngumi za kulipwa kufika kwa wingi siku ya tamasha hilo.
“Tunatarajia kuwa na mapambano makali yenye ushindani wa hali ya juu. Tunatarajia Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Damas Ndumbaro ambaye ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma pamoja na Wabunge wote wa majimbo ya uchaguzi kuhudhuria tamasha hilo,” alisema Yazidu.