Urusi imevishutumu vikali baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi kwa kuripoti kutoka eneo linalodhibitiwa na vikosi vya Ukraine tangu uvamizi wake wa kushtukiza, na kuanzisha uchunguzi wa uhalifu dhidi ya waandishi habari wa Italia kwa ripoti ya televisheni kutoka eneo hilo.
Urusi yamtaka afisa wa Marekani kulaani vitendo vya waandishi habari
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema ilimtaka Naibu Mkuu wa Ubalozi wa Marekani Stephanie Holmes kutangaza pingamizi kali kuhusiana na vitendo vya uchochezi vya waandishi habari wa Marekani ambao waliingia katika eneo hilo la Kursk kinyume cha sheria.
Soma pia:Zelensky: Wanajeshi wetu wanatimiza malengo yao huko Kursk
Wizara hiyo haikutaja shirika husika la habari lakini imesema inapanga hatua mwafaka za uchunguzi ili kuwachukulia hatua za kisheria waandishi hao.
Wizara hiyo ya mambo ya nje pia imesema vitendo kama hivyo vinaonyesha kuwa Marekani ni mshirika wa moja kwa moja katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine, hoja ambayo Urusi imekuwa ikiitumia kwa muda mrefu kuionyesha Ukraine kama nchi ambayo haifanyi maamuzi yake yenyewe.
Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimechapisha ripoti kutoka Sudzha
Katika siku za hivi karibuni, vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimechapisha ripoti kutoka ndani ya Sudzha, mji mkuu ambao umetekwa na Ukraine.
Zaidi ya watu 122,000 wameondoka katika maeneo ya mpaka ya Kursk
Wizara ya kukabiliana na hali za dharura ya Urusi imesema zaidi ya watu 122,000 wameondoka katika maeneo ya mpaka ya Kursk nchini Ukraine tangu uvamizi wa Ukraine katika eneo hilo.
Artem Sharov, mwakilishi wa wizara hiyo amesema kuwa katika eneo la Kursk, vitengo vya Wizara ya Hali ya Dharura ya Urusi vinaendelea kufanya kazi katika hali ya dharura na kwamba kazi inaendelea ya kuwapa makazi mapya wakaazi katika maeneo ya mipakani na kuwaeka katika maeneo salama.
Ukraine yaidhinisa muswada dhidi ya mashirika yenye uhusiano na Urusi
Katika hatua nyingine, wabunge nchini Ukraine wameidhinisha muswada unaoharamisha mashirika ya kidini yenye uhusiano na Urusi, likiwemo Kanisa la Orthodoks la Ukraine linalohusishwa na Urusi.
Muswada huo ulipongezwa na ofisi ya Zelensky.
Soma pia:Zelensky asema aanajeshi wanazingatia sheria za kiutu wanapozidi kuingia Kursk
Katika ujumbe aliochapisha katika mtandao wa Telegram, mkuu wa watumishi katika ofisi hiyo Andriy Yermak, alisema kuwa hakutakuwa na kanisa la Urusi nchini Ukraine.
Nchini Urusi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Maria Zakharova, amesema Ukraine inajaribu kuharibu Uorthodoksi wa kweli.
Muswada unasubiri kutiwa saini na Rais kuwa sheria
Muswada huo unahitaji kutiwa saini na Rais Volodymyr Zelensky ili kuanza kutumika na utachukua miaka kutekelezwa, lakini bado ulisababisha hali ya wasiwasi miongoni mwa wafuasi wa Kanisa la Orthodoks la Ukraine.