USHINDI ule wa medali ya dhahabu ya michezo ya Jumuiya ya Madola huko Christchurch, Newzealand, 1974, ukiambatana na rekodi ya dunia ulimweka Fibert Bayi juu kabisa ya orodha ya wanariadha bora duniani na kwa hakika kulipaisha sana jina la Tanzania.
Nakumbuka wakati mmoja niliambatana na timu ya Simba kwenda Nigeria na mara tu tulipofika hotelini mhudumu aliyetupokea hapo tulipomwambia tunatoka Tanzania akatuuliza “kwao Filbert Bayi?” uthibitisho halisi wa nguvu na ushawishi wa michezo.
Kwa hiyo Bayi akawa nyota halisi ya michezo inayowaka sana, akijizolea medali na tuzo mbalimbali kutoka kila kona duniani.
Mnamo mwaka 1975 alishinda na kuweka rikodi mpya ya dunia kwenye mbio za maili moja huko Kingston, Jamaica na mwaka huo huo akachaguliwa kuwa mwanamichezo bora barani Afrika kwenye tamasha kubwa la wanamichezo lililofanyika Congo Brazzaville.
Na ndipo ukaingia mwaka 1976, mwaka wa michezo ya Olimpiki iliyopangwa kufanyika Montreal Canada. Pamoja na kwamba Olimpiki ni mkusanyiko wa wanamichezo bora sana wa michezo mbalimbali kutoka kote duniani lakini michezo hii ya mwaka huu wa 1976 mapema kabisa ilibatizwa kuwa ni raundi ya pili ya marudiano ya mpambano baina ya Filbert Bayi na ‘mgomvi’ wake mkubwa John Walker wa Newzealand kwenye mbio za mita 1500. Ikawa inatusubiri tuone.
Hali hii ilieleweka vizuri sana na kuchukuliwa kwa uzito mkubwa serikalini. Mikakati, mipango na maandalizi makubwa ikawekwa siyo kwa Bayi peke yake bali kwa timu nzima ya Tanzania itakayoshiriki huko Montreal.
Kwa dhamira hii ni wazi Serikali ilikuwa imetambua uzito na faida kubwa inayopatikana na taifa kwa ushindi wa wanamichezo wetu kwenye michezo mikubwa ya kimataifa kama hii ya Olimpiki.
Kwa upande mwingine kipindi hiki cha miaka hii ya sabini na themanini ndicho kilichokuwa kipindi cha harakati nyingi na kubwa za ukombozi kwa nchi za kusini mwa Afrika na hasa harakati za kutaka kuachiliwa kwa mpigania uhuru Nelson Mandela na kuondolewa kwa sera ya kiubaguzi nchini Afrika Kusini. Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kabisa kwenye harakati hizi.
Kuna nyakati hata suala la ushirikiano wa kimichezo na nchi hiyo ya Afrika Kusini lilikuwa likizua mzozo mkubwa kwenye majukwaa ya majadiliano ya kimataifa. Vivyo hivyo dalili zilikuwa zimeanza kujitokeza za kuwepo kwa mvutano mkubwa wa kutaka kuzizuia nchi zilizo na ushirikiano wa kimichezo na Afrika ya Kusini zisiruhusiwe kushiriki huko Montreal.
Wakati fukuto hili likizidi kuimarika, hapa nyumbani maandalizi ya timu yetu nayo yalikuwa yakiendelea kwa kasi. Kwa mara nyingine nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari waliochaguliwa kwenda kuripoti kuhusu michezo hii na sote tuliokuwa kwenye orodha ya safari hii gharama zetu zote zililipwa na Serikali, tangu mavazi ya safari, suti, viatu, sare nyingine rasmi, masanduku, mifuko na kadhalika. Kwa ujumla ulifika wakati tulijua tuko vizuri na tuko tayari kwa michezo hiyo ya Montreal, Canada. Safari ilikuwa imeiva.
Lakini wakati muda ukiwa unakwenda mbio hivyo, siku moja majira ya saa tatu asubuhi nikapokea simu kutoka kwa mkurugenzi wa habari Ikulu, Sam Mdee. Katika hali isiyo ya kawaida, Mdee aliniambia nisubiri taarifa maalumu ya Serikali itakayotolewa mara tu baada ya kikao cha baraza la mawaziri kitakachoongozwa Rais, Mwalimu Julius Nyerere.
Kwamba Mdee aliniambia mimi kama mtayarishaji wa kipindi cha kila siku cha saa mbili kasorobo cha michezo ni wazi taarifa hiyo itahusiana na mambo ya michezo, nilitafakari mwenyewe na bila ya shaka michezo yenyewe itakuwa ya olimpiki, nilijisemea kimoyomoyo.
Siku ile niliona saa zikienda taratibu mno nikiisubiri kwa hamu kubwa simu ya Sam Mdee, haikuja, saa nane haijapigwa, ilipofika saa tisa hivi nikaamua mimi mwenyewe kumpigia Mdee nilikuwa na kimuyemuye. Akaniambia kikao bado kinaendelea.
