Dar es Salaam. Wazazi, dhana ya ugumu masomo ya sayansi, vimetajwa kusababisha idadi ya wahandisi wanawake kuwa ndogo nchini.
Ambapo idadi ya wahandisi wanawake Tanzania Bara hadi mwaka 2024 wanafikia 5,006 kati ya zaidi ya 38,000 wa kada zote.
Mbali na hizo uwajibikaji, ajira, kutoaminiwa na waajiri, waajiri kuwa na imani haba kwa wahandisi wanawake, kuonewa, maamuzi yasiyo sahihi ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wahandisi wanawake hapa nchini.
Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, leo Agosti 21, 2024 kwenye Kongamano la tisa la Wahandisi Wanawake (Tawece) lililofanyika jijini hapa, wahandisi wanawake wameanika changamoto hizo.
Mwenyekiti mstaafu wa Kitengo cha Wanawake wahandisi Tanzania, Upendo Haule amesema baadhi ya wazazi kuwaeleza mabinti zao uhandisi ni kazi ya wanaume, jambo linalochangia kuwakatisha wengi tamaa kusomea masomo ya sayansi.
Upendo ambaye ni mshauri wa mwenyekiti wa sasa wa kitengo hicho, amesema mkakati wao wa kwanza ni kufanya uhamasishaji wa masomo ya hesabu na sayansi mashuleni.
“Tunapita kuwaambia sisi ni wanawake na tunaweza, kwani wakiwa huko muda mwingine wanapotezana kifikra. Niwashauri wazazi pia wawape moyo wanafunzi kwa kuwa wana nafasi kubwa. Wasiwakatishe tamaa kwani wao ni msingi.”
Amesema, wanafunzi walioacha walikatishwa na wazazi na wanaoendelea wamepewa mioyo na wazazi, hivyo wana nafasi kubwa katika maendeleo ya wahandisi wanawake.
Wakati Upendo akiyaeleza hayo kwa upande wake mhandisi wa umeme, Mensia Gabriel, amesema mabinti wenyewe hawana uthubutu wa kuchukua masomo ya sayansi ambayo ndiyo msingi wa uhandisi.
Amesema wakati mwingine wanajenga hofu kutokana na washauri walionao ,nawaomba wapambane kwani hakuna kitu kigumu ni kujianga na kuamua.”
Aidha ameridhishwa na idadi iliyopo ya wahandisi wanawake akilinganisha na hapo awali ambapo walikuwa wachache. Amesema na Serikali inachangia idadi kukua kutokana na kuwapatia miradi mingi tofauti na awali.
“Hata mimi ni mfano kuna miradi mipya ya uzalishaji wa umeme na mimi ni sehemu na wanawake tupo tunapambana na makandarasi kutoka nje. Kwa kweli Serikali inajitahidi,” amesema.
Mikakati yetu ni kwenda shuleni mfano kwa sasa kuna shule 26 za wanawake zilizojengwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kote nchini.
Changamoto wanazokutana nazo
Mwenyekiti wa Kitengo cha Wanawake cha Taasisi ya Uhandisi Tanzania, Rehana Yahaya amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wahandisi wanawake ni uwajibikaji, ajira kuwa mwiba kutokana na waajiri kutowaamini.
Kuhusu wanafunzi wa kike ameitaja changamoto ni kuozeshwa au kupewa ujauzito. “Wanawake hawashirikishwi, wanakatishwa tamaa, wanaonewa na kuambiwa kuna baadhi ya fani wanaostahili kusoma ni wanaume,”
Kutokana na kauli mbiu ya mwaka huu ya kongamano hilo isemayo ‘Kutumia Nguvu za Wahandisi Wanawake ili Kuendeleza Maendeleo Kuelekea Ulimwengu Endelevu’ imeelezwa mkakati ni kuwainua wahandisi wanawake kwa kuwapatia fursa mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Menye Manga amesema mkakati uliopo unataka hadi kufikia mwaka 2030 wawe wamefikia asilimia 50 kwa 50 kati ya wahandisi wanawake na wanaume.
“Serikali imefungua mlango wa ushirikishwaji wa wahandisi hivyo wanachopaswa ni kuwa tayari kwa kuwa fursa za kushiriki katika miradi ya maendeleo ni kubwa,” amesema.
Ameshauri wakipata mradi wafanye vizuri ili fursa hiyo isipotee huku akiahidi bodi itaendelea kushirikiana na taasisi za kitaaluma za wahandisi kwa ajili ya maendeleo nchini.
Mpango mkakati kuwainua wazawa
Akieleza mikakati ya Serikali, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema hadi sasa wizara yake imeshakamilisha mpango mkakati wa kuwawezesha makandarasi wazawa.
Waziri Bashungwa amesema wamekamilisha mkakati wa kuwawezesha washauri elekezi, makandarasi wazawa na wahandisi wahitimu.
Amesema kutokana na miradi mingi hapo awali kufanywa na wageni Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza uundwe mkakati wa kuwainua wazawa kwa kuwapa miradi.
“Takwimu za fedha zilizokuwa zinakuja sekta ya ujenzi asilimia 60 walikuwa wanapewa makandarasi na washauri elekezi wageni ambao wako chini ya asilimia nne, huku asilimia 96 ya wazawa wakinyang’anyana asilimia 40 ya fedha hizo,” amesema Bashungwa.
Amesema kutokana na hilo Rais Samia alielekeza wizara ije na mkakati huo ambao tayari umekamilika. Amesema mkakati umetengeza fursa ambayo itaanza kutekelezwa mwaka huu.
Ameeleza zaidi Sh840 bilioni zitatumika kuanzia mwezi ujao kujenga miundombinu ya barabara iliyoharibika na mvua za mwaka huu ambazo zitaenda kwa makandarasi wa ndani.
“Sheria ya manunuzi wa umma ya mwaka 2023 imefanyiwa marekebisho na kuongeza ukomo wa kazi kwa wazawa kutoka Sh10 bilioni hadi 50 bilioni,” amebainisha.
Akifafanua changamoto zilizokuwepo amesema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) walikuwa na masharti mengi kwa makandarasi wazawa bila sababu za msingi, sasa zimerekebisha ili kuwajengea uwezo.
“Tumepunguza kiwango cha mapato ghafi pia fedha hizi zilikuwa zinaenda kwa makandarasi wa nje zitabaki kwa wazawa. Watanzania tujiamini kwa kuwa masharti yaliyokuwa mwanzo tumeyatoa,” amesema.
Sambamba na hilo amewapongeza wahandisi wanawake kwa kukutana kila mwaka, akisema umoja huo ni muhimu kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Kongamano hilo litakalofanyika kwa siku mbili limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 900 lina lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa majukumu ya kihandisi hapa Tanzania.