Asilimia 3.4 ya watoto Mara wanateswa na utapiamlo mkali

Musoma. Mkoa wa Mara unakabiliwa na changamoto ya utapiamlo mkali kwa watoto walio chini ya miaka mitano kwa kiwango cha asilimia 3.4, huku tatizo la udumavu likiwa ni asilimia 23.4.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, mkoa huo una jumla ya watoto 391,191 wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Agosti 21, 2024 na Kaimu Ofisa Lishe wa Mkoa wa Mara, Grace Martin katika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe kwa mwaka 2023/24 mjini Musoma.

Martin amesema mkoa huo pia unakabiliwa na changamoto ya uzito pungufu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 7.6.

Hata hivyo, amesema licha ya changamoto hizo, mkoa huo umefanya vizuri katika utekelezaji wa mkataba kwa zaidi ya asilimia 95.

Amesema jitihada mbalimbali zinaendelea kufanywa ili kupunguza au kuondokana kabisa na changamoto za udumavu, utapiamlo mkali na uzito pungufu kwa watoto.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka (kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe mkoani Mara katika kipindi cha mwaka 2023/24. Picha na Beldina Nyakeke

Amesema ingawa kiwango cha udumavu kipo kwenye asilimia 23.4, lengo ni kufikia kiwango cha kitaifa cha asilimia 20 na mikakati imewekwa ili kufanikisha hilo, ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya kutambua na kutibu utapiamlo.

Martin amesema suala la kuwa na maofisa lishe wa kutosha ni moja ya vipaumbele vyao huku wakilenga kuwa na maofisa lishe wanne katika kila halmashauri mkoani humo. Amesema kwa sasa kila halmashauri ina ofisa lishe mmoja tu.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesisitiza kufanyika kwa jitihada zaidiĀ  kwa lengo la kuhakikisha mkoa unatekeleza afua za lishe kwa asilimia 100.

Amesema mkoa huo umeimarika sana ikilinganishwa na hali ya awali, ambapo mwaka 2017/18 bajeti ya watoto ilikuwa ikitekelezwa kwa asilimia 18 tu, lakini kwa mwaka huu imefikia asilimia 95 na fedha zinatolewa na kutumika kama zilivyokusudiwa.

Amesema kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji wa afua za lishe, kila halmashauri inatakiwa kutenga Sh1,000 kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano ili kutekeleza masuala mbalimbali ya lishe.

Pia ameuagiza uongozi wa kila wilaya kuhakikisha unatekeleza kiashiria cha siku ya afya na lishe ya kijiji, hatua ambayo itatoa fursa kwa wakazi wa vijiji kupata elimu ya kina kuhusu lishe bora.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka naye amesema nguvu zaidi inapaswa kuelekezwa vijijini ambako udumavu unaonekana kuota mizizi.

Related Posts