Ilikuwa karibu ya saa moja na nusu usiku hivi wakati simu ya Sam Mdee ilipokuja na akaniambia “Tido, kikao cha Baraza la Mawaziri kimemalizika hivi punde na kuamua kwamba Tanzania haitashiriki kwenye michezo ya mwaka huu ya Olimpiki huko Montreal kwa sababu kamati ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki (IOC), imekataa pendekezo la kutokuziruhusu kushiriki kwenye michezo hiyo nchi zenye uhusiano wa kimichezo na serikali ya makaburu ya Afrika ya Kusini”. Nilistuka.
Dakika chache baadaye niliitangaza habari hii kwenye kipindi changu cha michezo, huku nikiwa ninatetemeka, lakini dunia ilisikika na punde tu taarifa hii ikawa habari kuu pote duniani.
Usiku ule sikupata usingizi, nikiwaza na kuwazua nini maana ya uamuzi ule uliotuacha sisi tukibakizwa na suti,viatu na masanduku ya kumbukumbu ya Olimpiki. Nilijua hakuna tena la kufanya, ndoto imezima.
Nilingia ofisini RTD, Pugu Road mapema asubuhi siku ya pili lakini ghafla nikapokea simu kutoka Ikulu, nikaambiwa nisubiri, mara nikasikia sauti ya Rais Mwalimu Nyerere, nikajisemea ooh Mungu wangu, kuna nini tena. Nikamwamkia, naye upesi akaniuliza, “Tido unadhani uamuzi wetu wa kujitoa kwenye Olimpiki umepokelewaje na mashabiki wa michezo nchini?” Nilimjibu kwamba, kwa kawaida Watanzania hawana tashwishi na maamuzi yake kwakuwa mara nyingi huyafanya kwasababu ya maslahi mapana ya taifa. Aliniambia, kwa hali ilivyo hivi sasa ni vigumu kuitenga michezo na siasa ya kidiplomasia ya kimataifa. Hata hivyo akasema, amefurahi kwamba tayari kuna viongozi wawili wa nchi za Kiafrika waliompigia simu mara tu baada ya kusikia habari za uamuzi wake na kumwambia na wao watajitoa.
Kwa ujumla baadaye idadi kubwa ya nchi za Kiafrika zilitangaza kuunga mkono uwamuzi huo wa Tanzania kwa kutopeleka timu zao Montreal. Ulikuwa ushindi mkubwa wa kidiplomasia kwa Tanzania. Kwa bahati mbaya mpambano uliosubiriwa kwa hamu wa marudiano baina ya Bayi na Walker katika mbio za mita 1500 ukaota mbawa. Walker akashinda kirahisi. Sikutarajia hata siku moja kupokea simu kutoka kwa Mwalimu Nyerere, siku ile niliogopa. Ilichukua muda kwangu kutulia wakati wa mazungumzo yetu hayo.
Kwa bahati huu ukawa mwanzo wa kupata nafasi nyingine kadhaa za namna hii za mimi kuwasiliana na Mwalimu na hasa baada ya kung’atuka kwake kwenye Uraisi.
Nakumbuka wakati mmoja nikiwa BBC mjini London nilipokea simu kutoka kwa aliyekuwa msaidizi wa Mwalimu, Balozi Charles Sanga aliyeniambia Mwalimu alikuwa anataka kuniona kwenye hoteli aliyokuwa amefikia mjini hapo. Nilifika tukaongea mengi na Mwalimu tukiwa sisi wawili tu, hasa kuhusu yaliyokuwa yakitokea duniani wakati huo.
Hata hivyo kwenye baadhi ya mazungumzo haya wakati mmoja akitoa mfano, aligusia kuhusu uamuzi wake ule aliouchukua wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Montreal 1976. Nilishangaa kwa kumbukumbu ile. Akasema hakujutia na alipendezwa na matokeo yake ya baadaye.
Baada ya kuikosa michezo ya Olimpiki ya Montreal kukawa hakuna jingine kubwa la kufanya hadi 1978 ambapo michezo ya Afrika yaani African games na Jumuiya za madola ilipangwa kufanyika tena ikifuatana ikianza ile ya Afrika iliyofanyika Algiers, Algeria na baadaye Edmonton Canada kwa michezo ya Jumuiya za Madola, Tanzania ikiwakilishwa kikamilifu lakini kwa kiasi kikubwa na wachezaji haohao. ITAENDELEA KESHO
Tido Mhando anafahamika zaidi kwa uongozi wake BBC, TBC, MCL na Azam Media. Lakini kabla ya kufika huko aliwahi kuwa DJ na pia mtangazaji wa michezo akisafiri nchi nyingi duniani na wanamichezo wa Tanzania. Kwenye makala zake hizi tatu za ‘Olimpiki tumevuna tulichopanda’ Tido anachambua kiini cha kuendelea kufeli kwa Tanzania kwenye michezo hiyo. Kwa maoni: 0658 376417