Watafiti waungana kutafuta mbinu kubaini kifua kikuu kwa watoto

Dar es Salaam. Kutokana na ugumu wa kubaini Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) haraka kwa watoto, watafiti kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda wanafanya utafiti kupata dalili maalumu za kubaini.

Utafiti wa ugonjwa huu unafanyika wakati idadi ya watoto wanaopoteza maisha kwa nchi za Afrika kufikia 322,000 kwa mwaka kuanzia miaka 0 hadi 15 lakini asilimia 96 ya wanaopoteza maisha hawana historia ya kupata matibabu.

Utafiti huu pia, utaihusisha nchi ya Norway na utafanyika kwa miaka minne chini ya mradi wa OPTIC-TB wenye lengo kupambana na kifua kikuu kwa watoto chini ya miaka 10 kwa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mradi huo unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Chuo Kikuu cha Kampala Uganda, Chuo Kikuu cha Catholic Bukavu ya  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Chuo Kikuu cha Bergen kutoka Norway  na Chuo Kikuu Cha Makerere Uganda vyote vitashiriki kwenye utafiti huo.

Akizungumza leo Jumanne, Agosti 20,2024  Jiji Dar es Salaam katika mkutano uliowakutanisha watafiti hao, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  Dk Gunini Kamba amesema utafiti huo utakwenda kuboresha matibabu ya kifua kikuu kwa watoto.

“Tunatamani utafiti uje na majibu yatakayoisaidia Serikali kutengeneza utaratibu wa matibabu kwa watoto, niwaombe watakaofanya utafiti huu watumie uweledi mkubwa,” amesema.

Profesa Yunus Mgaya, Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Kimataifa Kampala -Tanzania, amesema utafiti huo unafanyika kuangalia ubora wa utafiti uliotoa dalili kwa mtoto mwenye ugonjwa wa kifua kikuu kuangalia uthabiti wa matokeo hayo kwenye mazingira halisi.

“Utafiti huu ni muhimu sana kwetu kwa sababu unapunguza vifo na kuongeza kasi na hamasa ya kutoa tiba ya kifua kikuu hasa kwa watoto na vifo vingi tunashuhudia katika ukanda wa Jangwa la Sahara,” amesema.

Profesa Adrew Kutua, Mwenyekiti wa Baraza la NIMR amesema ni faida kubwa kwa nchi hizo tatu kuunganisha nguvu kutafuta ufumbuzi wa kifua kikuu kwa watoto.

“Tunafanya utafiti kwa pamoja juhudi hizi ni kuhakikisha tunapata suluhu ya ugonjwa huu na pia kudhibiti magonjwa yanayozuilika,” amesema.

Naye Mtafiti Mkuu wa mradi OPTIC-TB, Profesa Sayoki Mfinanga amesema utafiti wanaofanya ni wa utaratibu uliotolewa na WHO wa kupima kifua kikuu na kutumia dalili kubaini kifua kikuu ambao utasaidia watoto kuanzishiwa matibabu kwa wakati wanapogundulika mapema na kifua kikuu.

“Utaratibu huu bado haujaingia kwenye mfumo wa kawaida wa afya, sasa huu utafiti tunaokwenda kufanya tumeungana nchi tatu kufanya utafiti wa kutekeleza mpango huu utakaowezesha kugundua wagonjwa kwa wakati na kuwapatia tiba,” amesema.

Profesa Mfinanga amesema kwa sasa utaratibu wa kubaini kifua kikuu kwa watoto kupitia makohozi ni mgumu kwa kuwa na pia hawana dalili jambo linalokwamisha utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo.

Njia hizo za kubaini kifua kikuu  zinajumuisha zana za kisasa za uchunguzi wa molekuli na mfumo wa upimaji wa kina ulioundwa ili kuboresha usahihi wa uchunguzi wa kifua kikuu kwa watoto, hasa katika maeneo yenye upatikanaji mdogo wa mashine za upimaji kama X ray.

Hali ilivyo Tanzania na Kifua kikuu

Takwimu za Wizara ya Afya nchini Tanzania inaonyesha  kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 wagonjwa wa kifua kikuu walioibuliwa ni 400,031, kati yao watoto wakiwa 67,000.

Watu 132, 000, wanaambukizwa ugonjwa huo kila mwaka, huku wengine 25, 800 wakiripotiwa ambao ni wastani wa watu 70 kupoteza  maisha kila siku takwimu zinazoipa Tanzania nafasi ya 30 duniani miongoni mwa nchi yenye wagonjwa wengi duniani.

Pamoja na idadi hiyo kubwa changamoto inayotajwa na Wizara ya Afya ni upatikanaji wa wagonjwa wanaoambukizwa kifua kikuu, bado ni tatizo kwa kuwa asilimia 35 ya wagonjwa hawagunduliki hivyo hukaa nyumbani bila matibabu.

Dalili za kifua kikuu hizi hapa

Ugonjwa huu ambao huambukizwa kwa njia ya hewa dalili zake ni kukohoa damu, homa,kukosa hamu ya kula,kupungua uzito, kutoka jasho kwa wingi wakati wa usiku, uchovu, maumivu makali ya kichwa, maumivu ya kifua na kupumua kwa shida.

Related Posts