Tanzania, Korea kujenga kituo cha utafiti wa madini

Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kuanzisha kituo cha utafiti wa madini na maabara kubwa ya uchambuzi wa madini itakayokuwa na jukumu la kukagua ubora na kiasi cha madini yanayozalishwa na wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo.

Ili kutekeleza mpango huo, leo Agosti 20, 2024 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambacho ni msimamizi wa ndani na Kampuni ya Serikali ya Korea Kusini (Yulho), wamesaini mkataba wa makubaliano (MoU).

Makubaliano hayo ni kwa kampuni ya ujenzi ya Korea Kusini kujenga taasisi chuoni hapo itakayosaidia wachimbaji madini na wazalishaji wa mafuta kupata teknolojia ili kuunda mnyororo wa thamani unaotakiwa katika sekta ya madini.

Miradi hiyo miwili yenye thamani ya Sh27 bilioni, inalenga kusaidia wavumbuzi na wataalamu kugundua maeneo ya uchimbaji madini na mbinu bora za kutambua madini yenyewe.

Mkataba huo unatoa muhtasari wa mbinu ya kina ya ushirikiano katika nyanja za utafiti wa madini na maendeleo ya rasilimali za kijiolojia, ukishughulikia mahitaji ya kitaaluma na ya viwanda katika eneo hilo.

Kupitia ushirikiano huo, UDSM na Yulho watafanya kazi pamoja kufikia malengo ya kuanzisha chuo cha utafiti wa madini na maabara ya uchambuzi wa madini.

“Pande zote mbili zitajihusisha kikamilifu katika kubadilishana taarifa za kitaaluma na data, pamoja na kushiriki katika semina na shughuli nyingine za ushirikiano zitakazohamasisha maendeleo ya pande zote katika uwanja huo,” inasema sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari.

Kutambua umuhimu wa kujenga uwezo, Yulho  inaweza kutoa ufadhili wa masomo kwa wafanyakazi na wanafunzi wa UDSM, hivyo kuimarisha zaidi maendeleo ya kitaaluma na taaluma ndani ya chuo kikuu.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, amesema makubaliano hayo ni muhimu kwa UDSM na Tanzania kwa jumla.

 “Hakuna shaka kwamba mpango huu utaongeza uwezo wa chuo kikuu chetu katika ufundishaji wake, utafiti na jitihada za huduma kwa umma.

“Utabadilisha uzoefu wa watafiti na wanafunzi kwani utaanzisha vifaa na mashine za kisasa. Hivyo, kuingiza teknolojia iliyopo katika uwanja wa jiolojia.”

Profesa Anangisye ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wale waliokuja kusaini mkataba kuwa uongozi wa chuo kikuu utatoa msaada wake kamili kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa wakati na vifaa hivyo vitatumika kwa ufanisi na kwa tija.

Ingawa hii siyo maabara ya kwanza ya utafiti wa madini nchini Tanzania, uwezo wake wa kupima aina zote za madini ndio unaufanya kuwa tofauti na vituo vingine vidogo vinavyolenga madini maalum pekee.

“Maabara hii itatusaidia kufanya uchambuzi wa madini yote yanayopatikana nchini, ikiwa ni pamoja na grafiti, nikeli na hata mabaki ya dhahabu,” amesema Dk Salama Abubakary, Kaimu Mkuu wa Shule ya Madini na Jiolojia.

“Kabla ya hili, Tanzania ililazimika kutuma baadhi ya madini kwenda Afrika Kusini, Kanada, na Australia kwa ajili ya uchunguzi.”

Rais wa Yulho, Jae Seong Lee amesema kampuni hiyo imejitolea kutoa juhudi zote zinazohitajika kuhakikisha kuanzishwa na uendeshaji wenye mafanikio wa chuo cha utafiti wa madini na maabara ya uchambuzi wa madini.

“Tunataka kuinua kiwango cha teknolojia katika maeneo haya kwa kushirikiana na UDSM. Tuna uwezo wa kurahisisha wachimbaji madini wa ndani kuepuka gharama kubwa za kusafirisha madini kwa ajili ya uchambuzi sehemu nyingine,” amesema.

Tume ya Madini (Tanzania) ina maabara iliyoko katika jengo la Shirika la Maendeleo ya Viwanda (TIRDO), Kimweri Avenue, Msasani Dar es Salaam.

Kazi kuu ya maabara hiyo ni kukagua ubora na kiasi cha madini yanayozalishwa na wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo.

“Kujengwa kwa maabara hii kubwa kunaleta mabadiliko chanya kwa kile ambacho tayari tunacho kama nchi,” amesema Dk Abubakary.

Related Posts