Dar es Salaam. Uwekezaji uliofanywa na Serikali umetajwa kuwa sababu ya usafirishaji mizigo kupitia Bandari ya Mtwara kuongezeka mara nane zaidi kati ya mwaka 2021 hadi mwaka 2023, Takwimu Msingi za Tanzania 2023 zinaeleza.
Uwekezaji huo unatajwa kuvutia na kuwezesha meli kubwa kutia nanga kwa ajili ya kubeba mizigo hususani makaa ya mawe yanayosafirishwa zaidi kupitia bandari hiyo.
Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2023 zinazoangazia usafirishaji kwa njia ya maji kupitia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, zinaonyesha bandari kuinuka kutoka mavumbini na kuonyesha utendaji ambao haukutarajiwa ndani ya muda mfupi.
Ripoti hii ambayo inataja chanzo cha takwimu zilizotumiwa zinatokana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), zinaonyesha usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Mtwara uliongezeka kutoka tani 204,000 mwaka 2021 hadi tani zaidi ya milioni 1.67 mwaka 2023.
“Siri kubwa ni uwekezaji uliofanywa na Serikali kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa gati jipya lililokamilika ujenzi wake Desemba 2020 lenye urefu wa mita 300, kina cha kuanzia mita 13 na uwezo wa kuegesha meli hadi zenye mita 230,” amesema Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi.
Alipozungumza na Mwananchi, Nyathi amesema maboresho hayo yalifanya sasa meli zilizo na uwezo wa kubeba hadi tani 65,000 kwa wakati mmoja kutia nanga ikilinganishwa na uwezo wa tani 45,000 iliyokuwpo awali.
Amesema ujenzi huo uliogharimu Sh157.8 bilioni ulienda sambamba na kuiongezea uwezo bandari katika kuhudumia shehena za mizigo kutoka tani 400,000 kwa mwaka hadi zaidi ya tani milioni moja.
“Pia, Serikali ilinunua mitambo ya kisasa ya kuhudumia meli na makasha hali iliyopelekea kuvutia zaidi wafanyabiashara mbalimbali walioamua kuleta meli kubwa zaidi hususani zinazobeba shehena ya makaa ya mawe,” amesema Nyathi.
Mbali na maboresho hayo pia kama bandari imetoa vivutio mbalimbali vya tozo kwa kutoa tozo maalumu za usafirishaji wa makaa ya mawe kufikia Sh16,236 (Dola 6 za Marekani) kwa tani na pia imepunguza tozo za mizigo mingine kwa takribani asilimia 30 ukilinganisha na viwango vilivyopo kwenye mwongozo wa tozo.
Hata hivyo, ripoti hii inaonyesha kuwa si kiwango cha mizigo pekee ndiyo kimepaa katika Bandari ya Mtwara bali hata idadi ya meli zinazofika iliongezeka.
Mwaka 2021 ni meli 125 pekee ndiyo zilitia nanga bandarini hapo lakini mwaka 2023 meli 332 ziliweka nanga kwa ajili ya kubeba mizigo.
Kuhusu usafirishaji wa makaa ya mawe ambao meneja ameuzungumzia, umeangaziwa pia katika ripoti hii.
Ripoti hii inataja kuwapo kwa ongezeko la makaa ya mawe yanayozalishwa nchini kati ya mwaka 2021 hadi 2023 ambayo huenda kutokana na kuwapo kwa urahisi katika kuyasafirisha kwenda katika masoko mbalimbali duniani.
Takwimu zinaonyesha uzalishaji wa makaa ya mawe uliongezeka kutoka tani 976,319 mwaka 2021 hadi kufikia tani milioni 3.256 mwaka 2023.
Uzalishaji huu wa makaa ya mawe ulianza kushuhudiwa kuongezeka tangu mwaka 2020 kutoka tani 689,989 na haukuwahi kushuka.
Mbali na makaa ya mawe yanayosafirishwa sasa, Tanzania bado inayo hifadhi nyingine ya tanimilioni 428 ambayo bado haijaanza kuchimbwa.
Makaa hayo yaligunduliwa mwaka 2013 katika ardhi ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe sambamba na chuma katika eneo la Mchuchuma na Liganga.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika kipindi hicho makaa ya mawe yapo katika eneo la ukubwa wa mraba 30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140.
Mbali na ile ya Mtwara kufanya vizuri, ripoti hii pia inaonyesha namna ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam unavyoendelea kushuhudiwa.
Bandari ya Dar es Salaam ambayo imekuwa ikifanyiwa maboresho mbalimbali ikiwamo uwekezaji kwa kukaribisha kampuni za nje, uhudumiaji wa mizigo uliongezeka kutoka tani milioni 17.06 mwaka 2021 hadi tani milioni 22.91.
Uhudumiaji huo wa mizigo ulienda sambamba na uhudumiajii wa meli kutoka 1,610 hadi meli 1,918 mtawaliwa.
Katika Bandari ya Tanga usafirishaji mizigo ulionekana kushuka kidogo kwani tani za mizigo zilizohudumiwa mwaka 2023 zilikuwa 976,000 kutoka tani 984,000 zilizokuwapo mwaka 2021.
Dadi ya meli nazo zilifikia 209 mwaka 2023 kutoka meli 156 mwaka 2021.
Hata hivyo, tofauti na Bandari ya Mtwara ambako hakukuwa na taarifa za abiria waliosafiri kwa njia ya maji, Bandari ya Tanga na Dar es Salaam kulikuwa na takwimu hizo.
Bandari ya Dar es Salaam inatajwa kuhudumia wananchi milioni 2.4 mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko kutoka abiria milioni 1.6 milioni mwaka 2021.
Kwa Tanga, idadi ya abiria nayo ilionekana kushuka kufikia 56,000 mwaka 2023 kutoka abiria 92,000 mwaka 2023.
Wakati Bandari ya Tanga ikilegalega katika utendaji, bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya mwaka 2024/2025 iliyosomwa bungeni jijini Dodoma na waziri wake, Profesa Makame Mbarawa ambaye ni waziri kiongozi wa wizara hiyo, ilianisha mikakati waliyonayo katika mwaka huu wa fedha.
Profesa Mbarawa alisema mradi wa kuboresha Bandari ya Tanga utakaotekelezwa na Serikali kwa kutumia fedha zitokanazo na vyanzo vya mapato ya TPA unalenga kuiwezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa za mzigo wa mafuta.
Kupitia mradi huo, Serikali itaendelea na shughuli mbalimbali ikiwamo ujenzi wa gati na miundombinu ya kupokelea na kusafirisha mafuta katika eneo la Raskazone – Tanga na kujenga gati la kuhudumia makasha na abiria na kupanua lango la kuingilia meli.
Lakini si Bandari ya Tanga pekee itakayonufaika bali na ile ya Mtwara ipo kwenye miikakati ya Serikali.
Mradi utakaotekelezwa katika bandari hiyo utaiwezesha kuhudumia meli mbalimbali zikiwamo za mzigo mchafu.
“Serikali kupitia mradi huu, itaendelea na shughuli za ujenzi wa bandari kwa ajili ya kuhudumia shehena ya mzigo mchafu ambao unaweza kuchafua mazingira. Mizigo hiyo ni pamoja na makaa ya mawe na saruji katika eneo la Kisiwa Mgao,” alisema Profesa Mbarawa.
Pia, TPA itaendelea na ukarabati wa maeneo ya kuhudumia shehena na miundombinu ya barabara zinazoingia bandarini.