Uhaba wa walimu katika shule za umma haujapoa nchini. Taarifa zinaonyesha kuna nakisi ya walimu wa elimu ya awali na ya msingi zaidi ya 116,885 ili kuweka sawa uwiano wa walimu kwa wanafunzi
Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa 2023 kilichotolewa na Wizara ya Fedha, Juni 13, 2024, shule za msingi pekee zinahitaji walimu 64,001 ili kuwa na uwiano uliopangwa na Serikali.
Taarifa njema iliyopo angalau Serikali ina kitu inafanya, nayo ni hatua ya kuajiri walimu 12,000 katika mwaka wa fedha 2024/2025. Je, idadi hiyo itasaidia kupunguza uhaba?
Wakati Serikali ikijihimu kupunguza nakisi hiyo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) inatajwa kuwa njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto ya walimu
Kwa mfano, kupitia Tehama na teknolojia zake, hiyo mwalimu mmoja anaweza kufundisha maelfu ya wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hilo linaweza kufanyika kwa kutumia njia za kitehama kama vile mwalimu kurekodi kipindi na kutuma mtandaoni, matumizi ya video na nyinginezo mbalimbali.
Hata hivyo, swali linabaki mazingira ya shule za umma ni wezeshi kwa Tehama kutekelezwa?
Ili Tehama ifanye kazi kunahitajika huduma muhimu za intaneti na nishati ya umeme, lakini takwimu za elimu msingi za 2021 zinaonyesha kuwapo kwa shule za msingi 7492 ambazo hazikuwa na umeme kati ya shule 16, 656 zilizokuwapo.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, mikoa iliyoongoza kwa kuwa na shule zisizokuwa na nishati ya umeme ni Ruvuma asilimia 32, Kigoma asilimia 25, Tabora asilimia 33, Shinyanga asilimia 34.8 na Mtwara asilimia 34.4.
Bila shaka hali hii inaweka kigingi hata pale Serikali au wadau wanapotaka Tehama itumike kufundishia kama ilivyo katika mataifa mbalimbali duniani.
Mdau wa elimu, Catherine Sekwao anasema suala la ufundishaji kwa kutumia Tehama shuleni, ni gumu kutekelezeka.
Anasema bado Tanzania haijafikia lengo la asilimia 20 ya bajeti yake kuwekweza kwenye sekta ya elimu, hatua ambayo pengine ingekuwa chachu ya kuboresha hali ya utoaji elimu. Anasema kiwango hicho kinawezekana kwa kuwa nchi ina utajiri wa kutosha.
“Tuna fedha nyingi ambazo tunaweza kuelekeza kwenye elimu; ni namna tu ya kudhibiti matumizi au mapato yanayopatikana. Tunakusanya kodi nyingi kwa wananchi lakini kupitia rasilimali hizo ni kiasi gani tupate fedha za kuboresha elimu?”anahoji.
Anashauri kuwa ili ndoto ya kutumia Tehama shuleni ifanikiwe, ni muhimu kwa Taifa kuzuia mianya ya upotevu na wizi wa fedha zinazotolewa na Serikali kama inavyoelezwa mara kwa mara kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hoja ya Sekwao inaungwa mkono na mtaalamu wa teknolojia za elimu na sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Jordan mkoani Morogoro Dk Kassimu Nihuka, anaysema upatikanaji wa umeme shule za msingi ni moja ya changamoto tete nchini.
“Kutokuwepo kwa umeme ni kweli kunakwamisha matumizi ya teknolojia katika uboreshaji wa utoaji wa elimu hasa katika ujifunzaji na ufundishaji. Lakini pia kuna changamoto ya kukosekana miundombinu ya Tehama na walimu wenye umahiri wa matumizi ya teknolojia,’’ anaeleza.
Ili kuwezesha Tehema shuleni, Dk Nihuka anasema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ingefanya uchambuzi yakinifu kuona shule zenye mazingira mazuri yatakayowezesha matumizi ya Tehama.
Anasema badala ya kusubiri kutatua changamoto kote nchini, ni vyema Serikali ikaanza matumizi ya teknolojia katika baadhi ya shule zenye mazingira wezeshi kwa utoaji wa Tehama.
