Dar es Salaam. Wanawake wametajwa kuwa mstari wa mbele kuripoti mashauri ya ndoa na kifamilia kuliko wanaume, sababu zikiwa ni ongezeko la talaka, kutafuta mirathi na matunzo ya watoto.
Hayo yamo kwenye ripoti ya msaada wa kisheria ya mwaka 2023 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) leo Jumanne Agosti 20, 2024 jijini Dar es Salaam.
Ripoti hiyo inaonyesha wanaume wanaongoza kwenye kesi za ardhi, ajira, jinai na madai.
Akiizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Utetezi na Mageuzi wa LHRC, Fulgence Massawe amesema kwa mwaka 2023, walipokea wateja 29,491 wakiwa wameongezeka kutoka 18,204 wa mwaka 2022. Kati ya hao wanaume ni asilimia 65 na wanawake asilimia 35.
“Katika kesi za kifamilia 4,578 zilizopokewa, wanawake ni asilimia 65 na wanaume ni asilimia 35. Hali hii inasababishwa na changamoto wanazopitia wanawake, zikiwamo za kisheria kama talaka, ulinzi wa watoto na haki za urithi,” amesema.
Taarifa hiyo inaakisi ongezeko la talaka ambazo Juni 30, 2024 gazeti la Mwananchi liliripoti kuongezeka kwa talaka kutoka 447 mwaka 2022 hadi 866 mwaka 2023, sawa na asilimia 93.7 zilizosajiliwa katika Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita).
Kwa upande mwingine, katika kesi 14,995 zilizopokewa za migogoro ya ardhi, wanaume walikuwa asilimia 66, huku wanawake wakiwa asilimia 34.
“Katika kesi za ardhi wateja wengi walikuwa wanaume kutokana na mila zinazohusisha wanaume na umiliki na udhibiti wa ardhi,” amesema.
Amesema katika kesi hizo kulikuwa na malalamiko ya mipaka (asilimia 29), kuondolewa katika eneo (asilimia 29), kuingia kwenye eneo kijinai (asilimia 26) na migogoro mingine (asilimia 8).
Katika eneo la ajira, amesema walipokea mashauri 3,507 ambayo wanaume wanaongoza kwa asilimia 69 na wanawake asilimia 31. Massawe amesema hali hiyo inaonyesha changamoto wanazopitia wanaume wengi kazini, zikiwemo za mikataba na masuala ya umiliki wa mali.
“Kuna changamoto za kuachishwa kazi, masilahi hasa kikokotoo, kuvunjiwa mikataba na ulinzi wa ajira,” amesema.
Mbali na kesi za ardhi na ajira, Massawe amesema wanaume pia wanashtakiwa zaidi kwenye kesi za jinai kwa asilimia 81 kuliko wanawake (asilimia 19). Amesema wengi wanahusishwa kesi za ubakaji, wizi na ulawiti.
Katika kesi za madai, wanaume wanaongoza kwa asilimia 77, huku wanawake wakiwa asilimia 23.
“Kutofautiana huku kwa wateja kulingana na jinsia kunatokana na mfumo wa kijamii na kiutamaduni, unaochangia kuwepo kwa nafasi ya mtu kufikia mifumo ya haki na uwakilishi wa kisheria,” amesema.
Kwa upande mwingine, Massawe amesema mwaka 2023 walipokea wateja 730 wenye ulemavu, wanaume wakiwa asilimia 75, na wanawake 25. Wengi walizaliwa wakiwa wazima.
Amesema katika mashauri waliyopokea, asilimia 44 yameshinda mahakamani, asilimia 35 yanaendelea na asilimia 21 yamekwama.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Nkasori Sarakikya amesema Serikali inaboresha miundombinu ya huduma za msaada wa kisheria kwa kuwapatia wasaidizi wa kisheria ofisi za Serikali na kuanzisha madawati katika maeneo ya vizuizi na kwenye vituo jumuishi vyote.
Ametoa mfano wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid) inayotekelezwa katika mikoa saba ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Simniyu, Singida na Njombe, akisema jumla ya wananchi 693,638 wamefikiwa.
“Wananchi 7,550 walihudumiwa katika maeneo ya vizuizi na vilevile wananchi 5,245 wamepatiwa huduma za usajili wa matukio muhimu ya binadamu kupitia Rita.
