Dawa ya kuongeza nguvu za kiume ilivyomsababisha ashiriki kuua

Arusha. Kweli dunia hadaa, ulimwengu shijaa, kwani kwa hadaa za dunia Mkazi wa Kijiji cha Matandarani Wilaya ya Mpanda, Joseph Adolf au Kisubi, amejikuta akihukumiwa adhabu ya kifo baada ya kushirikiana na mganga wa kienyeji kumuua Juma Shemeli, kwa ahadi ya kupewa dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Kwa mujibu wa mwenendo wa kesi hiyo, mganga huyo, Joseph Petro ambaye Polisi hawakufanikiwa kumkamata, alimuomba Kisubi ambaye walikuwa maswahiba washirikiane kumuua Shemeli ili achukue nyumba na mali za marehemu.

Katika maelezo yake ya onyo yaliyopokelewa mahakamani kama kielelezo, Kisubi alikiri kuhadaiwa na Petro kuwa wakifanikiwa kumuua Shemeli, angempatia dawa hiyo kwa kuwa uume wake ulikuwa hausimami wakati wa kufanya tendo la ndoa.

Hukumu hiyo ilitolewa Agosti 19, 2024 na Jaji Thadeo Mwenempazi baada ya kusikiliza ushahidi wa mashtaka na utetezi wa mshtakiwa, hivyo akasema Mahakama imeridhika kuwa Jamhuri ilithibitisha shtaka pasipo kuacha mashaka kuwa Kisubi alimuua Shemeli.

Inaelezwa mauaji hayo yalitokea Septemba 2, 2020 katika Kijiji cha Matandarani na baada ya mauaji hayo, Kisubi walishirikiana na Petro kuuzika mwili wa marehemu katika shimo la choo nyumbani kwa Petro, aliyefanikiwa kutoroka.

Katika maelezo yake, Kisubi alikiri kufukia mwili wa Shemeli kwenye shimo hilo lililochimbwa kwa ajili ya choo nje ya nyumba ya Petro (mganga) ambaye pia ni rafiki yake, wakidai kuchukizwa na tabia ya marehemu ya kutongoza wake za watu.

Tukio la mauaji lilivyobainika

Katika kesi hiyo Jamhuri iliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Kizito Kitandala na Flavia Shiyo huku mshtakiwa huyo akiwakilishwa na wakili Hamad Amour.

Shahidi wa kwanza, Luhende Manyanya ambaye ni jirani wa marehemu, aliieleza mahakama kwamba kulikuwa na hali isiyo ya kawaida nyumbani kwa marehemu, baada ya kuwaona Kisubi na Petro katika harakati za kuhamisha mali za marehemu.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, aliwaona wawili hao wakiwa wamebeba magunia ya mahindi na mchele kutoka nyumbani kwa Shemeli na alipowauliza, walimjibu kwamba wamenunua nyumba hiyo kwa Sh1.4 milioni.

Pia alisema walimwambia hata hivyo mwenyewe amesafiri kwenda Sumbawanga kumtembelea mganga wa kienyeji.

Alisema walipoulizwa na watu wengine kijijini hapo, walisema amekwenda kutafuta nyumba nyingine ya kuishi.

Luhende alisema hakuridhishwa na majibu hayo, akaamua kumpigia simu Shemeli lakini simu yake haikupatikana, na siku iliyofuata aliwaona tena Kisubi na Petro wakiendelea kutoa mahindi na mchele kutoka nyumbani kwa marehemu.

Aliieleza Mahakama kuwa baadaye  wakaanza kuhamishia vitu vya Petro kwenye nyumba ya marehemu, hapo ndipo alipoamua kuwashirikisha viongozi wa kijiji ili waingilie kati.

Ilidaiwa Septemba 9, 2020 majirani wengine waliamua kukutana nyumbani kwa marehemu na wakaanza kuihoji familia ya mganga huyo, ndipo alipotumia nafasi hiyo kukimbia baada ya kutilia shaka maelezo yao.

Alisema kesho yake walianza kumtafuta Shemeli na walipoenda shambani kwake alikokuwa akilima walimkuta mshtakiwa ambaye pia alisaidia kumtafuta.

Baada ya hapo alipendekeza waanze msako wa nyuma kwa nyumba na kwa kuanzia akasema waanze na nyumba ya mganga.

Wakiwa nyumbani kwa mganga walibaini shimo lililoandaliwa kwa ajili ya kujenga choo, akaomba jembe na kuanza kuchimba na ndipo wakaona mguu wa mtu na kumkamata mshtakiwa huyo.

Shahidi wa nne, Manamba Shimba, alidai kupokea simu na kufahamishwa kwamba Shemeli hayupo na Joseph (mganga) amehamia nyumbani kwake.