“Walimu walipewa vishkwambi lakini hakuna mafunzo waliyopata na hakuna anayewafuatilia namna wanavyotumia. Kinachotakiwa tuanze kutumia Tehama kwa utaratibu ili tuboreshe elimu yetu,”anafafanua.
Anaongeza: “Ukiangalia kwenye utekelezaji shuleni ni mdogo sana, teknolojia inatumika kuangalia matokeo ya wanafunzi ukija kwenye ufundishaji wapo nyuma ila miongozo na sera ipo vizuri sana kutenda ndio tatizo kubwa.’’
Aidha, Dk Nihuka anasema kukosekana kwa matumizi bora ya Tehema ni changamoto ya sekta nzima ya elimu kwani hata shule za sekondari na vyuo vikuu hakuna mfumo wa matumizi ya Tehama.
Mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha anasema kinachokwaza matumizi ya Tehama shuleni ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa.
“Katika uwekaji wa mipango na kuanza utekelezaji, tunapaswa kuweka jicho la kipekee kwa kutenga bajeti maalumu eneo la miundombinu ya Tehama na umeme shuleni. Pia tuhamasishe wadau kuwekeza; yapo maeneo yana uwekezaji mkubwa wa madini, lakini shule zilizo karibu na eneo la uwekezaji zina hali mbaya, tuwatumie watu hao kuboresha miundombinu,”anasema.
Alistidia anatoa mbinu mbadala ya matumizi ya umeme wa jua shuleni, akisema utasaidia kufikiwa kwa malengo ya Tehama shule za msingi.
Naye, Hamidu Bobali, anasema tatizo lililopo halmashauri nyingi zinasubiri mambo mengi yafanywe na Serikali kuu, akitolea mfano umeme unaweza ukawepo karibu na shule lakini hauingizwi shuleni hadi Serikali kuu ifanye hivyo.
“Ni jambo muhimu halmashauri kutenga bajeti na kupeleka umeme shuleni. Umeme unahitajika sana, ukiona ufaulu unaongezeka naweza kutaja umechangiwa na uwepo wa umeme mijini na vijijini. Mwanzoni shule za mijini ndizo zilizokuwa zikifaulisha lakini sasa hata za vijijini zinafanya vyema, kwa hiyo halmshauri zitoe kipaumbele katika upelekaji wa umeme shuleni,”anaeleza.
Anasema kwa maendeleo ya dunia ya sasa, kunahitajia matumizi ya vishwambi na vifaa vingine katika ujifunzaji, hivyo walimu nao wanapaswa kujifunza mbinu mpya za ufundishaji kwa njia ya Tehama.
Ikiwa ni sehemu ya kuleta mageuzi kwenye ufundishaji, Serikali imekuja na mfumo wa ufundishaji uitwao Ufundishaji Mubashara (Live Teaching), ambao unawezesha wanafunzi wa shule nyingine nchini kuunganishwa na mwalimu anayefundisha katika shule moja.
Februari 14, 2024, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilitembelea Shule ya Sekondari Dodoma kujionea majaribio ya mfumo huo. Wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wakifuatilia mada iliyokuwa ikifundishwa na mwalimu aliyekuwa katika Shule ya Sekondari ya Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kujionea mfumo huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Denis Londo alisema wameridhishwa na mfumo huo, huku akiipongeza Serikali kwa kuja na teknolojia hiyo ambayo inakwenda kukuza kiwango cha elimu nchini.
“ Niipongeze Serikali yetu kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, tumejionea shule nyingi zikijengwa, uwekezaji wa elimu bila malipo hadi kidato cha sita na sasa teknolojia hii ya wanafunzi wa shule nyingine kushiriki kipindi cha masomo na wenzao waliopo Kibaha Sekondari,”alisema na kuongeza: “Rai yetu kama kamati ni kuitaka Tamisemi kuusimamia kikamilifu mfumo huu ili uweze kuleta tija kwa wanafunzi wetu nchini. ‘‘
Lakini niwatake wanafunzi hawa wanaonufaika na mfumo huu kuutumia kikamilifu ili waweze kufaidika nao kwenye masomo yao na kupata matokeo mazuri.’’