RAIS WA TLS AHOJI MAMLAKA YA WAZIRIKATIKA KUFUTA VIJIJI NA VITONGOJI KATIKA ENEO LA NGORONGORO – MWANAHARAKATI MZALENDO

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amehoji uhalali wa hatua iliyochukuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ya kufuta baadhi ya vijiji na vitongoji vilivyopo katika eneo la Ngorongoro. Mwabukusi, akizungumza asubuhi ya Jumanne, Agosti 20, 2024, jijini Dar es Salaam, alieleza wasiwasi wake kuhusu tafsiri na utekelezaji wa sheria iliyotumika katika uamuzi huo.

Mwabukusi alisema kuwa, baada ya kupitia vifungu vya sheria husika, hana shaka kwamba hakuna kifungu chochote kinachompa Waziri mamlaka ya kufuta vijiji na vitongoji kama ilivyoelezwa. “Kifungu cha 30 alichokitumia Waziri ni tafsiri ya upotovu na ni kinyume cha sheria. Tunamtaka Waziri mwenye dhamana atoke atuoneshe hiyo sheria tofauti na ile ambayo wengine wote tunayo ni ipi? Ilitungwa lini na nani kupitia bunge lipi?” alihoji Mwabukusi.

Aliongeza kuwa kifungu cha 30 cha sheria kinachozungumzia mamlaka ya Waziri hakijampa Waziri mamlaka ya kufuta vijiji au vitongoji. Alisisitiza kuwa, Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa watu wa asili katika maeneo yao ni watu ambao walikuwepo kabla ya sheria hizi kuanza kufanya kazi. “Unaweza kuweka mipaka lakini huwezi kuwafuta watu kwenye eneo lao la asili na wala Waziri hana hayo mamlaka kwa mujibu wa sheria aliyodai kuitumia,” alisema.

Mwabukusi alitoa wito kwa Waziri kutoa ufafanuzi wa kisheria juu ya hatua alizochukua, akisisitiza kuwa suala hili linahitaji uwazi wa kisheria ili kuepusha migogoro na ukiukwaji wa haki za watu wa asili wa eneo la Ngorongoro.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts