Tabora. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kondo Kapinga amefariki dunia baada ya kugongwa na basi la Kampuni ya Mumuki linalofanya safari zake kati ya Mpanda na Arusha.
Ajali hiyo imetokea katika Kijiji cha Ngukumo Kata ya Puge Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wakati Kapinga akiendesha baiskeli.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Agosti 21, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi hilo kuendesha bila kuchukua tahadhari, hivyo kumgonga mwendesha baiskeli huyo na kupoteza maisha.
“Ni kweli Agosti 20 saa 7:20 mchana ilitokea ajali ya basi la Kampuni ya Mumuke lenye usajili namba T 892, lililokua linafanya safari zake Mpanda kwenda Arusha ambapo lilimgonga mwendesha baiskeli aliyefahamika kwa jina la Kando Kapinga na kufariki papohapo, ambapo mwili wake umeshafanyiwa uchunguzi na umeshakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.”
“Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo aliyejulikana kwa jina la Juma Ally kuendesha chombo bila kuchukua tahadhari, ambapo tunamshikilia na tunakamilisha taratibu zote ili afikishwe mahakamani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili,” amesema Kamanda Abwao.
Hata hivyo, amesema baada ya ajali hiyo basi hilo lililokuwa limebeba abiria 57 liliegemea upande na hakuna majeruhi wala madhara yaliyotokea kwa abiria waliokuwamo ndani.
Abwao ametoa wito kwa madereva mkoani humo kuendesha magari yao kwa kufuata sheria za barabarani na watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Tutaendelea kuwachukulia hatua madereva hao ambao wanaendesha magari bila kuchukua tahadhari na mfano mzuri ni dereva aliyegonga watoto wawili Ipuli Tabora, Muksini Tambwe wa Kampuni ya basi la Allys ambaye amehukumiwa kwenda jela miezi sita na faini laki sita na kufungiwa leseni miezi sita ” amesema kamanda huyo.
kwa Upande wake Elizabeth Asegelile ameliomba jeshi hilo kuchukua hatua kali kwa madereva wa Kampuni ya Mumuke akidai husababisha ajali za mara kwa mara kutokana na uzembe.
“Hili basi mpaka sasa limeshaua karibia watu wanne kwenye matukio mawili tofauti, tarehe 19 mwezi wa saba liliua watu watatu lilipogongana na daladala, na hii tena limeua huyu mtu aliyekuwa anaendesha baiskeli, hapana Polisi waimulike vizuri,” amedai Asegelile.