Dagaa waadimika Moshi, walaji wahaha

Moshi. Wafanyabiashara wa dagaa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wameeleza sababu za kupungua kwa bidhaa hiyo kuwa ni ushindani wa wafanyabiashara wakubwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kupungua kwa dagaa katika Ziwa Victoria.

Kauli ya wafanyabiashara hao imekuja ikiwa ni wiki moja tangu kuadimika kwa bidhaa hiyo kwenye viunga vya Manispaa ya Moshi.

Leo, Agosti 21, 2024, Mwananchi Digital imetembelea masoko mbalimbali ya manispaa hiyo, likiwamo la Mbuyuni, Kati na Manyema na kushuhudia uhaba wa bidhaa hiyo.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa dagaa, Emanuel Lui, mmoja wa wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni amesema umeathiri biashara yake.

Amesema sasa hivi gunia moja la dagaa limepanda bei kutoka Sh450,000 hadi Sh700,000.

“Kwa kipindi hiki dagaa wamekuwa adimu sana. Licha ya mabadiliko ya hali ya hewa, wafanyabiashara kutoka Congo wamekuwa wengi sokoni kutokana na mitaji yao kuwa mikubwa,” amesema Lui.

Mfanyabiashara huyo ameongeza kuwa dagaa wengi kutoka Ziwa Victoria na Mafia wanapelekwa Congo, hali inayosababisha upatikanaji wake kuwa mdogo kwa wafanyabiashara wa ndani.

Naye Baraka Simon, mkazi wa Manispaa ya Moshi amesema kupungua kwa dagaa sokoni kunafanya maisha kuwa magumu, akidai ni kitoweo cha gharama nafuu inayoweza kununuliwa hata na wenye kipato cha chini.

Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni, Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro wakiendelea na biashara zao za kila siku. Hata hivyo katika soko hilo upatikanaji wa dagaa umekuwa ni mgumu kutokana na kuadimika kwa bidhaa hiyo.

Mwananchi pia ilizungumza na Sofia Jacob mfanyabiashara wa chakula eneo la Moshi Mjini ambaye amesema kabla ya dagaa kuadimika, alikuwa na uwezo wa kununua dagaa wa Sh1,500 waliotosha kupika kwa siku moja.

Lakini amesema kwa sasa wamepanda bei na hata upatikanaji wake ni wa shida.

“Mwanzoni tulikuwa tunapimiwa dagaa hata wa Sh500, lakini sasa haifai hupati ukiwapata utauziwa kafungu kadogo sana kwa Sh2,000. Hii hali imeathiri biashara zetu kwa sababu huwezi kumpandishia mteja bei ya chakula ghafla,” amesema Sofia.

Naye Jackson Lukumai, mkazi mwingine wa manispaa hiyo, amesema uhaba wa dagaa unawalazimisha kula ugali na tembele badala ya dagaa, jambo linaloongeza changamoto katika maisha yao ya kila siku.

“Dagaa ni bidhaa inayopendwa sana, lakini sasa wamekuwa adimu Moshi, na tunalazimika kula ugali na tembele badala ya dagaa,” amesema Lukumai.

Related Posts