Tanzania, Kamanda ahamishwa baada ya kauli iliyozusha hasira – DW – 19.08.2024

Sakata la binti aliyebakwa na kulawitiwa nchini Tanzania, limechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo, IGP, Camilius Wambura kumuhamisha kamanda wa polisi mkoani Dodoma, RPC Theopista Mallya na nafasi yake kuchukuliwa na George Katabazi, huku jeshi hilo likitangaza kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti wa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam. 

Hatua hiyo ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Dodoma Theopista Mallya kuhamishwa katika wadhifa huo, imeendelea kuibua hasira na maoni mseto kutoka kwa watu tofauti nchini Tanzania yakiwemo makundi mbalimbali ya kutetea haki za binadamu.

Soma pia: Polisi wa mgodi walaumiwa kwa mauaji Tanzania

Jeshi la polisi nchini Tanzania kupitia mkuu wa jeshi hilo, Camilius Wambura limemuondoa aliyekuwa RPC mkoani Dodoma, ikiwa ni siku moja tu mara baada ya kamanda huyo wa polisi, kunukuliwa katika vyombo vya habari akisema kuwa binti aliyebakwa na kulawitiwa alikuwa ‘kama’ kahaba na kwamba katika uchunguzi Jeshi la Polisi lilibaini vijana hao wanaotuhumiwa kwa madai ya kutumwa, walikiri kutoagizwa na askari kama ilivyoelezwa.

Watu mbalimbali waliozungumza na DW wameonyesha kushangazwa na kauli ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Dodoma huku wakisema kuwa hata kama binti huyo alikuwa anajiuza mwili hakupaswa kufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili vilivyotweza utu wake.

Kauli yenye ukakasi ya polisi yazusha hasira
Hatua ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Dodoma Theopista Mallya kuhamishwa katika wadhifa huo, imeendelea kuibua hasira na maoni msetoPicha: DW/S. Khamis

Kwa upande wake wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Tanzania, wanasema kuwa habari hiyo ni ya huzuni na masikitiko makubwa kwa afisa wa jeshi la polisi kutoa kauli kama hiyo.

Soma pia: UN yalaani unyanyasaji dhidi ya wafanyakazi wa kiutu

Hata hivyo, jeshi la polisi nchini Tanzania limekanusha kauli hiyo iliyotolewa na aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Dodoma na kusema kuwa si msimamo wa jeshi hilo, bali kauli sahihi ni zile zilizotolewa na msemaji wa jeshi hilo kwa umma Agosti 4, 6 na 9 mwaka huu wa 2024.

Msingi wa Jeshi la Polisi Tanzania kutoa taarifa hiyo ni habari iliyochapishwa na moja ya gazeti nchini humu yenye kichwa cha habari kianchosema “RPC: Anayedaiwa kubakwa, kulawitiwa na vijana wa “afande” ni kama anajiuza.

Mnamo Agosti 4 mwaka huu, ilisambaa vidio katika mitandao ya kijamii ikionyesha vijana watano wakidaiwa kumbaka na kumuingilia kinyume cha maumbile binti anayedaiwa kuishi Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam na hivyo kuzua hasira kwa watu katika mitandao ya kijamii wakitaka waliohusika kufanya unyama huo wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.

Related Posts