“Kampeni hiyo imepita katika halmashauri 48, kata 520, vijiji 1,539,” amesema.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Anna Henga amesema kituo hicho kinapitia changamoto, zikiwamo za rasilimali watu katika vituo vya kutoa misaada ya kisheria. Pia wateja wao kuombwa rushwa kwenye vyombo vya sheria.
“Tunafananishwa na vyama vya siasa tunapokuwa kwenye kesi za kimkakati, mara wakati mwingine watuite Chadema, ACT-Wazalendo, wakituona na UWT (Umoja wa Wanawake wa CCM) wanasema tumeunga mkono juhudi,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema migogoro ya ndoa na familia inasababishwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
“Jamii imepatwa na tatizo la mmomonyoko na maadili kwa sababu wazazi na walezi wameacha kulea watoto, wamekuwa wakiwafuga. Kufuga ni kuangalia maendeleo ya kibaiolojia, mtoto amekula, akiumwa anapelekwa hospitali analala pa zuri, lakini upande wa kiroho anahitaji malezi bora na ndiyo yamekosekana. Kile kizazi kinachoitwa wazazi leo, jana kilikosa malezi bora,” amesema.
Amesema pia utandawazi umechangia migogoro hiyo, kwani jamii imekuwa na mambo mengi kuliko kuzingatia maadili.
“Nafasi waliyonayo leo vijana katika mitandao ya jamii wanaona mambo mbalimbali ambayo awali yalikuwa ni ya watu maalumu, leo yamekuwa ya watu wote. Mtoto mdogo anashika simu anajua aende wapi aone ambayo hayafai kwake kuona. Maana yake watoto wanakua kabla ya wakati, matokeo yake wanakuwa na tabia chafu,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima amesema wanawake ndio wanabeba jukumu kubwa la malezi katika familia na ndiyo maana wanaguswa zaidi na migogoro katika ndoa.
“Ni wazi katika jamii wanawake wanapokuwa kwenye maisha ya familia ndio wanaobeba zaidi jukumu la malezi, uhai wa watoto na wana uchungu na watoto hasa inapotokea wametelekezwa, wao hawapo tayari kuwaacha. Wao ndio walinzi wa watoto, unajua mama anabeba mtoto kwa miezi tisa, kwa hiyo ukitokea mgogoro wa ndoa ni wazi yeye ndiye atakayeumia zaidi,” amesema.
Akieleza sababu za migogoro ya ndoa kuongezeka, Dk Kitima amesema jamii ya sasa imeacha mila na desturi na imeacha kumcha Mungu.
“Mila na desturi za makabila mbalimbali zilikuwa zinalinda ndoa nyingi kuliko tunavyoona hivi sasa. Siku hizi wanachukuana kutoka kwenye kabila hili na lile na makabila mengine yanapotea, kwa hiyo zile mila na desturi hazipo tena, watu wanakutana huku mjini, kila mtu amekuja kutafuta fursa za maisha,” amesema.
“Pia nguvu ya dini imeachwa kwa uamuzi wa mtu binafsi, dhamira yake ndio inamsukuma kwamba ajali ndoa, awajali watoto. Sasa dini kuwa hiari ya mtu ndiyo inaleta changamoto kwenye taasisi ya familia na hasa ndoa. Ili ndoa idumu isiachwe tu kwenye sheria, bali iunganishwe na desturi na dini, na zile tunu zilizomo zinazomhusisha Mungu.
“Mtu asipomweka Mungu, asipoweka mila na asili ya kwao anaweza asione kwa nini aishi na mtu huyu. Turudi kwenye misingi ya Mungu,” amesema.
Mwanasaikolojia, Jacob Kilimba amesema sababu ya wanawake kulalamikia zaidi masuala ya ndoa na familia ni za kihisia.
“Wanawake ni watu wa hisia na wanaume ni wa kimantiki zaidi. Kwa hiyo vitu vinavyohusiana na hisia vinamgusa zaidi mwanamke. Kwa mfano familia ikitelekezwa, mgogoro ukitokea, mwanamke ndio anabaki na watoto.
“Kwa hiyo suala la kujali watu, liko sana kwa wanawake kwa sababu wamepewa uwezo wa kulea, kuwa na mapenzi na kujali,” amesema.
Amesema wanaume wao ni watendaji zaidi kwa sababu wapo zaidi kwenye vitu, hata watoto wakicheza utaona wa kike wanachukua midoli na wa kiume magari au bastola, akieleza michezo yao inaeleza jinsi wanaume walivyo kwenye vitu.