Rais Ruto apata ushindi Mahakama ya Juu

Nairobi. Mahakama ya Juu zaidi nchini Kenya imesimamisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa uliobatilisha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023.

Kwa mujibu wa gazeti la Nation, katika uamuzi ambao sasa unairuhusu Serikali kuendelea kukusanya kodi kwa kutumia sheria hiyo, Mahakama hiyo ilirejelea masilahi ya umma, ikisema kusimamishwa kwa sheria hiyo kutasaidia kudumisha utulivu katika mchakato unaoendelea wa bajeti na mgawo wa fedha.

“Kwa kuzingatia masilahi ya umma katika suala hili, tunaagiza rufaa isikilizwe  haraka iwezekanavyo baada ya uamuzi huu kutolewa,” umeeleza uamuzi wa majaji Martha Koome, Philomena Mwilu, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola, William Ouko na Mohammed Ibrahim.

Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 imekuwa ikipingwa kisheria, walalamikaji wakidai haikuzingatia ushirikishwaji wa umma.

Serikali ikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu, Bunge la Kitaifa na Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA), walikata rufaa katika Mahakama ya Juu zaidi.

Katika notisi ya maombi iliyowasilishwa mbele ya Mahakama hiyo, Serikali ilitaka kusimamishwa kwa utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama ya Rufaa hadi rufaa iliyokatwa itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Walalamikaji walidai uamuzi wa Mahakama ya Rufaa unasababisha hali tata, Serikali ikilazimika kutegemea Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha unaokuja, kwa kuwa Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2024 ulikuwa umesitishwa.

Walalamikaji walisema kubatilishwa kwa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 kutasababisha nakisi ya mapato ya Shilingi 240 bilioni za Kenya ambayo haiwezi kurejeshwa isipokuwa amri za kusimamisha utekelezaji zitolewe kwa haraka.

Walibainisha hali hiyo inaleta changamoto kubwa kwa sera ya fedha na uchumi wa Taifa.

Serikali ilieleza uamuzi wa kubatilisha sheria hiyo unaweza kusababisha mgogoro wa kikatiba kwa kuzuia uwezo wa serikali kukusanya na kusambaza fedha kwa mujibu wa sheria.

Usumbufu huo walieleza unaweza kusababisha kukwama kwa huduma muhimu za umma, jambo ambalo linaweza kusababisha serikali kushindwa kufanya kazi kabisa.

Waombaji walidai Serikali inaweza kulazimika kukopa fedha kufidia nakisi ya kifedha, jambo ambalo linaweza kuongeza deni la umma na mfumuko wa bei.

Walidai pia kuwa uamuzi huo unaiweka Serikali katika hatari ya changamoto nyingi za kisheria, ikiwa ni pamoja na mashtaka kutoka kwa wadau walioathiriwa na usumbufu katika shughuli za kifedha.

KRA ilidai mfumo wa ukusanyaji kodi ulikuwa umenunuliwa na kuanza kutumika, hivyo  kubatilishwa kwa sheria  kutaifanya Serikali kurejesha mfumo wa zamani, jambo ambalo litakuwa na gharama kubwa na kusababisha usumbufu.

Wajibu maombi walidai kutoa amri zinazotafutwa hakutakuwa na manufaa kwa masilahi ya umma.

Walidai iwapo rufaa iliyounganishwa itashindwa, Wakenya wanaweza kutozwa kodi zisizo za kikatiba kwa muda mrefu.

Pia walidai hakuna nafasi kwa watu kurudishiwa kodi zilizolipwa chini ya Sheria ya Fedha ya 2023.

Wajibu maombi 50 walidai Kifungu cha 208 cha Katiba kinaanzisha Hazina ya Dharura kwa ajili ya dharura au hali zisizotarajiwa, hivyo serikali haiwezi kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kifedha.

Wakati wa kutoa uamuzi, Mahakama ya Juu ilisema, “kwa upande wetu, tukizingatia hali ya sintofahamu kuhusu hatua za kukusanya mapato na ugumu unaoweza kutokea katika shughuli za Serikali Kuu na zile za kaunti kama ilivyosemwa na waombaji, pamoja na athari kubwa za kutangazwa kwa Sheria ya Fedha ya 2023 kuwa kinyume cha Katiba, tumeshawishika kuwa rufaa iliyounganishwa inaweza kupoteza maana. Zaidi ya hayo, kwa mtazamo wa awali, hatuamini kuwa matokeo ya tangazo hilo yatakuwa na uwezo wa kurekebishwa endapo rufaa iliyounganishwa itafanikiwa.”

Uamuzi huo unamaanisha kuwa Wakenya wataendelea kulipa kodi zote zilizomo kwenye sheria inayopingwa, ikiwa ni pamoja na asilimia 16 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mafuta.

Rufaa hiyo itatajwa mbele ya msajili msaidizi wa mahakama hiyo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa maagizo ya awali kuhusu uwasilishaji wa stakabadhi yametekelezwa.

Rufaa itasikilizwa kwa njia ya mtandao Septemba 10 na 11, 2024.

Related Posts