Simiyu yahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi serikali za mitaa

 

VIONGOZI wa Mkoa wa Simiyu wameanza kuhamasisha wananchi mkoani humo kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, ili waweze kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Simiyu … (endelea).

Akizungumzia kuhusu suala hilo hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi amewataka wananchi wa mkoa kujisajili katika orodha ya wapiga kura kwa wingi.

Kihongosi alisema wananchi watakapojiandikisha kwa wingi watakapata fursa ya kuchagua viongozi watakaowaongoza katika ngazi ya vijiji, vitongoji na mtaa.

“Nitoe wito kwa wananchi wote wa Simiyu wajitokeze kwa wingi kujisajili na wakati wa uchaguzi hakikisheni mnapiga kura kuchagua viongozi wazuri, waadilifu, wazalendo na wachapakazi ambao watakwenda kutoa utumishi wa wananchi kwa kuzingatia katiba,” alisema Kihongosi.

Naye Diwani wa Kata ya Bariadi iliyopo mkoani humo, Kija John, alisema wameanza kufanya mikutano ya hadhara ili kuyafikia makundi mbalimbali yanayohitajika kupiga kura, kwa ajili ya kuwahamasisha kushiriki uchaguzi huo.

“Tumeshaanza kufanya mikutano ya hadhara ili kuhamasisha watu wa makundi mbalimbali ambayo yanahitajika kwenda kuchagua viongozi wa kujenga Serikali yetu na kusaidia jamii,” alisema Kija.

About The Author

Related Posts