Mazungumzo kwenye simu hiyo alimuomba  aende nyumbani hapo akaulize vizuri.

Alisema alifanya hivyo na alipofika aliwauliza wana familia aliowakuta kwa nini wamehamia hapo, wakamjibu kwamba mganga amenunua nyumba hiyo, hakuridhika akaamua kuipeleka familia hiyo kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji.

Shahidi wa pili ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Daniel Maembe alisema alipopata taarifa hizo walipiga simu Polisi na baadaye watu waliokuwa wakimtafuta Shemeli walifika na walipomuhoji Joseph, alikiri kuwa walimuua.

Mmoja wa maofisa wa Polisi waliofika eneo la tukio, H. 751 D/Koplo Kennedy alisema walimkuta mtuhumiwa akiwa amekamatwa tayari na walipomhoji alieleza namna walivyomuua Shemeli na aliwapeleka mpaka walipokuwa wameufukia mwili wake.

Alivyokiri kumuua marehemu

Katika maelezo yake aliyoyaandika Polisi, Kisubi alieleza mwanzo mwisho wa tukio zima la mauaji na ushiriki wake hatua kwa hatua, maelezo hayo yalipokelewa mahakamani kama kielelezo.

“Nakumbuka siku kadhaa nyuma nilikaa na rafiki wa Joseph Petro na kupanga namna ya kumuua Juma Shemeli ili mwenzangu achukue eneo la shamba lake na nyumba kwa kuwa alikuwa amepanga katika nyumba ya Shemeli.”

“Mimi nilitaka kuchukua sehemu ya mgao toka kwake, rafiki yangu aliniahidi tukifanikiwa kumuua mimi atanipatia dawa ya nguvu ya kiume kwa kuwa uume wangu ulikuwa hausimami wakati wa tendo la ndoa kama zamani kipindi nilichofanikiwa kupata watoto wawili na rafiki yangu alikuwa mganga wa jadi,” alikiri.

Alisema Septemba Mosi, 2020 Saa 4:00 usiku baada ya Juma Shemeli kupiga jembe na kuwatangazia wananchi kupeleka watoto kwenye chanjo, yeye alikuwa nyumbani kwa rafiki yake Joseph Petro wakipanga namna ya kumpata Shemeli ili wamuue.

“Ndipo rafiki yangu alienda nyumbani kwake na kumdanganya ampeleke porini kuchimba dawa na baadaye walifika nyumbani akiwa ameongozana na Shemeli, rafiki yangu alichukua fimbo na kumpiga sehemu za kichwani akaanguka chini akafa.”

“Tukamchukua na kwenda kumfukia kwenye shimo lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya choo pale nyumbani kwa rafiki yangu na baada ya kumfukia tuliachana na kukubaliana tuonane kesho asubuhi,” alisimulia mshitakiwa huyo.

Hukumu ya Jaji ilivyokuwa

Katika hukumu yake, Jaji Mwenempazi alisema baada ya kutathimini ushahidi wa maelezo ya onyo ya mshtakiwa, amebaini alikuwa huru na aliweza kufunguka baada ya kuhakikishiwa kuwa yuko katika mikono salama.

Alisema hata kupatikana kwa mwili huo kulitokana na mtuhumiwa ambaye aliwaonyesha watu mahali walipouzika mwili huo na mashahidi wa kwanza, tatu, tano na wa sita walitoa ushahidi kuwa mwili wa marehemu ulitolewa kwenye shimo hilo na mshtakiwa ndiye aliyeuonyesha mwili ulipo.

Huku akinukuu rufaa ya jinai ya Nyerere Nyague dhidi ya Jamhuri, namba 67 ya mwaka 2010 katika ukurasa wa tano hadi sita, mahakama ilisema:-

“Muhusika ambaye atashindwa kumuhoji shahidi juu ya jambo fulani atachukuliwa kuwa amekubali jambo hilo na atazuiwa kuiomba mahakama kutoamini alichosema shahidi,” alisema Jaji akinukuu msimamo wa sheria.

Jaji alisema ukweli huo haukupingwa wakati wowote na kwa mazingira hayo, hana shaka kuwa mshtakiwa huyo alihusika na mauaji ya Juma Shemeli, kitendo alichokifanya pamoja na rafiki yake Petro ambaye anadaiwa kukimbia.

“Kuhusu kama kulikuwa na ubaya uliofikiriwa hapo awali ili kuainisha kitendo hicho kama mauaji, ni wazi katika maelezo ya onyo, kitendo hicho kilipangwa ili rafiki yake achukue nyumba ya marehemu na sehemu ya ardhi,”alisema Jaji.

Jaji Mwenempazi alisema kwa kuzingatia mazingira hayo, mshtakiwa amekutwa na hatia ya kosa la mauaji hivyo anamtia hatiani kwa kosa hilo na adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.

Related Posts